1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya6 Julai 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yanaichambua ziara ya Rais Obama barani Afrika,na pia yanayazungumzia matukio ya nchini Misri na kukamatwa kwa aliekuwa dikteta wa Chad Hissene Habre.

Rais Barack Obama akihutubia CapeTown
Rais Barack Obama akihutubia Cape TownPicha: DW/L. Schadomsky

Juu ya ziara ya Rais Barack Obama barani Afrika gazeti la"Berliner" limeinukuu taarifa ya gazeti la Marekani "New York Times" inayomsifu Rais wa Marekani wa hapo awali George Bush

Gazeti la"Berliner" limeikariri makala ya gazeti la "New YorkTimes" ikisema kwamba nchini Marekani,Bush anaonekana kuwa ni mchochea vita, lakini barani Afrika Bush, anapewa hadhi kubwa .Kwani yeye ndiye alieuzindua mradi wa dola Bilioni 15 wa kuwasaidia watu wenye maradhi ya ukimwi katika bara hilo.

Hata hivyo gazeti la "Berliner Zeitung" linasema katika makala yake kuwa Rais Obama alithibitisha uwezo mkubwa katika ziara yake ya nchi tatu za Afrika.Ziara hiyo ilikuwa kama kampeni ya uchaguzi.Obama aliiwekea kila nchi kipaumbele na kila nchi ilikuwa na mpango wake maalumu.Gazeti la "Berliner" limetilia maanani kwamba Obama alizindua miradi mipya ya maendeleo kwa munufaa ya Afrika na Marekani.

Obama amechelewa kuenda Afrika:

Gazeti la "der Freitag" pia limechapisha makala juu ya ziara ya Rais Obama barani Afrika.Lakini gazeti hilo linasema kuwa Obama amechelewa kuenda Afrika na kwa hivyo itakuwa vigumu kunufaika na raslimali za bara hilo.

Gazeti la "der Freitag" linasema,katika kipindi cha miaka mitano iliyopita viongozi wa China wamekuwa wanatia saini mikataba ya biashara na nchi 30 za Afrika, sambamba na kufadhili miradi ya miundombinu.

Jeshi lamwondoa Mursi:


Gazeti la "Süddeutsche" limechapisha makala juu ya matukio ya nchini Misri.Gazeti hilo limeandika kuwa wafuasi wa aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Mursi walitaka kutumia kila njia ili Mursi aendelee kuwamo madarakani, lakini wanajeshi wa nchi hiyo walikuwa na mpango mwingine.

Na gazeti la"Berliner"limechapisha  makala juu ya Jenerali Abdel Fattah al-Sisi aliemng'oa madarakani Mohammed Mursi baada ya muda uliotolewa na jeshi wa kuutatua mgogoro kupita. Gazeti hilo linatoa wasifu mfupi wa Jenerali huyo ambae pia ni Mkuu wa majeshi na Waziri wa ulinzi.

Jenerali al-Sisi mwenye umri wa miaka 58 alipewa uongozi wa jeshi na Mursi kwa matumaini ya kuzianzisha zama mpya jeshini.Jenerali huyo ni mstadi wa mambo ya vifaru aliepata mafunzo nchini Misri,Saudi Arabia,Uingereza na Marekani. Gazeti la "Berliner" linafahamisha kwamba vyombo vya habari vya nchini Misri vinaeleza kuwa Jenerali al-Sisi hana uzoefu wa vita. Lakini Jenarali huyo ni mtu mwenye uchungu na nchi yake. Huwa anazungumza, machozi yakimtoka juu ya nchi yake.

Lakini Gazeti la "Berliner " linafahamisha kuwa pana madai kwamba Jenerali al-Sisi ni kibaraka wa Marekani. Gazeti hilo linasema tuhuma hizo ni sahihi kutokana na ukweli kwamba jeshi la Misri linapewa msaada wa dola Bilioni1 ,5 kila mwaka na Marekani na kwamba hatua zote muhimu za jeshi la Misri zinajadiliwa kwa pamoja na Marekani.

"Hissene Habre akamatwa:

Gazeti la"die tageszeitung  limechapisha makala juu ya aliekuwa mbabe wa kivita na Rais wa Chad  Hissene Habre ambae sasa amekamatwa nchini Senegal.Gazeti  hilo linaeleza kwamba Hissene Habre aliekuwa anaishi bila ya kujificha nchini Senegal anajulikana kama Pinochet wa Afrika .

Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu,Chini ya utawala wake wa miaka minane nchini Chad watu karibu 40,000 waliuawa ikiwa pamoja na wapinzani wa kisiasa. Hissene Habre alitawala nchini Chad kuanzia mwaka 1982 hadi1990 alipopinduliwa.Gazeti la "die tageszeitung" linasema kukamatwa kwa Hissene Habre kunahusiana sana na ziara ya Rais Obama nchini Senegal.Dikteta huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 70 alikamatwa jumapili iliyopita baada ya kuishi nchini humo kwa muda wa miaka 22 bila ya hata kujificha.    

Hata hivyo gazeti la "die tageszeitung" linasema katika taarifa yake kwamba, Hissene Habre hatafikishwa mahakamani kabla ya mwaka wa 2014 kujibu mashtaka juu ya uhalifu alioutenda.Kulingana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya ICC mjini The Hague,uliopitishwa mwaka uliopita,Hissene Habre anapaswa  kupelekwa kwenye mahakama hiyo au afikishwe mahakamani nchini Senegal.   

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen:

Mhariri:

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW