1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya15 Julai 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya hatua ya pili ya mapinduzi nchini Misri na juu ya kitabu kinachotoa ushauri wa njia za kuupunguza umasikini . NARR:

Mapamabano yanaendelea nchini Misri
Mapambano yanaendelea nchini MisriPicha: DW/M. Sailer

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limefanya mahojiano juu ya hatua ya pili ya mapinduzi nchini Misri .Katika mahojiano hayo mtaalamu wa masuala ya usalama wa Mashariki ya Kati,Mustafa el Labbad anaelezea matumaini yake juu ya mustakabal wa Misri.

Bwana al Labbad kutoka kituo cha Al Sharq cha mjini Cairo kinachoshughulikia masuala ya usalama amesema katika mahojiano hayo kuwa watu wa Misri sasa wameingia katika hatua ya pili ya mapinduzi,na hakuna kurudi nyuma.

Mtaalamu huyo ameeleza kuwa chama cha Udugu wa Kiislamu hakina nguvu ya kuyarudisha mambo nyuma nchini Misri na kwa hivyo hatimaye chama hicho kitakubaliana na hali halisi ya kisiasa nchini Misri.

Uchumi mbaya:

Gazeti la"Süddeutsche" limechapisha muhtasari wa kitabu kinachoitwa "uchumi mbaya" Poor Economics. Katika kitabu hicho waandishi wanatoa ushauri juu ya njia za kupambana na umasikini. Waandishi hao Abhijit Banerjee na mwanzake Esther Dulfo wanaonyesha katika kitabu chao jinsi masikini wanavyofikiria.Wanatoa mfano wa maskini wa Afrika na India.

Waandishi hao wanaeleza kuwa mara nyingi masikini,pia wa barani Afrika wanaipinga mipango au miradi ya wataalamu yenye lengo la kuwasaidia. Katika kitabu chao, Abhijit Banerjee na Esther Duflo wanabainisha kwamba mtazamo wa masikini ni muhimu sana katika juhudi za kupambana na umasikini.Wanatoa mfano wa huduma ya chanjo .

Wanasema mashirika au serikali, wakati mwingine zinajaribu kutoa huduma hiyo kwa masikini barani Afrika, lakini hakuna anaekwenda .Matokeo yake maskini hao hulipa gharama kubwa zaidi, pale panapotokea maradhi. Badala ya kukinga, masikini wanaingia katika mtego wa kutibu kwa gharama kubwa.

Katika kitabu hicho waandishi wanajaribu kusisitiza umuhimu wa kuwaelekeza masikini barani Afrika katika kupitisha maamuzi sahihi katika harakati za kuondokana na umasikini.

Ujerumani na Somalia:

Gazeti la "Die Welt" limechapisha makala juu ya Ujerumani na Somalia. Gazeti hilo limemnukulu Waziri wa ulinzi Thomas de Maizere akisema kwamba mtu anahitaji kuwa na subira sana anapokuwa na shughuli na Afrika. Gazeti hilo linaifafanua kauli Waziri de Maizere.

Kwa muda wa zaidi ya miaka 20 Somalia ilihesabika kuwa ni taifa lisilofanya kazi.Kila kitu kilianguka.Lakini sasa hali imekuwa bora,na ipo serikali nchini Somalia inayofanya kazi. Hali hiyo imetokana na mchango wa majeshi ya nchi za Umoja wa Afrika nchini katika kulinda amani nchini humo. Majeshi hayo yanadhibiti usalama pia nje ya mji mkuu, Mogadishu.


Gazeti la "Die Welt" linatilia maanani kwamba nchi za Umoja wa Ulaya ikiwa pamoja na Ujerumani zimetoa mchango mkubwa kwa kutoa mafunzo kwa askari wa Somalia,chini ya mradi unaoitwa EUTM-yaani mradi wa mafunzo yanayotolewa na Umoja wa Ulaya nchini Uganda.

Gazeti la "Die Welt" limefahamisha kwamba sasa Ujerumani inakataa kusema iwapo itawapeleka wawakilishi wake mjini Mogadisho kwenye ofisi ya Umoja wa Ulaya ya mafunzo kwa ajili ya askari wa Somalia. Limemkariri Waziri wa ulinzi wa Ujerumani de Maizere akisema kwamba mtu anahitaji kuwa na subira anapofanyakazi na Afrika.

Mvuvi wa kisomali aliefungwa jela kwa makosa nchini Ufaransa:

Gazeti la "Süddeutsche linatupasha habari juu ya mkasa wa mvuvi mmoja wa kisomali. Wafaransa walimfunga jela mvuvi huyo kwa kumfikiria kuwa ni haramia. Kosa alilolifanya ni kuwa pamoja na watu waliokuwa wanagawana kitita cha fedha kilichotokana na kuiteka nyara meli moja ya abiria ya Wafaransa. mnamo mwaka 2008. Mmiliki wa meli aliwalipa maharamia zaidi ya dola Milioni 2.

Gazeti limearifu kuwa mvuvi huyo Abdulkader Guled Said alipanda gari la maharamia ili kwenda sehemu yenye samaki wengi zaidi. Lakini njiani gari hilo lisimamishwa na helikopta ya Ufaransa. Askari wa Ufaransa walizipata,ndani ya gari sehemu ya fedha zilizolipwa na mmiliki wa meli iliyotekwa nyara,Na ndipo walipowakamata wote waliokuwamo ndani ya gari pamoja na mvuvi huyo aliepelekwa katika jela ya Fleury-Merogis kusini mwa mji wa Paris.Sasa ameachiwa baada ya kuwa jela kwa miaka kadhaa.

Mwandishi:Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW