1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya27 Septemba 2013

Magazeti karibu yote ya Ujerumani wiki hii yamechapisha makala juu ya matukio ya nchini Kenya na pia yameandika juu ya kuthibitishwa kwa adhabu ya kifungo cha aliekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.Picha: John Muchucha/AFP/Getty Images

Gazeti la "Süddeutsche " limeandika juu ya ugaidi wa kundi la al-Shabaab nchini Kenya. Gazeti hilo limeandika kwamba watu wa Kenya wanaomboleza vifo vya raia zaidi ya 60 wa nchi hiyo na wa kutoka nje waliouawa kutokana na utekaji nyara uliofanywa na magaidi wa kundi la kisomali la al-Shabaab kwenye duka kubwa la Westgate katika mji wa Nairobi.

Gazeti la "Süddeutsche" linasema haijulikani kwa uhakika ni watu wangapi waliokufa kutokana na mkasa huo. Wakati serikali ya Kenya inasema waliouawa ni watu 61, magaidi wa al-Shabaab wanadai kwamba mateka zaidi ya 130 waliuawa.

Gazeti la "Süddeutsche" pia linasema katika makala yake kwamba mkasa huo wa ugaidi utabaubadilisha mtazamo wa nchi za magharibi juu ya Rais Uhuru Kenyatta. Kwani mpaka sasa uhusiano wake na viongozi wa nchi za magharibi umekuwa wa kiwango cha chini kutokana na madai yanayomkabili ya kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu. Kutokana na ugaidi uliofanywa na kundi la al-Shabaab, viongozi wa nchi za magharibi wameonyesha mshikamano na Rais Kenyatta.Gazeti la "Süddeutsche" limetilia maanani kwamba jumapili iliyopita Rais Barack Obama alizungumza na Rais Kenyatta kwa njia ya simu.

Ugaidi umebadilika :changamoto kwa wote

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linakumbusha kwamba ugaidi umerudi tena Afrika Mashariki pale pale ulipotokea miaka 15 iliyopita.Na linaeleza kwamba katika miaka hiyo 15 ugaidi umebadlika. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema ugaidi sasa ni changamoto kubwa kwa wote. Haijawahi kutokea kwamba magaidi kutoka mataifa mbalimbali wanaungana ili kufanya mashambulio kama ilivyotokea mjini Nairobi, kwani walioshiriki hawakuwa tu magaidi wa kisomali, bali pia walikuwamo wamarekani na waingereza.

Rufani ya Charles Taylor yakataliwa
Gazeti la"die tageszeitung" limechapisha makala juu ya aliekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor ambae kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 50 jela baada ya kupatikana na hatia ya kutenda uhalifu wa kivita. Gazeti la "die tageszeitung" limeanza makala yake kwa kusema kwamba Taylor ataendelea kutumikia kifungo jela. Gazeti hilo linaeleza kuwa Mahakama maalumu inayosikiliza kesi juu ya Sierra Leone imeithibitisha adhabu ya kifungo cha miaka 50 jela kwa Charles Taylor.

Gazeti la "die tageszeitung"limearifu kwamba mahakimu wameridhika na ushahidi kwamba alipokuwa Rais wa Liberia Taylor aliwapa silaha waasi katika nchi jirani ya Sierra Leone kwa malipo ya" almasi za damu." Taylor pia aliyapeleka majeshi Sierra Leone wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Charles Taylor alitaka rufani kupinga adhabu aliyopewa, lakini mahakimu wameithibitisha adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 50 jela.

Faru hatarini kumalizwa barani Afrika

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii pia limeandika juu ya hatati ya kutoweka kwa faru kutokana na uhalifu wa majangili. Gazeti hilo linaarifu kwamba majangili wamewaua faru karibu 688 mnamo mwaka huu barani Afrika. Gazeti la "die tageszeitung"limeikariri taarifa ya serikali ya Afrika Kusini inayosema kuwa idadi hiyo maana yake ni ongezeko la faru 20 kulinganisha na idadi ya mwaka wa 2012.Gazeti la "die tageszeitung" linasema kuwa pembe za wanyama hao zinamezewa mate sana katika nchi za Asia. Msemaji wa shirika la ulinzi wa wanyamapori Roland Gramling amesema njia ya kufaa ya kuukomesha uhalifu wa majangili ni kuzuia biashara ya vipusa katika nchi za Asia. Pembe za faru zinazingatiwa kuwa tiba ya ajabu katika nchi hizo.Gazeti la"die tageszeitung"limearifu kuwa ujangili wa faru umeongezeka sana barani Afrika katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW