Afrika katika magazeti ya Ujerumani
18 Oktoba 2013Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema nchi za Afrika zinahitaji kupewa msaada wa maana ili kuziwezesha kukabiliana na tatizo la wakimbizi.Linahoji kwamba yapo masuala yanayopaswa kuzingatiwa kwa makini. Gazeti hilo linahoji kuwa yapo masuala ya msingi barani Afrika yanayosababisha tatizo la ukimbizi. Kuanzia utawala mbaya katika nchi nyingi, hadi kushindwa kufanya kazi vizuri kwa serikali.Pili ni tatizo la idadi kubwa ya watu.Bara la Afrika sasa lina watu zaidi ya Bilioni moja. Na kila mwaka wanaongezeka watu Milioni 36 katika bara hilo.
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema hata ikiwa bara la Ulaya litawachukua wakimbizi milioni moja kila mwaka kutoka Afrika,tatizo litakuwa bado halijatatuliwa. Gazeti hilo linasema bara la Afrika linahitaji msaada wa maana kutoka Ulaya ili liweze kuyatatua matatizo yake.
Gazeti linaloitwa "Freitag" pia linazungumzia juu ya tatizo la wakimbizi katika muktadha wa maafa makubwa yaliyotokea katika bahari ya Mediterania ambapo mamia ya wakimbizi walikufa maji baada ya mashua yao kuzama. Mwandishi wa makala ,Helon Habila anasema katika makala yake kwamba bara la Afrika limenyamaza kimya juu ya maafa hayo. Mwandishi huyo anasema,katika nchi za Afrika ambako wakimbizi walitokea hakuna anaesema chochote.
Mwandishsi huyo anasema labda viongozi wa Afrika wametingwa na matatizo yao ya kibinafsi.Umoja wa Afrika haujasema ni hatua gani unakusudia kuchukua ili kulikabili tatizo la ukimbizi.
Mwandishi wa gazeti la "Fritag" anasema , wanasiasa, wafanyabiashara,watu wa tabaka la kati na vijana wanaowakilisha matumaini ya Afrika ya kesho, wanaona ni bora kuzungumzia juu ya masuala ya ustawi wa uchumi na njia za kuwavutia wawekaji vitega uchumi.
Afrika na Mahakama ya Kimataifa
Gazeti la "Neues Deutschland" limechapisha makala juu ya mvutano baina ya nchi za Umoja wa Afrika na Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague. Gazeti hilo linaeleza kwamba uhusiano baina ya nchi za Afrika na Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague umekuwa wa mvutano katika miaka ya hivi karibuni. Sababu ni kwamba mwendesha mashtaka mkuu wa hapo awali Moreno Ocampo alidaiwa kuwa mtu aliekuwa anawaandama wahalifu kutoka Afrika tu.
Gazeti la "Neues Deutschland" linasema Umoja wa Afrika unamlaumu Ocampo kwa kuiongoza mahakama ya mjini The Hague kwa kuzitumia itikadi za kibeberu wakati alipokuwa mwendesha mashtaka mkuu. Gazeti la "Neues Deutschland" linauliza katika makala yake, jee Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague inakaribia mwisho? Gazeti hilo linatilia maanani kwamba kwenye mkutano wao wa kilele mjini Addis Ababa hivi karibuni viongozi wa Umoja wa Afrika waliitaka Mahakama ya Kimataifa iache kuzihukumu kesi zinazowakabili Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto na izihamishie kesi hizo barani Afrika.
Tuzo isiyokuwa na mpokeaji
Gazeti la "Berliner" limeandika makala yenye kichwa cha habari kinachosema "tuzo isiyokuwa na mpokeaji" Makala hiyo inahusu tuzo ya Mo Ibrahim inayotolewa kwa viongozi wastaafu wa Afrika waliofanya kazi nzuri walipokuwa madarakani.Lakini safari hii pia hakupatikana wa kuipokea tuzo hiyo inayoambatana na donge nene. Gazeti la "Berliner" linaeleza kuwa mwaka huu vile vile hakupatikana mpokeaji wa tuzo ya utawala bora ya Mo Ibrahim.Hii sasa ni mara ya nne .Gazeti hilo linaeleza kuwa masharti ya kutunukiwa tuzo hiyo ni ya juu sana. Ndiyo sababu gazeti la "Berliner"limelikariri jarida la Internet la Afrika Kusini-"Daily Maverick" lililopendekeza kuitoa tuzo hiyo kwa pia kwa wakuu wa mashirika yasiyo ya kiserikali,kwani watu wanaotenda mema barani Afrika wamejaa ila tu wao siyo marais wa nchi.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Yusuf Saumu