Afrika katika magazeti ya Ujerumani
17 Januari 2014Gazeti la "Neues Deutschland"limeandika juu ya mgogoro wa Sudan Kusini.
Gazeti hilo linatilia maanani kwamba mazungumzo yanayofanyika mjini Addis Ababa juu ya kuutatua mgogoro huo ni magumu.Gazeti la "Neues Deutschland" linaeleza katika makala yake.kwamba licha ya juhudi kubwa ,ikiwa pamoja na kufanya mazungumzo ya kuleta amani mapigano bado yanaendelea baina ya majeshi ya serikali na ya waasi.Gazeti la "Neues Deutschland" linatilia maanani kwamba kikwazo kimojawapo kikubwa cha mafanikio kwenye mazungumzo ya mjini Addis Ababa ni watu wa upande wa waasi waliotiwa ndani.
Watu hao wa kiongozi wa uasi ,Riek Machar, aliekuwa makamu wa Rais wanatuhumiwa kuhusika na jaribio la kuiangusha serikali. Waasi wanataka watu wao waachiwe ili mazungumzo yaweze kusonga mbele.
Msimamo wa China wabadilika
Gazeti la "Berliner Zeitung" linatahadharisha kwamba migogoro inayotokea barani Afrika kama vile nchini Sudan Kusini, inayahatarisha maslahi ya kiuchumi ya China katika bara hilo.Gazeti hilo linasema hadi sasa China imekuwa inafanya biashara na nchi za Afrika bila ya kujiingiza katika mambo ya ndani ya nchi hizo.Lakini gazeti hilo linasema sera hiyo imeanza kubadilika.
Gazeti la "Berliner Zeitung" linaeleza kwamba wajumbe kutoka China wanalizuru bara la Afrika wakiwa na makasha ya fedha. China inajenga barabara, hospitali, shule na viwanja vya ndege katika nchi kadhaa za Afrika. Na kwa ajili ya kuijenga hali nzuri ya kibiashara China inazisamehe madeni nchi za Afrika.
Gazeti la "Berliner Zeitung" linatilia maanani katika makala yake kwamba hadi hivi karibuni ,China haikujiingiza katika mambo ya ndani ya Afrika. Lakini sasa mambo yamebadilika. Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi alikutana na wawakilishi wa serikali na wa waasi wa Sudan Kusini wakati wa ziara yake nchini Ethiopia.
Japan na Afrika
Gazeti la "Neues Deutschland" wiki hii pia limeandika juu ya ziara aliyoifanya Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe barani Afrika. Juu ya ziara hiyo gazeti hilo linasema kwa muda mrefu China imekuwa inajitandaza barani Afrika bila ya ushindani.Lakini sasa China inaanza kupata ushindani mkubwa wa Japan.
Gazeti hilo limearifu kuwa Waziri Mkuu Shinzo Abe ameenda Afrika na dola Bilioni 14 za misaada na mikopo. Hata hivyo gazeti la" Neues Deutschland" linasema Japan haitoi fedha hizo kutokana na moyo wa hisani tu. Limemnukulu Waziri Mkuu Shinzo Abe akitabiri kuwa bara la Afrika litakuwa kitovu cha ustawi katika miaka ijayo.
Gazeti la "Neues Deutschland" limearifu kwamba China imekasirishwa na ziara ya Waziri Mkuu wa Japan barani Afrika. Limemnukulu Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi akisema kuwa Japan inalenga shabaha za kisiasa barani Afrika.
Gazeti la "die tageszeitung" limeandika juu ya kuuliwa kwa aliekuwa mkuu wa ujasusi wa Rwanda Patrick Karegeya nchini Afrika Kusini. Alikutwa kitandani amenyongwa usiku wa tarehe 2 januari. Gazeti la " die tageszeitung" limemnukulu balozi wa Rwanda nchini Uingereza William Nkurunziza akisema kuwa Karegeya alikuwa adui wa nchi. Karegeya aliekuwa anaishi katika hifadhi ya kisiasa nchini Afrika Kusini alikuwa mpinzani wa serikali.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Josephat Charo