Afrika katika magazeti ya Ujerumani
14 Februari 2014Gazeti la "Berliner" limeandika juu ya baa la ujangili barani Afrika.
Gazeti hilo limeandika katika makala yake kwamba ujangili unawamaliza wanyama pori barani Afrika. Gazeti la "Berliner" limeandika: Maalfu ya ndovu wanauliwa na majangili kila mwaka barani Afrika kutokana na mahitaji ya pembe za wanyama huo kuongezeka hasa katika nchi za Asia. Gazeti la "Berliner" linaeleza katika makala yake kwamba viumbe hao wanauliwa kwa njia za ukatili mkubwa.
Gazeti la "Berliner" limemnukuu jangili mmoja John Sumokwo kutoka Kenya akisema kuwa wakati wote "nilikuwa na mikuki miwili.Ikiwa mkuki mmoja haukuingia vizuri katika mwili wa tembo basi nilitupisha mwingine.Nilipajua vizuri pale ulipokuwapo moyo wa tembo. Nilipompiga mkuki katika sehemu hiyo alianguka mara moja. Tulipata fedha nyingi kutokana na biashara ya pembe za ndovu". Gazeti la Berliner limearifu kuwa jangili huyo John Sumwoko alipewa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja tu jela licha ya uhalifu mkubwa alioufanya.
Ndovu wanamalizika Tanzania
Gazeti la "Berliner" pia limezungumzia juu ya ndovu wa Tanzania.
Limearifu kwamba miaka mitano tu iliyopita mbuga ya Selous ilikuwa na tembo alfu sabini lakini sasa wamebakia alfu13 tu. Gazeti hilo limemnukuu mchapishaji wa gazeti la mambo ya ikolojia ,Zac Goldsmith akisema kwamba ikiwa mauaji ya ndovu yataendelea kwa kasi iliyopo sasa, basi katika kipindi cha miaka 5 ijayo Tanzania haitakuwa na tembo tena. Gazeti la Berliner pia limeripoti juu ya mkutano wa kimataifa uliofanyika mjini London kujadili njia za kupambana na ujangili.
"Berliner Zeitung" limefahamisha kwamba wajumbe kutoka nchi zaidi ya 40 walishiriki kwenye mkutano huo ikiwa pamoja na kutoka China nchi ambako meno ya ndovu na pembe za faru zinanunuliwa sana.
Wanajeshi wa Ujerumani kupelekwa Somalia
Gazeti la "Süddeutsche" wiki hii limeandika maoni juu ya Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen. Gazeti hilo linasema waziri huyo ameyasema mengi juu ya Afrika hivi karibuni.Gazeti hilo linaeleza katika maoni yake kwamba Waziri von der Leyen pia amezungumzia juu ya kuwapeleka askari wa Ujerumani nchini Somalia.
Jee askari hao wanaenda kufanya nini? Jukumu lao litakuwa kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Somalia. Na kwa sababu Somalia inahitaji wanajeshi stadi, aliyoyasema waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen ni sahihi.Gazeti la"Suddeutsche" limeeleza kwamba wanajeshi 20 wa Ujerumani watarudishwa Somalia kwa sababu hali ya usalama sasa ni nzuri.
Umoja wa Ulaya kupeleka majeshi Jamhuri ya Afrika ya Kati
Mauaji bado yanaendelea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati licha ya uwepo wa majeshi ya Ufaransa na ya Afrika katika nchi hiyo. Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya Umoja wa Ulaya unapanga kupeleka majeshi.Gazeti la "die tageszeitung" linaarifu zaidi. Umoja wa Ulaya umeanza matayarisho thabiti ya kupeleka majeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mnamo mwezi wa mei.
Kwenye mkutano uliofanyika Alhamisi iliyopita,Umoja wa Ulaya uliamua juu ya nchi zitakazochangia askari watakaopelekwa katika Afrika ya Kati. Nchi hizo tisa ni pamoja na Ujerumani na Uingereza.Kamanda wa majeshi hayo atatoka Ufaransa.
Hata hivyo katika taarifa yake gazeti la "die tageszeitung" linasema hadi mwezi wa Mei mambo yanaweza kuwa yamechelewa kwa Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Umoja wa Ulaya unakusudia kuwapeleka jumla ya askari 500.
Gazeti la "die tageszeitung" limemnukuu Kamishna wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisema kuwa kiwango cha maafa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, hakina mithili na kwamba lazima jumuiya ya kimataifa iingilie kati kijeshi nchini humo.
Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Yusuf Saumu