Afrika katika magazeti ya Ujerumani
28 Machi 2014Gazeti la "Das Parliament" limeandika juu ya uhusiano baina ya bara la Afrika na Umoja wa Ulaya. Gazeti hilo limeandika juu ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Afrika na wa Umoja wa Ulaya.
Linasema katika makala yake kwamba bara la Afrika, jirani wa Ulaya ambalo limekuwa linasahauliwa kwa muda mrefu sasa linazidi kuwa muhimu kwa nchi za Ulaya.Viongozi wa nchi za Ulaya na wa Afrika watakutana tena mnamo wa Aprili. Umuhimu wa Afrika kwa nchi za Ulaya unaonekana katika kauli za wabunge wa Ujerumani wanaosema kwamba uhusiano baina ya Afrika na Ulaya usiwe tu katika ushirikiano wa kijeshi.
Afrika yataka mkataba wa EPA ujadiliwe upya
Hata hivyo gazeti la "Das Parliament" linatilia maanani kwamba nchi za Afrika zinataka mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi EPA ujadiliwe tena. Sababu ni kwamba ,ikiwa muundo uliopo sasa utaendelea kama ulivyo,itakuwa vigumu kwa nchi za Afrika kuingia katika soko la Umoja wa Ulaya.
Gazeti la "Süddeutsche" linaiangalia ziara ya Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika nchi tatu za Afrika. Nchi hizo ni Ethiopia,Tanzania na Angola.
Gazeti "Süddeutsche linasema Waziri Steinmeier amefanya ziara barani Afrika na kwa hivyo Ujerumani inapaswa kuwa na mkakati mpya kuhusu bara hilo. Lakini swali ni iwapo Ujerumani itaweza kuutekeleza mkakati huo mpya.
Gazeti la "Süddeutsche" limemnukuu Waziri Steinmeier akisema kwamba bara la Afrika limepiga hatua kubwa ya mandeleo katika miaka ya hivi karibuni japo bado ipo migogoro ya hapa na pale kama vile nchini Mali,katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini. Waziri Steinmeier ametilia maanani ustawi wa uchumi wa haraka barani Afrika.
Meli ya kihistoria " Liemba"
Gazeti la Süddeutsche" pia limeripoti kwamba katika ziara yake nchini Tanzania Waziri Steinmeier pia alizungumzia juu ya meli ya miaka mingi, SS Liemba ambayo ni ishara ya historia ndefu ya uhusiano baina ya Tanzanzia na Ujerumani. Meli hiyo sasa itafanyiwa ukarabati na ndiyo sababu katika ujumbe wake Waziri Steinmeier aliongozana na meneja wa kampuni ya Ujerumani ya uundaji wa meli "Meyer Werft"
Miaka 20 tokea mauaji ya Rwanda,Umoja wa Mataifa ulikuwa wapi?
Gazeti la "Die Zeit" limeandika juu ya Rwanda ambayo kwa sasa imo katika matayarisho ya kuyakumbuka mauaji halaiki yaliyotokea katika nchi hiyo miaka 20 iliyopita.
Gazeti la "Die Zeit" linakumbusha katika makala yake kwamba wakati mbunge wa Marekani Patricia Schröder alipoulizwa mwishoni mwa mwaka wa 1994, kwa nini Marekani haikujishughulisha zaidi ili kuyakomesha mauaji nchini Rwanda mbunge huyo alijibu kwa kusema kwamba mamia ya wapiga kura wake nchini Marekani walimpigia simu kuonyesha wasi wasi mkubwa zaidi juu ya sokwe wa Rwanda kuliko juu ya binadamu.
Gazeti la "Die Zeit" linakumbusha katika makala yake kwamba miaka 20 iliyopita, kati ya mwezi wa Aprili na Juni, watu 800,000 waliuawa .Gazeti hilo linasema kwamba katika kuyakumbuka mauaji hayo viongozi wa Rwanda pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa mara nyingine watatoa maazimio juu ya kuhakikisha kwamba maafa kama hayo hayatokei tena.
Lakini gazeti la "Die Zeit " limesema kuwa wanaharakati pia watakumbusha jinsi Umoja wa Mataifa ulivyoshindwa kuyazuia mauaji hayo.
Wakulima wa Afrika watiliwe maanani, asema dada yake Obama
Dada yake Rais Obama wa nyumba ndogo,Auma anataka wakulima wa Afrika watiliwe maanani. Hiyo ni taarifa ya gazeti la "der Freitag".
Gazeti hilo linaarifu kwamba Auma Obama, mwasisi wa wakfu unaoitwa "Sauti Kuu" nchini Kenya ametoa mwito wa kuwatilia maanani wakulima wa Afrika.Auma alikuwa anazungumza kwenye mkutano juu ya biashara ya haki uliofanyika mjini Berlin. Amesema Waafrika hawahitaji kupewa makombo bali wanahitaji biashara ya haki.
Mwandishi:Mtullya Abdu
Mhariri:Yusuf Saumu