Afrika katika magazeti ya Ujerumani
11 Mei 2014Gazeti la "Süddeutsche" linauzungumzia mkasa wa kutekwa nyara wasichana zaidi ya mia mbili nchini Nigeria. Gazeti hilo linasema ,kutekwa nyara kwa wasichana hao na magaidi wa kundi la Boko Haram kumemshtua kila mtu.Gazeti la "Süddeutsche limemnukuu Rais Goodluck Jonathan akisema kwamba jeshi la Nigeria linazo nguvu za kutosha za kuweza kuwakabili waliowateka nyara wasichana hao.
Kauli ya Rais yatuliza lakini ...
Lakini gazeti la "Süddeutsche " linasema yumkini kauli ya Rais Jonathan imewatuliza wazazi na ndugu wa watoto hao, na huenda pia imewaliwaza waliotekwa nyara. Lakini viongozi wa Nigeria walipaswa kuwa na busara ya kuitambua hatari inayotokana na kundi la Waislamu wenye itikadi kali, la Boko Haram, na kupiga mbiu ya mgambo siku nyingi.Lingekuwa shauri zuri kwa viongozi wa Nigeria kuchukua hatua ya kuuchunguza mzizi wa ugaidi ili kulipata jawabu la haraka.
ANC yashinda tena kwa kishindo
Gazeti la "die tageszeitung limeandika juu ya uchaguzi uliofanyika nchini Afrika Kusini mapema wiki hii. Katika makala yake gazeti hilo limesema kuwa, mshindi alijulikana tokea mapema kabisa- chama kinachotawala ,ANC. Hata hivyo gazeti la "die tageszeitung" linasema kwa chama cha Rais Jacob Zuma kilichohusu, hasa historia ya Nelson Mandela kuliko mustakabal wa nchi.Rais Zuma ameisheherekea historia ya chama chake.
Gazeti la "die tageszeitung" linatilia maanani kwamba katika utawala wake Zuma hakusababisha madhara makubwa kama ilivyohofiwa na watu wengi. Hayo yalitosheleza kumletea ushindi thabiti, lakini hayatoshi katika kutoa uhakika wa mustakabal wa nchi.
Waziri Gerd Müller asema inawezekana kuwalisha wote
Gazeti la "Frankfrter Allgemeine" limechapisha makala juu ya Waziri wa Ujerumani anaesimamia ushirikiano wa maendeleo, Gerd Müller. Gazeti hilo limeandika juu ya mipango ya waziri huyo.
Limemnukuu Waziri Müller akisema kuwa ni kashfa kubwa kuendelea kuwapo njaa duniani. Amesema ardhi iliyopo inaweza kutoa chakula cha kutosha kwa ajili ya watu Bilioni kumi.
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limefahamisha kwamba Waziri wa ushirikiano wa maendeleo anapanga kuanzisha vituo kumi vya kilimo barani Afrika ili kuhakikisha kwamba njia inayotoka shambani inaelekea moja kwa moja kwenye meza ya chakula. Na kwa ajili hiyo wizara yake itaekeza katika shule na mafunzo.
Bara la matumaini
Bara la Afrika linazingatiwa kuwa soko la mwisho la siku za usoni duniani. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Die Zeit" mnamo wiki hii.Hata hivyo gazeti hilo linatahadharisha kwamba anaetaka kuekeza vitega uchumi katika bara hilo anahitaji kuwa na moyo wa ujasiri.
Gazeti hilo linaeleza kwamba bara la Afrika linaonyesha matumaini makubwa ya siku za usoni kama jinsi ilivyokuwa kwa nchi zinazoinukia kiuchumi, miaka 20 hadi 30 iliyopita. Lakini jambo muhimu ni kuchagua vizuri pale pa kuekeza vitega uchumi .
Takwimu zinaonyesha kwamba nchi za Afrika za kusini mwa jangwa la Sahara zitafikia ustawi wa uchumi wa hadi asilimia 5.5 mnamo mwaka huu. Gazeti la "Die Zeit" linasema katika makala yake kwamba nchi kama Kenya,Ghana na Nigeria zinahesabika kuwa miongoni mwa mataifa yanayoinukia kiuchumi. Hata hivyo gazeti hilo linatahadharisha kwamba mashaka ya kisiasa bado yapo na haifai kuyapuuza.
Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Yusuf Saumu