1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya22 Agosti 2014

Wiki hii magazeti karibu yote ya Ujerumani yameandika juu ya maradhi ya Ebola yaliyoripuka tena barani Afrika. Magazeti hayo pia yameandika juu ya vita vya kiwakala vinavyoongozwa na makanisa ya Marekani barani Afrika.

Maafa ya Ebola nchini Liberia
Maafa ya Ebola nchini LiberiaPicha: picture-alliance/dpa

Juu ya maradhi ya Ebola yaliyoripuka tena barani Afrika gazeti la Neues Deutschland linazungumzia juu ya matumaini ya kupatikana chanjo ya ugonjwa huo. Gazeti la Neues Deutschland linaarifu kwamba katika harakati za kupambana na maradhi hayo,kwa mara ya kwanza majaribio ya chanjo yatafanyika kwa binadamu. Kampuni ya Marekani," US Newlink Genetics imesema ,kuwa inazo chanjo za kutosha.

Meneja asema dawa zinaweza kutengezwa kwa wingi
Gazeti la Neues Deutschland limemnukuu meneja wa kampuni hiyo Charles Link akisema kuwa kampuni yake ina mpango wa kutengeneza maalfu kwa maalfu ya mikebe ya chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola.

Gazeti la Neues Deutschland pia limefahamisha kwamba kampuni kubwa ya dawa ya nchini Uingereza GlaxoSmith-Kline pia inasubiri kupata kibali ili ianze kutoa chanjo za majaribio, ikiwezekana hata mwezi ujao.

Hakuna miujiza

Gazeti la "Berliner Zeitung" linawatahadharisha watu juu ya kungojea kutokea miujiza katika juhudi za kupambana na maradhi ya Ebola. Gazeti hilo linakumbusha juu ya mkasa uliotokea mnamo mwaka wa 1885.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na EbolaPicha: AP

Linaeleza kuwa mnamo mwaka huo wa1885 mtoto mmoja aliekuwa na umri wa miaka 9 aliumwa na mbwa aliekuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa. Lakini ulitokea muujiza. Mtaalamu mmoja wa madawa Louis Pasteur alimpa mtoto huyo chanjo ambayo hadi wakati huo ilikuwa inatolewa kwa wanyama tu. Lakini mtoto huyo alipona baada ya kupewa dawa hiyo.Hata hivyo gazeti hilo linasema Shirika la Afya Duniani, WHO limechukua hatua sahihi na ya kijasiri kwa kuruhusu kutolewa dawa ambayo mpaka sasa bado haijajaribiwa kwa binadamu.

Lakini gazeti la Berliner Zeitung linasema watu wasitarajie miujiza.Gazeti hilo linakumbusha kwamba Kasisi wa Uhispania aliepewa dawa ya majaribio hakubahatika kupona. Hatahivyo habari kutoka Marekani zinasema kuwa daktari aliyeambukizwa Ebola ametolewa kwenye kitengo cha wagonjwa wenye maradhi ya kuambukiza.Daktari huyo Kent Brantly amesema yeye sasa ni mzima wa afya baada ya kutibiwa kwa dawa ya majaribio.

Kanisa la Marekani lapinga ushoga barani Afrika
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii limechapisha makala juu ya kile inachokiita vita vya kiwakala barani Afrika vinavyoongozwa na Kasisi wa "Kanisa huru" la Marekani, Scott Lively anaetambulika kwa msimamo wake wa kukanusha kutokea maangamizi ya wayahudi. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limearifu kuwa Kasisi huyo ameenda Afrika kuongoza kampeni ya kuyatetea maisha ya ndoa baina ya mke na mume.

Gazeti hilo linatueleza kwamba mnamo mwaka wa 2009 ,maalfu ya watu mjini Kampala walienda kwenye hoteli maarufu ya Triangle ambako semina ilikuwa inafanyika. Waandalizi wa semina hiyo,kutoka "Kanisa huru "walisema lengo lao lilikuwa kuzifichua njama za mashoga wanaotaka kuitawala dunia. Mgeni mkuu kwenye semina hiyo alikuwa Kasisi Scott Lively kutoka "Kanisa huru" la Marekani.

Kasisi adai, lengo la mashoga ni kuitawala dunia


Gazeti la "Frankruter Allgemeine" linatufahamisha kwamba Kasisi Scott Lively aliwaambia wajumbe kwenye semina hiyo kwamba familia ya jadi barani Afrika ya mke na mume imo hatarini. Gazeti hilo limemkariri kasisi Lively akisema kuwa pana njama duniani za kuuteketeza utaratibu wa maisha ya jadi wa ndoa baina ya mwanamke na mwanamume. Kasisi Lively amesema njama hizo zinafanywa na mashoga na kwamba lengo lao ni kuitawala dunia.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeime,linasema katika makala yake kwamba mfano wa Uganda ni mmojawapo tu unaoonyesha jinsi makanisa ya Marekani yanavyojitandaza barani Afrika na jinsi yanavyozidi kupata umaarufu kutokana na kampeni ya kuupinga ushoga. Kwa mujibu wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine"maalfu kwa maalfu ya watu nchini Kenya wanajiunga na mtandao wa "Kanisa huru la Marekani."

.Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusufu Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW