1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya13 Septemba 2014

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika kuhusu madai yaliyotolewa juu ya walinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia kwamba askari hao wanawadhalilisha wanawake kingono.Na pia yameandika juu ya Boko Haram

Majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia
Majeshi ya Umoja wa Afrika nchini SomaliaPicha: picture alliance/AP Photo

Gazeti la "die tageszeitung" limeandika juu ya madai yaliyotolewa na Shirika la kutetea haki za binadamu HRW kuhusu wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia. Shirika hilo linadai kwamba wanajeshi hao wanawadhalilisha wanawake kingono.

Gazeti hilo linaeleza kwamba wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanaopaswa kulinda amani nchini Somalia, wanadai ngono kutoka kwa wanawake wa nchi hiyo kwa mahitaji wanayowapatia wanawake hao kama vile maji na dawa.


Gazeti la "die tageszeitung" linasema mambo hayo siyo siri tena. Gazeti hilo limearifu kwamba asasi ya kutetea haki za binadamu ya HRW ,imezipata habari hizo kutokana na kuwahoji wanawake wanaodai kufanyiwa mambo hayo na pia kutokana na kuwahoji maafisa wa nchi zilizochangia majeshi na wajumbe wa kimataifa.

Gazeti la "die tageszeitung" limelinukuu shirika la HRW likisema kwamba baadhi ya mikasa ya kunyanyaswa wanawake wa Somalia imefanyika kwenye makao ya majeshi ya Umoja wa Afrika. Lakini gazeti la "die tageszeitung" limesema Umoja wa Afrika umeyakanusha madai hayo.

Boko Haram waendelea kuiteka miji kaskazini mashariki mwa Nigeria

Gazeti la "Süddeutsche limechapisha makala juu ya kundi la magaidi wa Boko Haram nchini Nigeria. Gazeti hilo linasema magaidi hao wanaendelea kuiteka miji kaskazini mashariki mwa nchi.

Kutokana na hali hiyo gazeti hilo linauliza iwapo Nigeria itaendelea ,kuwa nchi moja?Gazeti la "Süddeutsche" linaendelea kuuliza jee kundi la Boko la Haram ni dola la Kiislamu la barani Afrika, linalojaribu kuigawa Nigeria wakati jeshi la serikali halina uwezo wa kufanya lolote.

Kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau alito mwito mnamo mwezi wa Agosti wa kuunda dola la Kiislamu kaskazini mashariki mwa Nigeria mithili ya dola la Kiislamu la nchini Iraq na Syria. Gazeti la "Süddeutsche" linatilia maanani, kwamba makundi ya Boko Haram na Dola la Kiislamu yanatumia mikakati inayofanana, ikiwa pamoja na kuwateka nyara raia na hasa wanawake na wasichana.

Hata hivyo gazeti hilo limekariri mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa wa nchini Nigeria Nkwachukwu Orji akisema makundi hayo mawili hayawezi kulinganishwa.

Waziri Gerd Müller ataka mafuta ya kampuni ya Shell yasusiwe

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeripoti juu ya mwito ulitolewa na Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller wa kuyasusia mafuta ya kampuni ya Shell. Waziri Müller alifanya ziara nchini Nigeria hivi karibuni.

Gazeti hilo linaeleza kuwa Waziri Müller amewataka wenye magari nchini Ujerumani wayasusie mafuta yanayouzwa kwenye vituo vya petroli vya kampuni ya Shell. Sababu ni kwamba njia zinazotumiwa na kampuni hiyo ya kuchimba mafuta katika jimbo la Niger Delta zinayateketeza mazingira.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukuu Waziri Müller akisema ili Wajerumani waweze kuwa na maisha bora mazingira yanateketezwa nchini Nigeria.Waziri Müller amekaririwa na gazeti hilo akisema kuwa lazima viwekwe vigezo juu ya kuvifikia viwango vya kuyalinda mazingira.

Wanyonge ndio wanaoumia
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limearifu kwamba Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller pia amelalamika juu ya hali za wafanyakazi kwenye viwanda vya nguo katika mabara ya Afrika na Asia. Amesema wakati jezi moja ya timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani inauzwa kwa bei ya Euro 84, mfanyakazi anaeishona jezi hiyo analipwa senti 15 tu.

Mwandishi:Mtullya Abdu. Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW