1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

.

Abdu Said Mtullya9 Januari 2015

Wiki hii magazeti hayo yameandika juu ya mafanikio yaliyopatikana katika juhudi za kupambana na maradhi ya Ebola na juu ya vitega uchumi vya China barani Afrika

Rais Paul Biya wa Cameroon
Rais Paul Biya wa CameroonPicha: Patrick Kovarik/AFP/Getty Images

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linasema mafanikio yameanza kupatikana katika juhudi za kuyakabili maradhi ya Ebola nchini Liberia.

Gazeti la "Der Tagespiegel" linatueleza kwamba kutokana na msaada mkubwa wa jumuiya ya kimataifa mafanikio yameanza kuonekana nchini humo .Hadi hivi karibuni watu 350 walikuwa wanakufa kila wiki nchini Liberia kutokana na ugonjwa wa Ebola. Lakini katika wiki ya mwisho ya mwezi wa Desemba ni mikasa 31 tu ya Ebola iliyoripotiwa nchini Liberia kote.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limefahamisha kwamba tokea kuripuka maradhi ya Ebola katika nchi za Afrika magharibi karibu mwaka mmoja uliopita, watu zaidi ya 20.600 waliambukizzwa na zaidi ya 8,000 wameshakufa.

Cameroon katika mtego wa deni

Gazeti la "Süddeutsche" linasema Cameroon imo katika hatari ya kulemewa na madeni kutokana na kupungua kwa mapato ya serikali. Lakini gazeti hilo linasema China inaweza kusaidia nchi hiyo.

Gazeti hilo linaeleza kuwa Douala ni mji wa bandari ambao ndiyo moyo wa uchumi wa Cameroon. Lakini sasa moyo huo unahitaji kuwekewa mashine ili uendelee kudunda. Kuanguka kwa bei ya mafuta kwenye masoko ya dunia kumeyapunguza mapato ya serikali kwa kiwango kikubwa.

Hadi mwanzoni mwa mwaka uliopita serikali ya Cameroon ilikuwa inaingiza kiasi cha dola Bilioni 1.3 kila mwaka. Lakini wataalamu sasa wanakadiria kwamba mapato hayo yamepungua kwa nusu nzima.

Gazeti la "Süddeutsche "linafahamisha katika makala yake kwamba kutokana na mapato ya serikali kupungua Cameroon imo katika hatari ya kulemewa na deni kubwa. Gazeti hilo limezikariri takwimu za asasi binafsi ya mitaala ya uchumi zinazoonyesha kuwa deni la Cameroon sasa limefikia asilimia 20 ya pato lake jumla. Na kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya kiuchumi,Amaizo aliyenukuliwa na gazeti la "Süddeutsche" China ndiyo inayoweza kuwa mwokozi wa Cameroon.

Vitega uchumi vikubwa kutoka China na athari zake

Na gazeti la "Berliner Zeitung" linasema katika makala yake wiki hii linatilia maanani kwamba vitega uchumi vikubwa vya China katika nchi za Afrika pia vina matatizo yake.

Gazeti hilo linaeleza kuwa China siku nyingi imeshazipiku Marekani na nchi nyingine za magharibi katika kuekeza vitega uchumi barani Afrika.Katika kipindi kifupi kinachonzia mwanzoni mwa karne hii, biashara ya kubadilishana bidhaa baina ya China na nchi za Afrika imeshafikia thamani ya dola Bilioni 200 .

Hata hivyo gazeti la "Berliner Zeitung" linaeleza kwamba mikataba inyofikiwa baina ya serikali za nchi za Afrika na China aghalabu haijulikani kwa wananchi.Gazeti hilo linadai kuwa watu barani Afrika hawajui ni kwa kiasi gani serikali zao zinadaiwa na China. Linadai kwamba wananchi hawajui chochote juu ya mikataba inayofikiwa baina ya serikali zao na China. Lakini gazeti hilo linatilia maanani kwamba China sasa ndiyo mshirika mkubwa kabisa wa biashara wa nchi za Afrika.

Kamanda wa magaidi wa LRA ajisalimisha
Gazeti la "die tageszeitung" limezikariri taarifa kwamba kiongozi wa ngazi za juu wa kundi la kigaidi la Uganda LRA. kamanda Domic Ongwen amejisalimisha kwa majeshi ya Marekani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ongweni ni miongoni mwa viongozi wa kundi hilo ambae amekuwa anasakwa kwa miaka mingi na Mahakama ya mjini The Hague ya ICC.


Mwandishi:Mtullya Abdu. Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Iddi Ssessanga.