1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

.

Abdu Said Mtullya23 Januari 2015

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na maradhi ya Ebola na pia yameandika juu ya ukatili wa Boko Haram

Maandamano ya kupinga kuchapishwa kikaragosi cha Mtume Mohammad
Maandamano ya kupinga kuchapishwa kikaragosi cha Mtume Mohammad nchini NigerPicha: Boureima Hama/AFP/Getty Images

Gazeti la "Süddeutsche " linaarifu juu ya chanjo za kujikinga na maradhi ya Ebola. Chanjo hizo zinatarajiwa kutolewa wiki ijayo katika nchi tatu zilizokumbwa na ugonjwa wa Ebola,Sierra Leone,Guinea na Liberia.

Gazeti hilo linaeleza kwamba mwaka mmoja baada kulipuka maradhi ya Ebola, katika kiwango kisichokuwa na mithili katika historia,sasa aina kadhaa za chanjo zinatayarishwa, ili kutolewa kwa watu.

Wataalamu bado hawajakubaliana kwa uhakika juu ya siku ya kuanza kuwachanja watu,katika nchi tatu za Afrika magharibi zilizokumbwa na maradhi ya Ebola lakini dawa hizo zinatarajiwa kujaribiwa mnamo mwezi huu wa Janauri.

Hayajatokea maambukizi tokea mwezi wa Desemba nchini Mali


Na katika makala yake gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limechapisha habari njema kutoka Guinea. Gazeti hilo limearifu kwamba mikasa ya maambukizi ya Ebola imepungua kiasi kwamba sasa shule zinaweza kuanza tena,baada ya kufungwa kwa muda mrefu. Habari nyingine za kutia moyo zinatoka Mali, Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema.kuanzia tarehe sita ya mwezi wa Desemba hapajatokea mkasa wowote wa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola nchini humo.

Boko Haram hawatosheki na damu ya Nigeria sasa wanaingia Cameroon

Gazeti la "Berliner " wiki hii limeandika juu ya kundi la magaidi wa Boko Haram nchini Nigeria. Gazeti hilo linasema magaidi hao hawatosheki na mauaji wanayoyafanya nchini Nigeria, bali sasa pia wanaenda kuua katika nchi jirani ya Cameroon´

"Berliner Zeitung" linaeleza kuwa mwanzoni mwa wiki iliyopita wapiganaji wa Boko Haram walivivamia vijiji kadhaa kaskazini magharibi mwa Cameroon na kuwateka nyara watu 80, miongoni mwao wasichana 50 na wavulana wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 15. Lakini mateka 20 walikombolewa na jeshi la Cameroon, muda mfupi baada ya kutekwa nyara.Wanajeshi wa Cameroon walipambana na wapiganaji wa Boko Haram kwa saa kadhaa.

Gazeti la "Berliner " limesema katika ujumbe wa video kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau, alitangaza mwanzoni mwa mwaka huu kwamba kundi lake litaimarisha mashambulio katika nchi jirani ya Cameroon.Shekau amemtaka Rais Paul Biya wa nchi hiyo aibatilishe katiba ya sasa na badale yake aunzishe utawala wa kiislamu.

Biashara huru baina ya Marekani na Ulaya itawaathiri wavuvi wa Afrika

Nchi za Afrika zinahofia kuwa zitapata hasara kutokana na mkataba wa biashara huru baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya, kwa kifupi TTIP. Hizo ni habari nyingine zilizoandikwa na gazeti la "Süddeutsche" mnamo wiki hii.

Gazeti hilo linaeleza kwamba alipofanya ziara nchini Ujerumani,Rais wa Ghana John Dramani Mahama aliuliza jee kitatokea nini katika sekta ya uvuvi, ikiwa mkataba wa biashara huru baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya utatiwa saini? Jee itakuwaje kwa wavuvi wa Ghana na nchi nyingine za Afrika magharibi wanaouza samaki wao kwenye soko la Umoja wa Ulaya?

Gazeti la"Süddeutsche" limemnukulu Rais Mahama wa Ghana akisema, anahofia huenda wavuvi wa nchi za Afrika magharibi wakabaguliwa kutokana na vigezo vipya vitakavyowekwa katika biashara ya samaki baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani.

Maandamano ya kupinga kibonzo cha Mtume wa dini ya Kiislamu

Gazeti la "Die Welt" wiki hii limeripoti juu ya ghasia zilizotokea nchini Niger baada ya waislamu wa nchi hiyo kufanya maandamano ya kupinga kuchapishwa kibonzo cha Mtume wa dini ya Kiislamu Mohammad na jarida la "Charlie Hebdo" la mjini Paris. Gazeti hilo limearifu kwamba watu waliuawa na makanisa kadhaa yalichomwa moto katika mji mkuu wa Niger ,Niamey.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu