1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram walemewa

13 Machi 2015

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yamechapisha habari juu ya adhabu ya kifungo iliyotolewa kwa mke wa aliekuwa Rais wa Ivory Coast na pia yameandika juu ya magaidi wa Boko Haram

Mke wa aliekuwa Rais wa Ivory Coast , Simone Gbagbo
Mke wa aliekuwa Rais wa Ivory Coast, Simone GbagboPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Blackwell

Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha habari juu ya mke wa aliekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo. Mama huyo Simone Gbagbo amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na vitendo vilivyosababisha umwagikaji damu.

Gazeti la "die tageszeitung" linatufahamisha kwamba Simone Gbagbo alihukumiwa adhabu hiyo Jumanne iliyopita baada ya kupatikana na hatia ya kuhujumu usalama wa nchi, kushiriki katika upinzani wa kutumia nguvu dhidi ya dola na kuvuruga utulivu wa nchi.

Kwa jumla watu 83 walifikishwa mahakamani mjini Abdijan kujibu mashtaka hayo yaliyotokana na matukio ya baada ya uchaguzi wa Rais wa mwaka 2010 nchini Ivory Coast.


Gazeti la "die tageszeitung "linatukumbusha kwamba mumewe Simone,yaani aliekuwa Rais wa Ivory Coast wakati huo Gbagbo alishindwa katika uchaguzi huo lakini alikataa kuyatambua matokeo.Ghasia zilianza nchini humo na kusababisha vifo vya maalfu ya watu.

Boko Haram wala kiapo cha utiifu kwa "Dola la Kiislamu"

Gazeti la "Die Welt" limechapisha habari juu ya kiapo cha utiifu cha Boko Haram.Gazeti hilo linaeleza kwamba kutoka Maiduguri kaskazini mwa Nigeria, hadi Rakka,Syria ni umbali wa kilometa karibu alfu tano. Licha ya umbali huo,pametokea jambo la kusababisha ngozi ya kimbimbi. Kundi la magaidi wa Boko Haram lilitangaza utiifu kwa kundi linaloitwa dola la kiislamu IS.


Gazeti la "Die Welt" linauliza iwapo kiapo hicho cha Boko Haram maana yake ni kuungana kwa makundi hayo mawili ya kigaidi jambo ambalo limekuwa likihofiwa na wataalamu kwa muda mrefu? Na ndiyo kusema sasa unajengeka mfungamano wa dunia nzima wa Waislamu wenye itikadi kali?

Lakini gazeti la " Tagesspiegel" linasema katika makala yake kwamba kiapo cha utiifu cha Boko Haram kwa magaidi wanaoitwa Dola la Kiislamu ni dalili ya kutamauka. Gazeti hilo linaeleza kwamba mashambulio yaliyofanywa dhidi ya Boko Haram na majeshi ya nchi za Afrika magharibi yaliyoshirikiana, yameanza kuonyesha dalili za kulemewa kwa magaidi hao. Majeshi ya Nigeria na ya nchi jirani yamefanikiwa kuzirudisha katika mikono ya serikali sehemu ambazo hapo awali zilitekwa na Boko Haram.

Gazeti hilo limesema kutokana na kuanza kubanwa kiongozi wa Boko Haram amewasilisha ujumbe kwa Dola la kiislamu kama ishara ya kuomba msaada.

Nigeria yawatumia mamluki

Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha habari juu ya kuuawa raia mweupe wa Afrika kusini katika mapambano dhidi ya magaidi wa Boko Haram.Mtu huyo Leon Lotz alikufa Jumatatu iliyopita katika mji wa Maiduguri kaskazini mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa habari zilizokaririwa na gazeti "tageszeitung" raia huyo wa Afrika Kusini aliekuwa mamluki , alikufa baada ya msafara wake kushambuliwa kwa makosa na kifaru cha jeshi la Nigeria. Gazeti hilo limeeleza zaidi kwamba Leon Lotz alikuwamo katika jeshi la utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini na alikuwa na uzoefu wa kupambana na ugaidi. Leon aliwakabili wapigania uhuru wa Namibia ,Swapo mnamo miaka ya 80.

Gazeti la "die tageszeitung"limearifu katika makala yake kwamba mamluki kadhaa kutoka Afrika Kusini wamekodishwa na serikali ya Nigeria katika harakati za kupambana na magaidi wa Boko Haram. Lakini gazeti hilo limezikariri taarifa zinazosema kuwa serikali ya chama cha ANC itawachukulia hatua za kisheria mamluki hao kwa kushiriki katika shughuli za kijeshi nje ya jeshi la serikali.

Mwandishi:Mtullya Abdu. Deutsche Zeitungen

Mhariri:Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW