1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yajadiliwa na nchi tajiri

7 Juni 2015

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya nafasi ya Afrika kwenye mkutano wa nchi 7 tajiri unaofanyika katika jimbo la Bavaria nchini Ujerumani . Na Waziri wa Ujerumani ataka wanunuzi wa meno ya tembo wabanwe

Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks
Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara HendricksPicha: Reuters/F. Bensch

Magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii pia yameandika juu ya wakimbizi wa Afrika wanaokufa kwenye bahari ya Mediterania na pia yanasema ,hakuna mahala ambapo aliekuwa Rais wa FIFA Blatter, anaenziwa kama barani Afrika.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linatilia maanani nafasi ya bara la Afrika kwenye mkutano wa viongozi wa nchi 7 tajiri kabisa duniani, unaofanyika katika jimbo la Bavaria kusini mwa Ujerumani.

Gazeti hilo limemnukulu mshauri wa Kansela wa Ujerumani juu ya masuala ya Afrika,Günter Nooke akieleza kwa nini Afrika inazingatiwa kwenye mkutano huo:


Bwana Nooke amesema ni lengo la nchi tajiri kuziunga mkono juhudi za nchi za Afrika katika kuweka msingi endelevu wa maendeleo, katika sekta za uchumi na afya. Bwana Nooke ameliambia gazeti la "Der Tagesspiegel" kwamba pamoja na nchi saba tajiri kuonyesha moyo wa kushikamana na nchi za Afrika, viongozi wa Afrika nao, pia wanapaswa kuwajibika juu ya matatatizo yanayowakabili watu wao, kama vile juu ya wakimbizi kutoka nchi za Afrika wanaokufa kwenye bahari ya Mediterania.

Na gazeti la "die tageszeitung" limeandika maoni juu ya wakimbizi wa Afrika wanaokufa kwenye bahari ya Mediterania. Chini ya utanguzi unaosema vifo bila ya vilio gazeti hilo linasema bara la Afrika linajisherehekea lenyewe lakini linalipuuza suala la wakimbizi wanaokufa kwenye bahari ya Mediterania.


Katika maoni yake gazeti la "die tageszeitung" linasema viongozi wa Umoja wa Afrika wanajipongeza kwa mafanikio yaliyofikiwa barani Afrika tangu kuundwa Umoja wa Afrika,OAU, lakini viongozi hao hawajasema mengi juu ya maafa ya wakimbizi.

Lazima kupambana na wanunuzi wa vipusa

Gazeti la "Die Welt" limechapisha mahojiano na Waziri wa Ujerumani juu ya tatizo la ujangili wa wanyama pori barani Afrika.

Katika mahojiano hayo Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks amesema kuwa sasa inapasa juhudi zielekezwe pia katika kupambana na wale wanaonunua pembe za ndovu na faru, badala ya kuzielekeza juhudi hizo katika kuwakabili majangili tu.

Waziri wa Ujerumani Hendricks ameliambia gazeti la "Die Welt" kwamba ujangili umefikia kiwango cha kutisha na kwa hivyo amesema haitoshi ,kuwakabili majangili kule wanakowaua wanyama. Bali sasa ni lazima nchi zote zishirikiane katika kuuvunja mtandao wa wanunuzi wa pembe za faru na ndovu.

Miaka ya hivi karibuni ilikuwa ni kipindi kibaya sana kwa ndovu barani Afrika.Mnamo mwaka wa 2010 tembo wapatao alfu 40 waliuliwa na majangili na katika mwaka uliopita tembo zaidi ya 20,000 waliangamizwa na majangili nchini Afrika kusini. Mnamo miaka ya 1970 walikuwapo ndovu zaidi ya 1,600,000 katika mbuga za Savannah .Lakini katika kipindi cha mwongo mmoja tu idadi hiyo ilipungua kwa zaidi ya nusu.

Sepp Blatter apendwa barani Afrika

Gazeti la "Berliner Zeitung" linasema ikiwa Sepp Blatter atatafuta mahala pa kuomba hifadhi basi itakuwa ni barani Afrika.Gazeti hilo linasema hakuna mahala ambapo Blatter aneenziwa kama barani Afrika.

Gazeti hilo linasema Sepp Blatter aliekuwa Rais wa Shirikisho la kandanda duniani,FIFA alivisaidia sana vyama vya soka barani Afrika. Kutokana na uongozi wa Blatter,mpango wa maendeleo wa Fifa ulianzishwa manmo mwaka wa 1999 barani Afrika.

Gazeti la "Berliner" linafahamisha kwamba kutokana na mpango huo wa maendeleo miradi 200 ya kuendeleza kandanda ilianzishwa katika nchi za Afrika. Gazeti hilo linakumbusha kwamba hadi mwaka wa 1966 hakuna nchi hata moja ya Afrika iliyopewa fursa ya kuingia katika fainali za kombe la dunia nchini Uingereza Ni baadae tu ambapo nchi za Afrika zilipewa nafasi mbili katika fainali za kombe la dunia. Ni Sepp Blatter alieongeza idadi, hadi kufikia nafasi tano kwa nchi za Afrika.

.Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW