1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kasi ya ustawi yapungua barani Afrika

12 Februari 2016

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kuanguka bei za malighafi kutoka Afrika na juu ya wasi wasi wa kutokea baa la njaa kusini mwa Afrika.

Viongozi wa Afrika kwenye mkutano wa AU mjini Addis Ababa
Viongozi wa Afrika kwenye mkutano wa AU mjini Addis AbabaPicha: picture alliance/dpa/Gcis

Hadi hivi karibuni tu bara la Afrika lilizingatiwa kuwa muujiza wa kiuchumi kutokana na ustawi wa uchumi, ambao wakati mwingine ulivuka asilimia 10. Lakini sasa hali imeanza kubadilika kutokana na kuanguka kwa bei ya mafuta na kutokana na kupungua kwa utashi wa malighafi katika soko la China.

Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Frankfurter Allgeimeine" mnamo wiki hii. Gazeti hilo linaeleza kwamba tangu uchumi wa China uanze kupungua kasi, mahitaji yake ya malighafi pia yamepungua. Wauzaji wa malighafi, yaani nchi za Afrika ,zimeathirika.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema kama Waafrika walikuwa wanafaidi uhondo wa tafrija, sasa tafrija hiyo imekwisha! Gazeti hilo linasema nchi zilizokuwa zinakula uhondo ni zile zinazouza, shaba,chuma cha pua, kobalt na madini mengine. Nafasi za ajira zaidi ya 50,000 zimeteketea nchini Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia.

Lakini pia wauzaji mafuta kama Nigeria na Angola wameathirika kutokana na bei ya bidhaa hiyo kuanguka kwenye soko la dunia.

Hata hivyo gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeinukulu taasisi ya Bretton- Woods ikitabiri kwamba uchumi wa Afrika utastawi kwa asilimia hadi 4,2 mnamo mwaka huu.

Ndoto ya kuleta mapinduzi ya viwanda bado ipo

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ,ADB, Donald KaberukaPicha: Getty Images/C. Somodevilla

Gazeti la "Neues Deutschland" linasema Afrika bado inaendelea kuota ndoto ya kuugeuza uchumi wake uwe wa viwanda. Kupungua mahitaji ya China ya malighafi kutoka Afrika kumepunguza kasi ya ustawi wa uchumi wa Afrika.Na kwa hivyo sasa bara la Afrika linakusudia kuleta mapinduzi ya viwanda ili kutenga nafasi za ajira na kuliimarisha tabaka la kati.

Gazeti la "Neues Deutschland" linaeleza kwamba matumaini juu ya Afrika kuweza kujenga uchumi wa viwanda yanatokana na dhamira ya Waafrika wenyewe ya kupania kuleta maendeleo badala ya kuzingojea serikali zao.

Gazeti hilo limemnukulu Profesa, wa masuala ya uchumi, Margaret McMillan kutoka chuo kikuu cha Marekani cha Tuft, akieleza kwamba bara la Afrika sasa limejaa watu wenye ari ya kufanya kazi ili kuyajenga maisha yao kwa mikono yao, badala ya kungojea hisani ya serikali zao.

Profesa Margaret McMillan amekaririwa akisema kwamba watu hao wanaanzisha miradi midogo midogo ya biashara mijini na mashambani. Hata hivyo gazeti la "Neues Deutschland" linasema mpaka sasa ni nchi nne barani Afrika zenye sekta kubwa ya viwanda- Afrika Kusini,Misri,Morocco na Tunisia.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linazungumzia juu ya hatari ya kutokea njaa nchini Zimbabwe na kusini mwa Afrika kwa ujumla kutokana na ukame wa muda mrefu. Zimbabwe imetangaza hali ya maafa katika majimbo kadhaa.

Lakini gazeti hilo linasema siyo ukame tu uliosababisha hali hiyo, bali sera ya ardhi ya Rais Mugabe pia inapaswa kulaumiwa.Lakini pia inapasa kutilia maanani kwamba Zimbabwe bado imewekewa vikwazo vya kiuchumi na nchi za magharibi.

.Mwandishi: Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef