1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

4 Agosti 2017

Yaliyoandikwa katika magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii tunaanza na gazeti la Die Welt juu ya kifo cha Chris Musando aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka ya nchini Kenya IEBC.

Kenia Christopher Msando
Picha: Picture-alliance/AP Photo

 

Marehemu Musando alikutwa amekufa akiwa na ishara za kuteswa kabla ya kuuliwa.  Gazeti la Die Welt linasema afisa huyo alikuwa na dhamira ya kuhakikisha kufanyika uchaguzi huru na wa haki hapo siku ya Jumanne nchini Kenya.  Polisi nchini Kenya imethibitisha kwamba hayati Musando aliuwawa nje kidogo ya jiji la Nairobi lakini mpaka sasa polisi haijatoa taarifa yoyote juu ya sababu ya kuuliwa Chris Mosando. Licha ya kuarifu kwamba karibu na mwili wake ilikuwapo maiti ya mwanamke ambayo pia ilionyesha kuwa aliuliwa.  

Gazeti la Die Welt limekumbusha katika makala yake kwamba mnamo mwaka 2007 watu zaidi ya 1000 waliuwawa kutokana na ghasia baada ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Kenya.  Hata hivyo gazeti la Die Welt limebainisha kutokana na utafiti wake kwamba Wakenya wengi hawaamini iwapo yaliyotokea baada ya uchaguzi huo wa mwaka 2007 yatajirudia lakini gazeti hilolinatilia maanani kwamba hofu kubwa ya kutokea machafuko imetanda nchini kote.

Gazeti la Süddeutsche wiki hii limeandika juu ya ziara ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen nchini Mali  ambapo waziri Von der Leyen alikwenda Mali ili kushiriki katika maombolezo ya marubani wawili wa jeshi la Ujerumani waliokufa nchini humo baada ya Helikopta yao kuanguka wiki iliyopita.  Waziri Von der Leyen amenukuliwa na gazeti la Süddeutsche akisema vifo vya marubani hao wawili ni hasara kubwa kwa jeshi la Ujerumani ''Bundeswehr''. Gazeti hilo linafahamisha kwamba wanajeshi zaidi ya 890 wako nchini Mali kama sehemu ya jeshi la Umoja wa Mataifa MINUSMA linalolinda amani na kupambana na magaidi nchini humo.

Uhusiano kati ya bara la Afrika na China

Ggazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya uhusiano baina ya bara la Afrika na China.  Gazeti hilo limeripoti juu ya maonyesho yaliyofanyika katika mji wa Leipzig uliopo Mashariki mwa Ujerumani. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linafahamisha kwamba maonyesho hayo yalihudhuriwa na wataalamu kutoka China pamoja na wasanii wa Afrika kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Nigeria, Angola na Afrika Kusini. Gazeti hilo linaeleza kwamba lengo la kutayarisha maonyesho hayo katika mji wa Ulaya ni kuwasilisha ujumbe ulio wazi kabisa kwamba mustakabali wa dunia unajengwa bila ya ushiriki mkubwa wa nchi za Ulaya, gazeti la Frankfurter Allgemeine limemnukuu mwanafalsafa wa Cameroon Achille Mbembe aliyesema ushiriki wa nchi za magharibi unazidi kuwa mdogo inapohusu kuujenga mustakabali wa dunia.  Hata hivyo gazeti hilo linauliza jee! Ni kwa kiasi gani nchi za Afrika zinaweza kujieleza kwa ufasaha inapohusu uhusiano wao na China?

Gazeti la Neues Deutschland wiki hii linatilia maanani kwamba wakulima wadogo wadogo wa zao la Korosho wanazidi kunufaika na zao hilo kuanzia ulimaji wake hadi soko lake. Ulaji wa Korosho unaongezeka kwa asilimia 10 kila mwaka duniani kote.  Bei ya zao hilo tamu inazidi kupanda barani Ulaya.  Wakulima wa zao hilo barani Afrika wanaweza kuondokana na umasikini kutokana na mauzo ya Korosho. Gazeti hilo la Neues Deutschland linasema wakulima wa Korosho katika nchi tano za Afrika wanaweza kunufaika na miradi ya kisasa ya kuliendeleza zao la Korosho. Gazeti hilo linafahamisha kwamba wafadhili wa miradi ya maendeleo kutoka Ujerumani pamoja na wakfu wa Bill Gates wanataka kuwasaidia wakulima wa Afrika ili wapate soko la zao lao. Gazeti la Neues Deutschland linakumbusha kwamba miaka 10 iliyopita kilo moja ya Korosho kabla ya kubanjuliwa ilikuwa senti 9 tu lakini leo kilo moja inaingiza senti 90 za Euro.

Mwanadishi: Zainab Aziz

Mhariri: Mohammed Khelef

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW