Afrika katika magazeti ya Ujerumani
11 Agosti 2017Gazeti la Süddeutsche Zeitung juu ya uchaguzi mkuu wa nchini Kenya, linasema katika nchi hiyo miaka iliyopita ilichukua muda hadi kumalizika kuhesabiwa kura na kufahamu yanayojiri baada ya kufanyika uchaguzi wa rais lakini safari hii ilichukua muda wa masaa machache kwa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, kusema kwamba ulifanyika udanganyifu katika uchaguzi. Gazeti hilo la Süddeutsche Zeitung limemnukulu Odinga akisema kuwa matokeo ya uchaguzi yalikuwa ni aibu na kwamba hayawezi kuaminika. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba hii ilikuwa ni mara ya nne kwa Raila Odinga kuwania urais, lakini kwa mara tatu kiongozi huyo wa upinzani amelalamika kuwa anaibiwa kura. Gazeti hilo limemkariri Odinga akisema: "Tunawaambia wafuasi wetu wasiyakubali matokeo ya uchaguzi." Lakini gazeti hilo la Süddeutsche Zeitung linasema kukataa kwa Odinga kuyatambua matokeo ya uchaguzi kunawakumbusha Wakenya wengi juu ya yaliyotokea baada ya kufanyika uchaguzi wa mwaka 2007. Gazeti hilo pia linakumbusha juu ya ghasia zilizosababisha vifo vya watu wapatao 1,200.
Gazeti la Neues Deutschland nalo limeandika makala yenye kichwa cha habari kinachosema J"aribio la mwisho la Raila Odinga". Gazeti hilo linaeleza kwamba kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2013, Raila Odinga na Uhuru Kenyatta wamepambana tena. Gazeti hilo la Neues Deutschland linaendelea kusema ndio sababu kwa muda wa miezi kadhaa kabla ya kufanyika uchaguzi, hofu ilitanda kwamba mgombea atakayeshindwa hatayatambua matokeo ya uchaguzi na huenda akatoa mwito kwa wafuasi wake kufanya ghasia. Gazeti hilo pia linakumbusha yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Ziara ya Sigmar Gabriel nchini Sudan ya Kusini
Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika juu ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Gabriel Sigmar, huko nchini Sudan Kusini. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba leo theluthi moja ya watu wa Sudan Kusini ni wakimbizi, matumaini yaliyokuwapo siku ya kujipatia uhuru yametoweka kwa watu wa nchi hiyo. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba watu wa Sudan Kusini sasa hawataki tena hoja inayoshikiliwa na watu fulani kama sala, kwamba nchi za magharibi ndizo zinazopaswa kulaumiwa kwa migogoro yote.
Mapambano dhidi ya Malaria
Gazeti la Die Zeit wiki hii linazungumzia juu ya juhudi za kupambana na ugonjwa wa Malaria. Gazeti hilo linaarifu kwamba mwezi ujao watafiti kutoka Ujerumani watafanya majaribio nchini Gabon ya kutoa kinga dhidi ya maradhi hayo kwa kutumia chanjo ambayo imekuwepo kwa muda mrefu. Gazeti hilo la Die Zeit lilifanya mahojiano na daktari, Benjamin Mordmüller, wa Ujerumani anayeshughulikia magonjwa ya nchi za joto. Daktari huyo amelieleza gazeti la Die Zeit jinsi chanjo hiyo inavyofanya kazi sasa. Daktari Mordmüller amesema chanjo hiyo kwanza inafanya kazi ya kupambana na wadudu wa Malaria na wadudu hao hufa katika muda mfupi. Daktari Mordmüller amelieleza gazeti la Die Zeit kwamba watafiti wamefanikiwa kutengeneza dawa inayotumika katika sindano. Ameeleza kwamba njia hiyo ina ufanisi mkubwa.
Maswala ya wanyamapori
Na Gazeti la Stern wiki hii limezungumzia juu ya zoezi la kuwahamisha ndovu 550 na kuwatawanya katika hifadhi tatu za wanyama nchini Malawi. Gazeti hilo linaeleza kwamba zoezi hilo lilikuwa ni lazima kufanyika kwa sababu ndovu hao walikuwa wanaharibu mazingira, waliharibu mazao na katika kipindi cha miaka mitano iliyopita waliuwa watu 45. Gazeti hilo linasema sababu nyingine ya kuwahamisha wanyama hao ni kwamba idadi yao katika hifadhi ya Nkotakota ilipungua sana kutokana na ujangili. Miaka ishirini iliyopita walikuwapo ndovu 1,500 kwenye hifadhi hiyo lakini hadi miaka ya hivi karibuni tembo hao walipungua na hawakufikia hata100. Gazeti hilo la Stern linasema idadi ya ndovu hao katika hifadhi hiyo kwa sasa inaridhisha. Gazeti hilo la Stern limemnukulu mkurugenzi wa hifadhi za wanyama, Andrew Perker, akielezea juhudi zinazofanywa ili kupambana na majangili. Mkurugenzi huyo amesema wametoa mafunzo kwa walinzi 9 wa hifadhi za wanyama nchini Malawi na pia amesisitiza juu ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuwalinda wanyama pori na faida zinazoletwa na wanyama hao kutokana na utalii.
Mwandishi: Zainab Aziz
Vyanzo: Stern, Die Zeit, Frankfurter Allgemeine, Süddeutsche Zeitung, Neues Deutschland
Mhariri: Mohammed Khelef