1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani.

1 Septemba 2017

Na wiki hii gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya kampeni ya kibaguzi inayowalenga watu weupe nchini Afrika Kusini. Nalo gazeti la Der Freitag linasifu juhudi za kinamama katika Mashariki mwa Kongo,

Makala ya gazeti la Süddeutsche juu ya kampeni ya kibaguzi dhidi ya watu weupe nchini Afrika Kusini yanaeleza kwamba lengo la kampeni hiyo ni kuwababaisha wananchi juu ya uhusiano wa kibiashara baina ya Rais Zuma na familia ya wafanyabiashara wakubwa ya akina Gupta nchini Afrika Kusini.  Kampeni hiyo inaendeshwa na kampuni moja ya vyombo vya habari. Kampuni hiyo inayoitwa Bell Pottinger inafanya kazi ya kuwajengea majina mazuri wateja wake kwenye vyombo vya habari.

Gazeti hilo la Süddeutsche linafahamisha kwamba miongoni mwa waliokuwa wateja wa kampuni hiyo yenye historia ya miaka 75 ni mke wa rais wa Syria, Bashar al Assad, aliyekuwa dikteta wa Chile, Agostinno Pinochet, Rais wa Belarus Aleksander Grigoryevich Lukashenko na Oscar Pistorius mwanariadha aliyemuuwa mpenzi wake huko nchini Afrika Kusini.  Gazeti hilo linaendelea kusema kwamba chama cha upinzani nchini humo cha Democratic Alliance kinaishutumu kampuni hiyo ya Bell Pottinger kwa kuendesha kampeni ya chuki kwa madhumuni ya kumsaidia Rais Zuma kuendelea kuiba fedha za umma lakini kampuni hiyo imejitetea kwa kueleza kwamba kazi yake ni kusafisha wajihi wa wateja wake.

Nalo gazeti la Der Freitag linatupia macho juhudi za kina mama watatu za kujijengea mustakabali bora mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na linaripoti kuwa ni salama zaidi kuwa askari kuliko kuwa mwanamke mashariki mwa Kongo hali hiyo ilijiri hadi katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, sasa rika jipya la wanawake limejitokeza ili kupigania haki zao. Wanawake hao wanapaza sauti zao ili kutetea haki, lakini kwa kufanya hivyo pia wanahatarisha maisha yao. Rebecca Kavugho ni mmojawapo wa wanawake hao kutoka jimbo la Goma Kaskazini. Pamoja na wenzake wanataka demokrasia iletwe kwa njia za amani katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  Gazeti hilo la Der Freitag linatufahamisha kwamba kinamama hao wamo katika jumuiya iliyofanikiwa kuleta mabadiliko mashariki mwa Kongo, kwani juhudi za wanawake hao zimeleta tija wakati ambapo nchi yao inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa. Rais Joseph Kabila mwenyewe ndiye chanzo cha mgogoro. Rais huyo alipaswa kuondoka madarakani mwezi Desemba mwaka uliopita. Gazeti la Der Freitag linafahamisha kwamba Rebecca Kavugho amelikwa nchini Marekani kutunikiwa tozo ya mwanamke jasiri inayotolewa na mke wa rais wa Marekani, Melania Trump. Mafaniko yamewapa moyo wanawake hao wa kuanzisha kikundi cha kuwasaidia wanawake wenzao wanaodhalilishwa au waliodhalilishwa kingono huko mashariki mwa Kongo.

Adhabu kali ya kifungo jela cha hadi miaka minne itatolewa kwa yeyote atakaye chafua mazingira kwa kutumia mifoko ya plastiki nchini Kenya. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la die tageszeitung.  Gazeti hilo limeripoti kwamba atayepatikana na hatia ya kutengeneza au kumiliki mifuko ya plastiki atapewa adhabu ya kifungo jela au atatozwa faini ya Euro elfu 37 sawa na Dola elfu 40. Gazeti la die Tageszeitung linatilia maanani kwamba Wakenya wengi wanakubaliana na sheria iliyopitishwa na serikali ili kuyalinda mazingira. Gazeti hilo limemnukulu mama mmoja akieleza kwamba hivi karibuni walichinja mbuzi kwa ajili ya sherehe za arusi na kukuta mifuko miwili ya plastiki ndani ya tumbo la mnyama huyo. Gazeti hilo limekariri takwimu za wizara ya mazingira zinazo onyesha kwamba maduka makubwa nchini Kenya yanatumia mifuko ya plastiki milioni 100 kwa mwaka. Gazeti la die tageszeitung limemnukulu waziri wa mazingira wa Kenya, Judy Wakhungu, akieleza kwamba mifuko hiyo inasababisha madhara makubwa katika mazingira na pia inaathiri afya za watu kwa kiwango kikubwa.

Je! Utani unasaidia katika kudumisha amani na utulivu baina ya watu wa makabila na dini tafauti? Jibu ni NDIYO! Na hicho ndico hasa kinachofanyika nchini Senegal kama gazeti la Die Zeit linavyotufahamisha. Gazeti hilo linasema mizaha haina mwiko nchini Senegal, Mkristo anaweza kumtania Muislamu kwa kumwambia kwamba atamchinjia nguruwe na Muislamu akamjibu kwa kusema nguruwe wako utamla mwenyewe! Gazeti linaendelea kuhadithia kwamba mara nyingine mtu anamsikia mtu wa kabila fulani akimtania wa kabila lingine kwa kumwambia kwamba kabila lake yeye lilikuwa la wafalme na huyo mtu mwingine anatoka kwenye kabila la waliokuwa watumwa. Gazeti hilola Die Zeit linasema watu nchini Senegal wanafanya mizaha pia juu ya kauli za wapita njia kuhusu mambo ya kidini. Labda mtu angefikiri mizaha inawakasirisha Wasenegali lakini gazeti la Die Zeit linasema asilani, badala yake mizaha inachangia katika kudumisha amani na utulivu kwenye taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW