Afrika katika magazeti ya Ujerumani
29 Septemba 2017Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger wiki hii linaanza kwa kusimulia kisa cha mwanamke mmoja Sena Sadia aliyekimbia vita pamoja na wanawe. Mwanamke huyo amesimulia vipi kundi la wapiganaji walivyovamia kijiji chao na kukitia moto mumewe akapigwa risasi na yeye mwenyewe akalazimika kukimbia na kuingia Uganda kupitia njia ya mpakani. Mwanamke huyo hakuweza kunusuru chochote isipokuwa nguo alizovaa yeye na wanawe. Pamoja na yote hayo Sena Sadia anajikuta akiishi katika kambi ya wakimbizi akijaribu kuwatafutia wanawe chochote cha kuwafanya waendelee kuishi. Uganda kwa sasa inawahifadhi wakimbizi milioni 1 na laki 3 kutoka Sudan Kusini waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwao. Wakimbizi hao wanasaidiwa pia na shirika la misaada la Malteser International kutoka mji wa Ujerumani wa Cologne. Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka wa 2011 baada ya vita vya muda mrefu na Sudan lakini baada ya kujipatia uhuru wake vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka. Jukumu la kuwahudumia wakimbizi hao linalotimizwa na Uganda linatambuliwa na jumuiya ya kimataifa. Shirika la misaada kutoka mji wa Cologne la Malteser International linaisaidia Uganda katika ugavi wa maji na huduma za usafi tangu mwaka wa 2013.
Der Tagesspiegel
Gazeti hilo limendika juu ya upinzani mkali dhidi ya kampuni ya usafirishaji Uber iliyoanzishwa nchini Marekani mnamo mwaka wa 2009. Teksi za kampuni hiyo zinatoa huduma za bei nafuu sana na zimeutanuza wigo wake wa huduma hadi nchini Afrika Kusini. Lakini kampuni hiyo inakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa madereva wa teksi wa nchi hiyo. Juhudi za ubunifu wenye lengo la kuleta maendeleo zinapingwa kwa mabavu ya kutumia mapanga na marungu. Kwenye mitaa ya jiji la Johannesburg, madereva wa kampuni ya Uber wanaotumia tekinolojia za kisasa, wanakabiliana na madereva wa teksi za kawaida wanaohofia kupoteza ajira zao kutokana na ushindani unaosababishwa na nauli za chini zinazotozwa na kampuni ya Uber. Mnamo mwaka huu teksi za Uber zilivamiwa kwa ukatili mkubwa mara zaidi ya mia tatu katika jimbo la Gauteng na katika miji ya Johannesburg na Pretoria. Chama tawala cha ANC kimeelezea wasi wasi mkubwa juu ya matukio hayo ya kikatili. Katika wiki za hivi karibuni matukio ya kikatili yaliendelea hadi kufikia kiasi cha kuhatarisha amani. Waziri Mkuu wa jimbo la Gauteng David Makhura amepitisha sheria inayowataka madereva wa teksi za Uber wajiandikishe na waombe leseni ili waweze kuendesha shughuli zao katika miji ya Afrika Kusini. Waziri mkuu huyo amechukua hatua hiyo ili kuzuia mauaji.
Ukoloni wa Wajerumani
Gazeti la Die Welt linaeleza juu ya historia ya ukoloni wa Wajerumani ambayo ni fupi. Hakuna sehemu yoyote barani Afrika iliyotawaliwa na Ujerumani kwa muda wa zaidi ya miaka 30. Hata hivyo katika muda huo mfupi Wajerumani walitawala eneo ambalo lilikuwa la tatu kwa ukubwa. Wajerumani bado hawajayasahau makoloni ya Afrika kutokana na sababu kadhaa. Kwanza koloni lao la zamani ambalo leo ni Namibia, ndiyo nchi pekee ambako Wajerumani bado wanaendelea kuishi tangu enzi ya vizazi vilivyohamia wakati wa ukoloni. Wajerumani wameacha alama zao. Baadhi ya mitaa nchini Namibia bado ina majina ya Wajerumani kama vile ya Gustav Nachtgall au Hermann Wissman hao walikuwa watafiti maarufu wa Kijerumani wa mambo ya Jiografia. Na nchini Tanzania meli ya SS Liemba bado inayakata maji kwenye ziwa Tanganyika. Meli hiyo ilipelekwa Tanganyika na Wajerumani wakati walipoitawala nchi hiyo.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitung
Mhariri: Yusuf Saumu