1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

13 Oktoba 2017

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika pamoja na mengine juu ya mgogoro wa nchini Kenya na njama za rais Mugabe za kuwapiga chenga wanasiasa wanaostahili kuuritihi wadhifa wake.

Kenia Präsidentschaftswahl Proteste in Nairobi
Picha: Reuters/T. Mukoya

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia  maanani   kwamba jumuiya ya kimataifa inawataka  wanasiasa  nchini  Kenya wawe na busara. Gazeti hilo linasema utulivu uliopo baada ya matokeo ya uchaguzi kubatilishwa hauwezi  kudumu kwa muda  mrefu. Gazeti hilo linaeleza kuwa kila siku za jumatatu na ijumaa wafuasi wanaomuunga mkono kiongozi wa  upinzani Raila Odinga wanafanya   maandamano nchini Kenya ya kutaka kuundwa upya kwa tume ya uchaguzi lakini polisi nao wanafanya kazi  yao. Ijumaa  iliyopita polisi hao walitumia gesi ya kutoa  machozi mjini  Nairobi ili kuwakabili waandamanaji. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linasema hali nchini Kenya ni ya kutia  wasiwasi na  ndiyo sababu mabalozi wa nchi  kadhaa miongoni mwao balozi  wa Ujerumani wamewataka viongozi wa Kenya waishughulikie hali ya sasa kwa busara. 

Magazeti yanasemaje juu ya Zimbabwe?

Nchini Zimbabwe, Rais Robert Mugabe  amefanya mabadiliko ya baraza la mawaziri. Gazeti la die tageszeitung linaeleza kwa nini Mugabe amechukua hatua hiyo. Zimbabwe inaendelea kuzama katika lindi la matatizo  ya kiuchumi lakini badala ya kuchukua hatua ili kuondokana na  hali hiyo rais Robert Mugabe anaelekeza juhudi zake katika kumuandalia mkewe urithi wa wadhifa wa urais. Katika mabadiliko aliyoyafanya  Mugabe amemuondoa Makamu  wake, Emmerson Mnangagwa kwenye wadhifa wa waziri wa sheria. Mnangagwa anazingatiwa kuwa hasimu mkubwa wa mke wa rais Mugabe, bi Grace. Lengo la Mugabe ni kuwafyeka mahasimu wa mkewe. Watu nchini Zimbabwe wananong'ona kwamba Grace Mugabe atatangazwa kuwa mrithi wa kiti cha mumewe kwenye mkutano mkuu ujao wa chama tawala cha Zimbabwe Zanu PF.   Juu ya mabadiliko ya baraza  la mawaziri yaliyofanywa na Rais Mugabe, gazeti limemkariri  katibu mkuu wa chama cha kikomunisti cha Zimbabwe Ngqabutho Mabhena, anaeishi katika hifadhi huko nchini Afrika Kusini, akisema mabadiliko hayo hayatayatatua matatizo ya Zimbabwe.

Yaliyojiri nchini Liberia wiki iliyopita

Gazeti la die tageszeitung wiki hii pia limendika  juu ya rais Ellen Johnson  Sirleaf wa Liberia. Linasema baada ya kuiongoza Liberia kwa muda wa miaka12 mama huyo ameng‘atuka. Hata hviyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba Ellen Johnson Sirlef alikuwa anaheshimiwa sana kimataifa, lakini utendaji kazi wake ndani ya Liberia ulikuwa unakosolewa sana.  Lakini vilevile gazeti hilo linamsifu Ellen Johnson  Sirleaf  kwa kuheshimu katiba. Linasema mama huyo hakuwa na mawazo ya kuibadilisha katiba ili kuendelea  kung'ang'ania madarakani, jambo  ambalo limekuwa la kawaida miongoni  mwa viongozi kadhaa barani  Afrika. Hata hivyo gazeti  la die  tageszeitung  linatilia  maanani  kwamba Ellen Johnson  Sirleaf  hakuweza kuitimiza  ahadi  ya  kuung'oa ufisadi katika  miaka 12  ya  uongozi  wake.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

                  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW