1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

20 Oktoba 2017

Wiki hii gazeti la "Die Zeit”, katika makala yake linatanabahisha juu ya mazingira yaliyosababisha mgogoro mkubwa wa wakimbizi usiokuwa na kifani katika historia ya hivi karibuni duniani miongoni mwa mada zingine.

Symbolbild Nigeria Bama Flüchtlinge
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Ola

Miezi michache tu kabla ya wakimbizi kuanza safari ya kukimbilia Ulaya mnamo mwaka 2015, Umoja wa Mataifa ulisimamisha misaada ya chakula kwenye kambi za wakimbizi  za nchini Syria,Jordan na Lebanon. Umoja wa Mataifa ulisema ulichukua uamuzi huo kutokana na ukosefu wa fedha. Gazeti hilo la „Die  Zeit" linapiga mbiu hiyo ya mgambo kwa sababu Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa sasa pia linaona kuwa linalazimika kupunguza mgao wa chakula kwenye kambi za wakimbizi za nchini Kenya na Uganda. Wakimbizi kutoka Sudan Kusini wanahifadhiwa kwenye kambi hizo. Kwa mara nyingine Umoja wa Mataifa hauna fedha.  Gazeti hilo linakumbusha kwamba bara la Ulaya lilikuwamo miongoni mwa wale walioahidi kuishughulikia mizizi ya ukimbizi. Linasema Jambo moja linapasa kuwa wazi kabisa, kwamba ni lazima kuchukua kila hatua, ili kuwapa watu barani Afrika na  katika Mashariki ya Kati, mustakabali mzuri ili waweze kuishi katika nchi zao. Watu katika sehemu hizo wanahitaji chakula  cha kutosha, maji safi na nafasi za ajira.

die tageszeitung

Shambulio la kigaidi katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu ambapo watu wapatao 280 waliuwawa, limeendelea kuzingatiwa na magazeti ya Ujerumani.  Watu wengine 300 walijeruhiwa  kutokana na shambulio hilo.gazeti la „"die  tageszeitung „ linasema shambulio hilo la kigaidi la mjini Mogadishu linathibitisha kwamba serikali ya Somalia bado haijakuwa na nguvu za kutosha za kuwakabili Waislamu wenye itikadi kali wa kundi la Al - Shabaab. Ni kweli kwamba majeshi ya Somalia kwa kushirikiana na jeshi la Umoja wa Afrika yamefanikiwa kuwafurusha magaidi hao wa Al-Shabaab katika mji wa Mogadishu na miji mingine, lakini magaidi hao bado wanadhibiti sehemu za mashambani.  Gazeti la „die tageszeitung" linatilia maanani kwamba baadhi ya wanasiasa wa Somalia wamezilaumu Marekani na Umoja wa Ulaya kwa kutotoa fedha za kutosha kwa ajili ya mishahara ya askari wanaopambana na magaidi wa Al-Shabaab, limewanukuu wanasiasa wa Somalia wakisema kwamba, Marekani na Umoja wa Ulaya hazikufanya juhudi kubwa ili serikali ya Somalia iondolewe vikwazo vya silaha ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa.

Frankfurter Allgemaine

Na gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema tangu rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alipoingia madarakani mnamo mwaka 2009 kumekuwa na mabadiliko 10 katika baraza lake la mawaziri. Gazeti hilo linasema Rais Zuma amefanya mabadiliko ya hivi karibuni katika baraza lake la mawaziri ili kuwapanguza wanaothubutu kumkosoa.  Mnamo mwezi Machi Zuma alifanya mageuzi ya kushangaza tena usiku wa manane pale alipomuondoa aliyekuwa waziri wake wa fedha Pravin Gordhan hatua iliyo sababisha kuporomoka kwa sarafu ya Rand katika soko la hisa. Mabadiliko hayo vilevile yamewashangaza watu. Hatua ya Zuma imewagawa wale wanaompinga na wale wanaomuunga mkono ndani ya chama tawala cha ANC. Zuma amewabadilisha mawaziri sita, hatua inayozingatiwa nchini Afrika Kusini kuwa ni mbinu zake za kisiasa, miezi miwili tu kabla ya kufanyika mkutano mkuu wa chama cha ANC. Kwenye mkutano huo wanachama wataamua juu ya mwenyekiti mpya wa chama atakayekuwa na uwezekano mkubwa wa kuchaguliwa kuwa Rais ifikapo mwaka wa 2019.

Mwandishi/Zainab Aziz/Deutschen Zeitungen

Mhariri:   Mohammed Abdul-Rahman

                

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW