1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

17 Novemba 2017

Magazeti ya Ujerumani wiki iliyopita yalizingatia matukio ya nchini Zimbabwe pia juu ya mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa wa mjini Bonn na hatua ya rais mpya wa Angola ya kumvua madaraka binti ya rais wa zamani.

Simbabwe Robert Mugabe hält Rede an der Uni
Picha: picture-alliance/dpa/AP/T. Mukwazhi

Gazeti la Die Landeszeitung linatuhumu kwamba Rais Robert Mugabe  ameangushwa na mkono unaotokea mbali. Linasema Jenerali aliyeziongoza hatua za kumwangusha Mugabe alialikwa China siku chache tu kabla ya hapo. Gazeti hilo linasema, ni muda mrefu sasa tangu sarafu ya China (Yuan) ianze kutumika rasmi  nchini Zimbabwe. Gazeti hilo linasema jeshi linakataa kuiita hatua yake kuwa ni mapinduzi ili kuepusha vikwazo kutoka  jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC.

Wenye maua shingoni marais wa China Xi Jinping na wa Zimbabwe Robert Mugabe Picha: picture-alliance/Photoshot/Xinhua/Lan Hongguang

Nalo  gazeti  la Reutlinger  General-Anzeiger linakubaliana na tuhuma hizo na linaeleza kwamba China inawekeza mabilioni nchini Zimbabwe kwa sababu inayataka madini ya nchi  hiyo. Na kwa hivyo mtu anaweza kutuhumu kwamba atakayechukua nafasi ya Mugabe atakuwa mtu atakaye wakosha roho Wachina.

Badischen Neuesten Nachrichten

Gazeti hilo halina matumaini makubwa juu ya majenerali wa Zimbabwe. Linasema lengo la majenerali  hao ni kuyalinda maslahi yao,  baada ya Mugabe kuondolewa. Wanajeshi hao hawajali hata chembe kwamba Mugabe aliigeuza Zimbabwe kuwa nyumba  ya masikini  Kusini mwa Afrika. Ni jambo la kulitilia mashaka  iwapo kundoka kwa Mugabe kutawaletea  neema watu  wa  Zimbabwe.

Die tageszeitung

Mwandishi wa gazeti hilo Dominic Johnson anasema dunia imeshuhudia wasaa  wa kihistoria. Baada ya kutawala kwa miaka zaidi ya miaka 37 enzi ya Mugabe imefikia mwisho. Hata hivyo katika kipindi hicho Mugabe alikuwa na usemi, siyo tu nchini mwake bali barani Afrika kote.

Rais Robert Mugabe na mkuu wa jeshi la Zimbabwe Jenerali Constatino ChiwengaPicha: Reuters/Zimpapers/J. Nyadzayo

Mwandishi wa die tageszeitung anasema uzito wa  kisiasa wa Mugabe barani Afrika  haukuwa wa kawaida. Kwanza alishinda vita vya ukombozi na baadae alisimama mstari wa mbele katika kuzikabili siasa za nchi za Magharibi. Mwandishi Dominc Johnson  anasema Mugabe alizipa kisogo nchi za Magharibi ili kuonyesha muamko mpya wa kisiasa wa Waafrika. Licha ya kuiangusha nchi yake kiuchumi katika namna ya kushtusha jina la Mugabe litaingia katika vitabu vya historia na kukumbukwa kama mzalendo adhimu wa bara la Afrika.

Mabadiliko yaa hali ya hewa  

Washiriki katika mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa wa mjini BonnPicha: DW/N.Ranjan

Hali ya hewa barani Afrika inawaweka  watu wa bara hilo kati ya mvua kubwa na ukame. Gazeti la Der Tagesspiegel limemnukuu Constance Okollet kutoka Uganda, akielezea juu ya hali hiyo kwenye mkutano wa mjini  Bonn ambapo wajumbe  kutoka duniani kote waliyajadili masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa. Gazeti hilo limemnukuu  mama huyo ambaye ni mkulima , akisema, wakulima  wa Afrika hawakusababisha  mabadiliko  ya tabia  nchi lakini  wao ndio   wanaoadhibiwa. Akikumbuka yaliyotukia kwenye kijiji chake  mnamo mwaka wa 2007, Okollet aliwaambia wajumbe kwenye mkutano huo kwamba alifikiri Mungu aliwaadhibu wanakijiji hao. Bi Okollet alielezea kuwa baada ya kunyesha mvua kubwa ulifuatia  ukame uliounguza mazao yao yote. Wajumbe  kutoka Afrika waliohudhuria mkutano wa mazingira mjini Bonn walipigia debe uwezekano wa kupatiwa msaada  mkubwa zaidi  wa fedha ili kujiweka sawa na hivyo kuweza kuzikabili athari za mabadiliko ya  hali ya hewa. Hata hivyo  gazeti hilo la Der Tagesspiegel  linatilia maanani mfuko wa fedha uliopo sasa kwa ajili ya kuwasaidia  wakulima wa Afrika ambao ulianzishwa kwa mujibu wa rasimu  ya Kyoto inayofikia mwisho wake mwaka wa 2020. Gazeti  linasema mustakabali wa mfuko huo umo mashakani.

die tageszeitung

Isabel dos Santos binti yake rais wa zamani wa Angola Jose Eduardo dos SantosPicha: Reuters/E. Cropley

Makala nyingine  ya gazeti la die tageszeitung inazunngumzia hatua  ya ujasiri iliyochukuliwa  na rais mpya wa Angola Joao Lourenco ya kumwondoa kwenye madaraka tajiri mkubwa sana barani Afrika, Isabel dos Santos binti wa rais wa zama wa nchi  hiyo Eduardo dos Santos. Gazeti hilo la die tageszeitung linafahamisha kuwa rais Joao Lourenco amemwondoa Isabel Santos kwenye uongozi  wa  kampuni ya mafuta -  Sonangol inayomilikiwa na serikali ya Angola. Isabel anayekadiriwa kuwa  na utajiri wenye thamani  ya zaidi ya dola Bilioni  tatu, aliteuliwa mnamo mwaka 2016 kuwa mkuu  wa kampuni  hiyo ya mafuta. Isabel aliteuliwa na baba yake, Dos Santos aliyekuwa rais wa Angola kuanzia mwaka 1979 hadi kuondolewa kwake mwaka huu wa 2017.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba rais mpya  wa Angola Joao Lourenco amechukua  hatua  za kutia moyo tangu alipoingia madarakani. Amewaengua vigogo wengi waliokuwa mashuhuri katika  medani ya siasa nchini humo.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Saumu Yusuf

        

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW