Afrika katika magazeti ya Ujerumani
19 Januari 2018Süddeutshce Zeitung
Alipokutana na wabunge kwenye Ikulu,Trump aliuliza kwa nini Marekani ipokee wahamiaji wengi kutoka nchi alizoziita shimo la uchafu! Gazeti la Süddeutsche linaeleza kwamba kauli hiyo imezikasirisha nchi za Afrika. Umoja wa nchi hizo AU umeelezea masikitiko na ghadhabu zake. Rais wa Senegal Macky Sall amesema Waafrika wanastahiki heshima kutoka kwa wote. Inatokea kwa nadra kwa bara la Afrika kusimama pamoja kisiasa. Rais wa Ghana Nana Ado Akufo amemwambia Trump kwamba Ghana siyo shimo la uchafu na Botswana ilimtaka balozi wa Marekani nchini humo atoe ufafanuzi juu ya kauli ya Trump.
Hata hivyo gazeti hilo la Süddeutsche linakumbusha kwamba hakuna mahala ambapo Trump alishangiliwa baada ya kushinda uchaguzi kama ilivyotokea katika nchi fulani za Afrika. Nchini Sudan ushindi wake ulitathminiwa kuwa ni hatua ya kusonga mbele. Rais wa Chad Idriss Deby alimwita Trump kuwa ni kiongozi mwenye sifa kubwa. Gazeti hilo la Süddeutsche linatilia maanani kwamba viongozi wa Afrika kama vile rais Joseph Kabila wa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo na Pierre Nkurunziza wa Burundi walikuwa mstari wa mbele kumsifu Trump. Gazeti hilo linasema ilionekana kana kwamba viongozi hao wanao ng'ang‘ania mamlaka katika nchi zao, wanafaanana na Trump kivitendo.
Frankfurter Allgemeine
Gazeti la Frankfurter Allgemeine ambalo wiki hii linazungumzia juu ya kitendawili cha utajiri wa madini ya Kobalti. Katika upande mmoja madini hayo yanaleta utajiri mkubwa na katika upande mwingine yanaleta maafa. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatufahamisha kwamba raslimali hiyo inahitajika kwa ajili ya kutengenezea betri za magari. Lakini uzalishaji wake ni wa utatanishi.
Gazeti hilo linatueleza zaidi kwamba asilimia 60 ya mahitaji ya madini ya Kobalti duniani yanachimbwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mara nyingi kazi hiyo inafanywa na watoto. Bei ya madini hayo imeongezeka mara nne tangu mwaka 2014 kutoka dola 24,000 kwa tani moja hadi dola 77,000. Uchimbaji wa Kobalti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaandamana na kukiukwa haki za binadamu, kutumikishwa watoto na madhara kwa afya za watu.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine pia linasema wababe wa kivita katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametumia fedha zinazotokana na mauzo ya madini ya Kobalti kwa ajili ya kununulia silaha na kuchochea migogoro.
Die Welt
Nalo gazeti la Die Welt limeandika juu ya Niger nchi masikini kabisa duniani, lakini wakati huo huo inaongoza duniani kwa wastani wa idadi ya watoto wanaozaliwa. Gazeti linasema wanaobeba mzigo ni akina mama, kina mama hao wanakufa au wanateseka kwa maradhi ya fistula.
Kwa mujibu wa takwimu kila mwanamke nchini Niger ana watoto takriban wanane. Hali hiyo inasababisha siyo tu kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu na umasikini,bali pia inasababisha matatizo makubwa ya kiafya. Nchini humo, kimsingi hakuna huduma za afya kwa akina mama wajawazito. Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, kwa kila watu1000 nchini Niger wapo madaktari tuseme sufuri nukta mbili.
Wanawake wengi wanakumbwa na maradhi ya fistula mmoja wao ni Mamatan. Mama huyo mwenye umri wa miaka 36 ni fundi cherehani kwenye kitongoji kimoja cha mji mkuu wa Niger, Niamey, aliwahi kujifungua mara tano na alipata maradhi ya fistula. Gazeti la Die Welt limemnukuu Mamatan akisema alikuwa na majonzi mazito kwa sababu hakuna mtu aliyetaka kumkaribia, hata mumewe alijitenga naye. Gazeti hilo linafahamisha kwamba kwa bahati nzuri mama huyo alifanyiwa upasuaji na alipona kabisa.
die tageszeitung
Na gazeti la die tageszeitung linasema, tangu miaka ya 1990 waasi wa ADF wamekuwa wanafanya mashambulio kutokea kwenye milima ya Rwenzori kwenyempaka baina ya Uganda na Kongo. Gazeti hilo wiki hii linatupasha habari juu ya operesheni ya pamoja baina ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda dhidi ya waasi. Hata hivyo opereshani hiyo imesababisha taharuki katika mji wa Beni wa mashariki mwa Kongo.
Sababu ya nchi mbili hizo kuanzisha juhudi hizo za pamoja ni mpango wa kuwekeza vitega uchumi katika mradi wa uchimbaji wa mafuta kwenye mpaka baina yanchi mbili hizo. Kutokana na taharuki Wakongo wapatao 10,000 wamekimbilia Uganda tangu mwezi wa Desemba. Mwishoni mwa wiki iliyopiota Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lilianzisha mashambilo katika jimbo la Kivu kaskazini mashariki mwa nchi hiyo dhidi ya waasi wa ADF ambao chimbuko lao ni Uganda.
kamanda wa jeshi la Kongo Jenerali Marcel Mbangu akisema kuwa opereshi hiyo ndiyo itaufikisha mwisho wa waasi. Jenerali huyo amenukuliwa akisema mapambano yataendelea mpaka pale utakapopatikana usalama na amani katika mashariki mwa Kongo.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman