1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

20 Aprili 2018

Joseph Kabila ahofia uchaguzi, ndiyo sababu anajaribu kumvunja nguvu mpinzani wake mkuu. Mugabe alikuwa anapigwa na mkewe Grace, hayo ni miongoni mwa yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika.

Simbabwe neuer Präsident Mnangagwa
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Frankfurter Allgemeine

Juu ya hali ya kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema rais Joseph Kabila anahofia uchaguzi na ndiyo sababu anajaribu kumvunja nguvu mpinzani wake mkuu Moise Katumbi. Gazeti limendika kwamba Rais Joseph Kabila alipaswa kumaliza muda wake wa urais mnamo mwaka wa 2016 lakini tangu wakati huo amekuwa anaahirisha kufunga virago na vyama vya upinzani vinadai kuwa njama zake zimeitumbukiza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika vurumai.

Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph KabilaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Na sasa Kabila anapanga hila za kumvunja nguvu mpinzani wake mkuu Moise Katumbi ambaye  hapo awali alikuwa ni gavana wa jimbo la Katanga, maarufu kwa utajiri wa madini ya shaba.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Rais Kabila anajaribu kumzuia Katumbi kushiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi kwa kutumia kisingizio kwamba mwanasiasa huyo wa upinzani amechukua uraia wa Italia.

Mpinzani mkuu wa rais Kabila nchini Kongo Moise KatumbiPicha: Getty Images/F. Scoppa

Gazeti hilo linasema hilo si jambo la ajabu katika Jamhuri ya Kidemokraisa ya Kongo kwa sababu wanasiasa wengi wa nchi hiyo wanachukua uraia wa nchi nyingine ili kuweza kusafiri kwa urahisi. Hata hivyo gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba, wapinzani watadhoofika vibaya sana ikiwa Katumbi atazuiwa kugombea urais.Uchunguzi wa maoni  uliofanywa hivi karibuni ulionesha kwamba, Katumbi peke yake angelipata asilimia 24 ya kura.

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linatupeleka Zimbabwe ambako linatukumbusha siku muhimu katika historia ya nchi hiyo iliyoadhimishwa Jumatano iliyopita. Ulitimu mwaka wa 38 tangu watu wa nchi hiyo wajikomboe kuondokana na ukoloni. Juu ya maadhimisho hayo gazeti hilo linatilia maanani kwamba.

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert MugabePicha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Kwa mara ya kwanza watu wa Zimbabwe wameadhimisha siku ya uhuru bila ya Robert Mugabe kuwepo uwanjani kuhudhuria sherehe hizo. Badala yake, mgeni wa heshima alikuwa Rais Emmerson Mnangangwa aliyechukua nafasi ya Mugabe baada ya kiongozi huyo wa hapo zamani kuondolewa madarakani.

Lakini Mugabe bado anataka kuendelea kuwamo katika harakati za kisiasa za nchi yake. Gazeti hilo la Neues Deutschland limevikariri vyombo vya habari vinavyosema kuwa Mugabe anamshutumu rais Mnangagwa kwa kuingia madarakani kinyume cha sheria. Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, Mugabe amesema haitawezekana kufanyika uchaguzi huru na wa haki nchini Zimbabwe.

Rais wa Zimbabwe Emmerson MnangagwaPicha: Reuters/P. Bulawayo

Mugabe anamshambulia mshirika wake wa hapo awali siyo kwa kutoa kauli tu. Kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe anakiunga mkono chama kipya cha kisiasa kinachojiita New Patriotic Front ambacho kimejisajili kwa jina la National Patriotic Front.

Chama hicho kilichoundwa na watu waliotoka ZANU PF, chama kinachotawala nchini Zimbabwe, kinaongozwa na brigedia jenerali wa zamani Ambrose Mutinhiri. Ingawa hakuna mtu anayetarajia  kumwona Mugabe akirejea madarakani, rais huyo wa zamani wa Zimbabwe bado ataendelea kuwa na uzito wa kisiasa kwa kupitia njia ya chama kipya. Gazeti la Neues Deutschland linasema mambo hayo hayampi raha wala furaha rais  Emmerson Mnangagwa.

die tageszeitung

Lakini gazeti la die tageszeitung limeandika habari za kushtusha juu ya Mugabe. Taarifa za gazeti hilo zinasema, Mugabe alikuwa anapigwa mara kwa mara na mkewe Grace ambaye wanapishana kwa umri wa miaka 42.

Bi Grace Mugabe mke wa rais wa zamani wa Zimbabwe Robert MugabePicha: Getty Images/AFP/Z. Auntony

Kwa mujibu wa die tageszeitung, mlinzi mmoja amethibitisha kwamba, wakati mwingine, walinzi walilazimika kuwaita ndugu wa Mugabe ili waingilie kati. Mlinzi huyo alinukuliwa akisema kuwa siku  moja walinzi walituma helikopta kwa dada yake Mugabe ili aende kumsaidia nduguye. Lakini gazeti hilo limesema taarifa hizo zimekanushwa na binamu yake Mugabe, Patrick Zhuwao, aliyewahi kuwa waziri wa masuala ya jamii.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef

 

      

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW