1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

3 Agosti 2018

Wiki hii magazeti ya Ujerumani karibu yote yameandika juu ya uchaguzi mkuu wa nchini Zimbabwe uliofanyika kwa mara ya kwanza tangu Robert Mugabe aondolewe madarakani.

Simbabwe Wahlkampf Präsident Mnangagwa
Picha: Reuters/P. Bulawayo

die tageszeitung

Matokeo ya uchaguzi yalikuwa wazi kabisa kwa sababu vyama vilivyopigania uhuru vinafahamika kuwa kichwa ngumu barani Afrika. Ni vigumu kuviondoa vyama hivyo vinapokuwamo madarakani. Licha ya uchaguzi huo wa  kwanza kufanyika bila ya Robert Mugabe mshindi alijulikana  tangu mwanzoni, mgombea wa chama tawala cha ZANU-PF.

Berliner Zeitung

Gazeti la Berliner Zeitung linatilia maanani kwamba risasi zilirindima katika mji mkuu, Harare baada ya matokeo ya uchaguzi kuanza kujulikana. gazeti hilo linaeleza kwamba chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC ) kimeilaumu tume ya uchaguzi kwa kuiba kura kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo wajumbe wa Umoja wa Ulaya walioruhusiwa kuwa waangalizi wa uchaguzi huo kwa mara  ya kwanza baada ya muda mrefu, wamesema kwa jumla uchaguzi ulionyesha dalili za kutia moyo japo yalikuwapo mashaka ya kutiliwa maanani.

Wajumbe kutoka Umoja wa Afrika - AU na kutoka jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika -SADC wamesema uchaguzi huo ulifanyika kwa haki na amani na kwamba umefungua njia ya kuendeleza demokrasia nchini Zimbabwe.

Kushoto:Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa Kulia: Kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC Nelson ChamisaPicha: picture-alliance/AP Photo

Süddeutsche Zeitung

Na katika maoni yake juu ya uchaguzi wa Zimbabwe gazeti la Süddeutsche linasema hakuna mshindi wa kweli katika uchaguzi huo bali ni Wazimbabwe wengi waliokula hasara. Gazeti hilo la Süddetusche Zeitung linafafanua kwamba uchaguzi wa Zimbabwe ulipaswa kuwa huru na wa haki lakini hali haikuwa hivyo.

Chama cha ZANU-PF kiliwashinikiza watu wampigie kura mgombea wa urais wa chama hicho Emmerson Mnangagwa aliekuwa mshirika mkubwa wa Robert Mugabe kwa miaka mingi lakini mgombea wa chama cha upinzani naye pia hakujipambanua kuwa bora kwa kujitangaza mshindi kabla ya matokeo rasmi kutolewa!

die tageszeitung

Katika makala yake nyingine wiki hii gazeti la die tageszeitung linatupeleka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatuliza wafuasi wa Jean Pierre Bemba, aliyerejea nchini humo baada ya miaka 11 nje ya nchi.

Mwanasiasa wa Kongo Jean Pierre BembaPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Kooren

Gazeti hilo linaeleza kwamba baada ya kuachiwa huru na mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague ICC na baada ya kutumikia kifungo cha miaka 10 jela, Bemba amerejea nyumbani.Mwanasiasa huyo aliewahi kuwa makamu wa rais, kiongozi wa upinzani, na mbabe wa kivita katika jamhuri  ya kidemokrasia ya Kongo anawania kiti cha urais. Kurejea kwake nchini Kongo, maana  yake ni kwamba kampeni za uchaguzi zimeshaanza.

Gazeti hilo la die tageszeitung linatilia maanani kwamba  Bemba anaweza kuwa mshindani mkali katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi Desemba lakini kwanza anapaswa kuruka kiunzi cha sheria kinachoweza kumzuia kugombea urais kutokana na kuhusika na matukio fulani ya miaka iliyopita. Gazeti hilo linakumbusha kwamba katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2006 ambapo alishindana na rais Joseph Kabila, Bemba alipata asilimia 42 ya kura.

der Freitag

Na sasa tunakwenda Nigeria ambako gazeti la der Freitag linatupasha kwamba wahubiri wanatumia dini kujitajirisha.Gazeti hilo limeandika katika makala yake kuhusu kuchangisha fedha kumegeuka kuwa biashara kubwa nchini Nigeria inayofanyika kwenye makanisa na jumuiya mbalimbali.

Wahubiri wanapewa hadhi kama nyota wa muziki na fedha wanazopata zinawawezesha kusafiri kwa ndege binafsi na kuishi maisha ya kifahari. Ripota wa gazeti la der Freitag aliyeshuhudia matukio kadhaa kwenye kanisa la Covenant mjini Lagos anasema alimwona kasisi Poye Ojumade jinsi alivyokuwa anawahamasisha waumini watoe fedha ili kulichangia kanisa lake.

Waumini wakiwa KanisaniPicha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Ripota huyo amesema aliziona bahasha zilizowekwa kwenye mabechi kwa ajili ya waumini wanaotoa viwango vikubwa vya fedha. Watu hao wanazitumbukiza fedha ndani ya  bahasha hizo na wale wanaotoa fedha, kuvuka Euro 800 wanapewa  vyeti.

Ushindani ni mkubwa katika biashara hiyo ya kuitumia dini.  Wahubiri  na wale wanaojiita mitume wanalazimika kuonyesha uwezo wa kutibu magonjwa kama vile kuwapunga watu mapepo na kuwatibu walemavu kama alivyofanya bwana Yesu! Shughuli hiyo imewatajirisha wahubiri hao kwa kiasi kikubwa.

Mchungaji mmoja David Oyedepo anasemekana kuwa na utajiri unaofikia dola milioni 150.  Inapasa kutilia maanani kwamba fedha zinazotokana na michango ya kanisani hazitozwi kodi. Licha ya kujua kwamba wahubiri wanazidi kujitajirisha watu wanaendelea kutoa michango na kuwatajirisha hata zaidi!

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef       

             

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW