Afrika katika magazeti ya Ujerumani
17 Agosti 2018Frankfurter Allgemeine
Mwanasiasa huyo Robert Kyagulanyi Ssetamu anayefahamika kwa jina la usanii Bobby Wine, anazingatiwa kuwa tishio la kisiasa kwa rais Yoweri Museveni. Alikuwa anatarajiwa kuongoza msafara wa wapinzani katika mji huo wa Arua. Polisi imesema wafuasi wa Ssetamu walilipiga mawe gari la rais Museveni ambaye pia alikuwako katika mji huo kwa ajili ya shughuli za kampeni. Polisi wamesema walinzi wa rais walipiga risasi hewani ili kuwatawanya wafuasi wa mwanasiasa huyo kijana, mwenye umri wa miaka 35.
Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limewanukuu polisi wa Uganda wakisema kuwa baada ya walinzi wa rais kufyatua risasi hewani, vurumai zilitokea na mtu mmoja aliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa. Gazeti hilo pia limewanukuu walioshuhudia kuuliwa kwa dereva wa Bobby Wine wakisema gari lake halikuwako karibu na sehemu ambako wafuasi wake walikusanyika.
die tageszeitung
Nalo Gazeti la die tageszeitung pia limeandika juu ya kuuliwa kwa dereva wa Bobby Wine na limewanukuu waandishi habari wa Uganda wakikanusha taarifa ya polisi kwamba dereva huyo alipigwa risasi kwa bahati mbaya na gazeti la die tageszeitung linasema uchunguzi wa waandishi hao umebainisha kuwa dereva huyo aliuawa muda wa saa mbili baada ya msafara wa rais Museveni kuondoka mji wa Arua na kwamba helikopta ilitumiwa katika mauaji hayo yaliyofanyika karibu na hoteli ambako Bobi Wine alikuwa amefikia.
Neue Zürcher
Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kong, rais Joseph Kabila alitangaza hatagombea tena wadhifa wa urais. Lakini gazeti la Neue Zürcher linasema mamlaka yataendelea kuwamo katika mikono yake. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba watu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamefurahishwa na mpango wa rais Kabila wa kung'atuka lakini furaha yao siyo ya kuonyesha magego. Sababu ni kwamba Kabila ameshawapachika watu wake katika sehemu muhimu za utawala, na atakayegombea urais mnamo mwezi wa Desemba ni mshirika wake wa karibu. Mgombea huyo Emmanuel Ramazan Shadary hadi mwezi wa Februari alikuwa waziri wake wa mambo ya ndani na usalama.
Die zeit
Gazeti la Die Zeit limechapisha makala inayojadili sababu ya kuzuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Afrika. Mshiriki mmoja katika mjadala huo Gero Von Randow amesema ukoloni ndiyo uliosababisha dhiki inayowafanya vijana wajaribu kuhamia Ulaya. Lakini washiriki wengine kwenye mjadala huo wanaipinga hoja hiyo.
Washiriki wengine kwenye mjadala huo wamesema udhalimu uliofanyika wakati wa ukoloni barani Afrika hauwezi kuwa sababu ya kuwafanya vijana walikimbie bara lao leo hii. Lakini bwana Gero von Randow anaesema ukoloni umechangia katika kusababisha mgogoro mkubwa wa wakimbizi ameeleza kuwa mizizi ya migogoro barani Afrika ilipandikizwa na wakoloni, na hata iking'olewa inaota tena! Washiriki wa mjadala wanaopinga tathmini ya bwana Gero von Randow wamesema ziko tofauti miongoni mwa nchi zilizokandamizwa kwa ukoloni barani Afrika.
Katika makala iliyochapishwa na gazeti la Die Zeit inaeleza kwamba baadhi ya nchi barani Afrika kama Botswana inafikia ustawi imara wa uchumi. Pato la wastani linafikia takriban dola 8000 kwa mwaka yaani mara 16 ya pato la wastani katika nchi jirani ya Zimbabwe. Wamekumbusha kwamba ilipopata uhuru wake mnamo mwaka 1966, Botswana ilikuwa na kilometa 12 tu za barabara za lami na pia ilikuwa na watu 22 tu waliokuwa na shahada za vyuo vikuu.
Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Josephat Charo