Afrika katika magazeti ya Ujerumani
24 Agosti 2018Süddeutsche Zeitung
Gazeti la Süddeutsche linatilia maanani kwamba katika muhula wake wa pili rais Ibrahim Boubacar Keita ataendelea kukabiliwa na changamoto zinazotokana na ugaidi na hali mbaya ya kiuchumi. Mali bado inapambana na tishio linalotokana na harakati zinazoendeshwa na Wataureg wanaotaka kujitenga. Sehemu ya Wataureg iliyoko kaskazini mwa Mali inayoitwa Azawad imegeuka kuwa kituo kikuu ambapo magaidi wanakusanyika. Licha ya juhudi za kulinda amani na kujaribu kuleta utulivu zinazofanywa na jeshi la Umoja wa Mataifa nchini humo, haikuwezekana kuwazuia magaidi kuingia katikati ya nchi hiyo, kutokea kaskazini.
Gazeti la Süddeutsche linakumbusha kwamba mkataba wa amani ulitiwa saini baina ya serikali na waasi wa kaskazini, mnamo mwaka 2015, lakini bado haujaleta matunda mpaka leo. Gazeti hilo pia linasema hali ya kiuchumi nchini siyo nzuri. Idadi kubwa ya watu hawana ajira na takriban nusu ya wananchi wanaishi kwa kipato cha wastani wa chini ya dola 2 kwa siku. Changamoto zitakuwa kubwa kwa rais Boubakar Keita ambaye sasa ana umri wa miaka 73.
Frankfurter Allgemeine
Waziri wa Ujerumani anayeshughulikia misaada ya maendeleo, Gerd Müller anadhamiria kusaidia barani Afrika na atafanya ziara katika nchi saba za bara hilo mnamo wiki hii, lengo la ziara ya waziri Müller ni kuiendeleza ajenda ya mpango wa Marshall unaolenga shabaha ya kuharakisha maendeleo ya uchumi barani Afrika na hivyo kutoa jawabu la mambo yanayowafanya vijana wa Afrika walihame bara lao na kukimbilia Ulaya.
Frankfurter Allgemeine linasema katika makala yake kwamba Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller ameanzisha kitengo cha mpango wa Marshall kwenye ziara yake mahsusi kwa ajili ya kufanya kazi bega kwa bega na nchi za Afrika ili kuharakisha maendeleo ya uchumi ya bara hilo. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limefahamisha kwamba Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atawaalika viongozi kadhaa wa Afrika kushiriki kwenye mkutano ambapo watajadili maendeleo ya nchi zao katika msingi wa pendekezo la kundi la nchi 20.
Berliner Zeitung
Nalo gazeti la Berliner limeandika juu ya ziara aliyofanya rais wa Angola Joao Lourenco nchini Ujerumani mnamo wiki hii. Mwenyeji wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alimhakikishia mgeni wake kwamba kampuni za Ujerumani zitawekeza vitega uchumi vya thamani ya zaidi ya bilioni moja nchini Angola. Gazeti hilo linatilia maanani katika makala yake kwamba Ujerumani na nchi za Ulaya zinapaswa kuziba pengo kubwa na linaeleza kwamba kiini cha mazungumzo kati ya Kansela Merkel na rais wa Angola Joao Lourenco kilikuwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi zao.
Kwa muda wa miaka mingi China imekuwa inawekeza vitega uchumi kwa kiwango kikubwa katika nchi za Afrika. Ndiyo sababu kwenye mazungumzo yake na rais wa Angola, Kansela Merkel alisisitiza umuhimu wa bara la Afrika. Kwa sasa Ujerumani haimo hata miongoni mwa nchi 10 zinazowekeza kwa kiwango kikubwa katika bara la Afrika.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung pia linakumbusha kwamba rais wa Angola Joao Lourenco aliahidi kupambana na rushwa mara tu baada ya kuingia madarakani mwaka uliopita. Je, amefikia wapi katika kuitekeleza ahadi hiyo. Gazeti hilo linatupasha kwamba watu wa Angola wamezidi kutia mashaka iwapo rais Joao Lourenco anayo dhamira ya kweli ya kuing'oa mizizi ya ufisadi nchini mwake kama alivyoahidi. Wakati wa utawala wa Rais Jose Eduardo Dos Santos, watoto wake, majenerali na wanasiasa waliokuwa karibu yake walijitajirisha bila ya kifani. Binti yake Dos Santos, aliyekuwa mkuu wa kampuni ya mafuta ya serikali, Isabel anakadiriwa kuwa na utajiri wa thamani ya dola za Marekani bilioni 2.6.
Gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba, rais Joao Lourenco amewaondoa mafisadi serikalini, ikiwa pamoja na Isabel. Lakini gazeti hilo limewanukulu watu wa Angola wakisema, ikiwa rais wao kweli ana dhamiria kuwakabili mafisadi, kwa nini mama huyo, Isabel bado hajafikishwa mahakamani?
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Josephat Charo