1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

31 Agosti 2018

Magazeti ya Ujerumani yamezingatia juu ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Senegal, Ghana na Nigeria na pia jitihada za Tchad za kuwasaidia wakimbizi kutoka nchi jirani ya Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

Ghana - Angela Merkel und Präsident Nana Akufo-Addo
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Handelsblatt

Gazeti la Handelsblatt linasema katika ziara kwenye nchi hizo Kansela Merkel anataka kuweka mkazo juu ya ushirikiano wa kiuchumi kwa lengo la kuwapa vijana wa Afrika mustakabal mzuri na hivyo waweze kubakia katika nchi zao. Jinsi kansela Merkel anavyosisitiza umuhimu wa ziara katika nchi hizo tatu inadhihirika katika ujumbe wa ngazi za juu unaotolewa na wasimamizi wa kampuni maarufu ikiwa pamoja na ile ya Siemens.

Gazeti la Handelsblatt linaongezea kwa kusema ziara ya Kansela Merkel inawakilisha matarajio makubwa ya kiuchumi barani Afrika. Limemnukulu Stefan Liebing mwenyekiti wa chama cha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Afrika na Ujerumani akisema kuwa nchi za Afrika zimekuwa zinasubiri kwa muda mrefu kuona kauli zilizotolewa juu ya ushirikiano wa kiuchumi zikitekelezwa. Mwenyekiti huyo bwana Liebig ameingiwa matumaini kwamba sasa hatua thabiti zitachukuliwa.

Neues Deutschland

Nalo gazeti la Neues Deutschland limesema mipango ya Ujerumani yenye lengo la kuisaidia Afrika kiuchumi itatoa mchango katika kuwazuia vijana wa bara hilo wanaohatarisha maisha yao ili kukimbilia barani Ulaya.Gazeti hilo linatilia maanani kwamba hii ni mara ya tatu kwa Kansela Merkel kufanya ziara barani Afrika ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi za bara hilo. Gazeti hilo la Neues Deutschland linasema maendeleo ya kiuchumi ni muhimu kwa Afrika kwa sababu yatachangia katika kuepusha baa la vijana kujiingiza katika hatari ya kuvuka bahari ili kukimbilia Ulaya.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akikagua gwaride la heshima nchini GhanaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaiangazia Tchad na linasema licha ya umasikini, nchi hiyo inawasaidia wakimbizi na linaeleza kwamba zaidi ya asilimia 80 ya watu milioni 15 wa nchi hiyo wanaponea kwenye kilimo cha jembe la mkono lakini umasikini umeongezeka baada ya bei ya mafuta kuanguka duniani. Frankfurter Allgemeine linaeleza zaidi juu ya nchi hiyo iliyoko kwenye ukanda wa Sahel na linasema, Chad inawahifadhi wakimbizi kutoka nchi za jirani kwenye kambi iliyoko kusini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wakimbizi wamewekwa katika nyumba ndogo ndogo za mabati zipatazo 150 katika kambi inayoitwa Silambi. Wapo wakimbizi wapatao 6000 katika maeneo ya Kusini mwa Chad ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vinandelea kwa miaka mitano sasa. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limemnukulu mkuu wa jimbo la Moissala la kusini mwa Chad Robert Ndoubadegue akieleza kuwa katika jimbo hilo lenye wenyeji 300,000 wapo wakimbizi 6000 kutoka nchi jirani ya Jamhuriya Afrika ya Kati.

der Freitag

Gazeti la der Freitag linazingatia matukio ya kutia moyo tangu waziri mkuu mpya nchini Ethiopia Abiy Ahmed aingie madarakani. Miongoni mwa matukio hayo ni kurejea nchini humo kwa mwanaharakati Jawar Mohammed aliyekuwa anaishi Marekani kama mkimbizi. 

Hadi miaka miwili tu iliyopita mwanaharakati huyo kutoka kabila la Oromo alikuwa anaitwa gaidi na serikali ya Ethiopia. Lakini sasa kutokana na mageuzi ya kisiasa ameweza kurejea nchini humo na kulakiwa kwa shangwe kubwa. Gazeti la der Freitag linasema mwanaharakati huyo Jawar Mohammed alianzisha mtandao wa kijamii, Oromia Media wakati akiwa nchini Marekani alioutumia kuendeshea harakati za kudai haki nchini Ethiopia.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Reuters/T. Negeri

Gazeti hilo la der Freitag linaeleza kwamba aliyokuwa anasema kwenye mtando wake yalikuwa na uzito mkubwa sana. Jawar Mohammed mnamo mwaka 2016 alifanikiwa kuwahamasisha watu wafanye maandamano ya kuipinga serikali ndipo serikali ya Ethiopia ililazimika kutangaza hali ya hatarina kumtangaza mwanaharakati huyo kuwa ni gaidi.

Hata hivyo sasa amerejea nchini Ethiopia na ameeleza kuwa aliutumia mtandao wa kijamii wa Oromia Media ili kuhamasisha harakati za kuipinga serikali. Jawar Mohammed amesema serikali haikuwa na budi ila kukubali mageuzi. Kurejea kwake nyumbani salama salimini ni sehemu ya mafanikio ya mageuzi ya waziri mkuu mpya Abiy Ahmed ambaye pia anatokea katika jimbo la Oromo.

Mwandishi: Zainab Aziz/ Deutsche Zeitungen

Mhariri: Iddi Ssessanga

       

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW