1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

14 Septemba 2018

Ahadi iliyotolewa na wale waliokuwa wanapora utajiri wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haiaminiki, haya yameandikwa na gazeti la Süddeutsche kwenye makala ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph KabilaPicha: Reuters/K. Katombe

Süddeutsche Zeitung

Ahadi hiyo imetolewa na rais Joseph Kabila. Anataka kuyatekeleza yale ambayo marais  waliotangulia hawakuweza kuyafanya katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Mapema mwaka huu rais Kabila alitia saini sheria yenye lengo la kuleta haki kwa watu wa Kongo. Kwa mujibu wa sheria hiyo kampuni zote za nje zinazozalisha madini nchini Kongo zitapaswa kulipa kodi kubwa. Gazeti la Süddeutsche linatufahamisha kwamba kampuni za nje zinaipinga vikali sheria hiyo lakini linasema rais Kabila amesimama kidete na limemnukuu msemaji wake akieleza kwamba watu wa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo wanaitaka sheria hiyo kwa sababu itaiwezesha serikali kuingiza fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Vijana wa Kongo wakiwajibika kwenye migodiPicha: Getty Images/AFP/J. Cartillier
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph KabilaPicha: Reuters/K. Katombe

Lakini Gazeti la Süddeutsche lina mashaka na linauliza Jee! ghafla tu mambo yanaweza kubadilika katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo? Kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 dola zipatazo milioni 750 zilizotokana na mauzo ya madini zilipotea. Rais Kabila ni kizazi kipya cha wale ambao wamekuwa wanaitawala Kongo kwa miongo kadhaa na kwa hiyo amekuwa anaimarishwa na wafanyabiasha kutoka nje wanaonufaika na raslimali za Kongo.

Die Zeit

Nalo gazeti  la Die Zeit wiki hii limeandika juu ya kuongezeka kwa idadi ya vijana wanaowania kuwa wajasiriamali nchini Nigeria wanaowahamasisha wawekezaji vitega uchumi kutoka nje. Lengo ni kuhakikisha kwamba vijana wa nchi hiyo wanabakia nyumbani badala ya kwenda nchi za nje. Wajasiriamali vijana wa Nigeria wanachukua hatua.

Gazeti hilo la Die Zeit linaeleza kwamba, kwa vijana wa Nigeria kuondoka nchini mwao ni uamuzi wa mwisho kabisa. Hata hivyo vijana wa Nigeria wapatao 40,000 mwaka uliopita waliomba hifadhi ya ukimbizi katika nchi za Umoja wa Ulaya. Nchini Ujerumani pekee asilimia 6.5 ya wakimbizi walioomba hifadhi walitoka Nigeria. Mwanzilishi wa kampuni inayoitwa Andela Nadar Enegesi anataka kuleta mabadiliko. Ameanzisha kampuni inayotoa vijana wanaokwenda kufanya kazi duniani kote.

Mwanamama mjasiriamali wa Nigeria Picha: P. U. Ekpei/AFP/Getty Images

Gazeti la Die Welt linaeleza kwamba kutokana na bidii ya kampuni hiyo idadi ya wawekezaji vitega uchumi kutoka nje imeongezeka nchini Nigeria na linatilia maanani kuwa shughuli za kampuni hiyo pia zimewavutia wawekezaji vitega uchumi kutoka Ujerumani, linasema miongoni mwa wafanyabiashara mashuhuri walioongozana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika ziara yake ya nchini Nigeria alikuwa mkuu wa kampuni maarufu ya Siemens, Joe Kaeser.

Mjasiriamali huyo kutoka Nigeria kijana Enegesi pamoja na wenzake watano waliunda kampuni yao hiyo ya Andela mnamo mwaka 2014 na tangu wakati huo wameshatoa ajira 1000 kwa watengenezaji wa programu za kompyuta. Lengo ni kuongeza idadi na kufikia milioni moja hadi hapo mwaka 2024.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: picture-alliance/AA/M.W. Hailu

Neue Zürcher

Baada ya kupigana vita katika miaka 10 ya uhasama kati yao, Djibouti na Eritrea zinakusudia kusawazisha uhusiano wao. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la Neue Zürcher mnamo wiki hii. Gazeti hilo linaeleza kwamba mnamo mwezi Julai kiongozi wa Eritrea Isaias Afewerki na waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed waliishangaza dunia baada ya kufikia makubaliano ya haraka juu ya kusawazisha uhusiano kati ya nchi zao zilizoko kwenye pembe ya Afrika.

Ni wazi kwamba makubaliano kati ya Eritrea na Ethiopia yamechangia katika kuleta amani baina ya Djibouti na Eritrea. Gazeti la Neue Zürcher limemnukulu waziri wa mambo ya nje wa Djibouti Abdoulkader Kamil Mohamed akitabiri kwamba pembe ya Afrika itazidi kuwa eneo la amani. Hata hivyo gazeti hilo linauliza iwapo mchakato huo wa amani utafika hadi Somalia kwenye mgogoro mkubwa kabisa katika eneo hilo la pembe ya Afrika? 

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW