1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

12 Oktoba 2018

Muktasari wa masuala na matukio ya barani Afrika uliozingatiwa na magazeti ya  Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na uamuzi wa rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wa kumteua waziri mpya wa fedha Tito Mboweni.

Nigeria - Heimkehr der Chibok Mädchen
Picha: picture alliance/dpa/AP/unday Aghaeze/Nigeria State House

Frankfurter Allgemeine

Waziri huyo wa zamani bwana Nhlanhla Nene aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa rais Ramaphosa ambae mapema mwaka huu alifanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri. Hadi mwezi wa Februari waziri mpya fedha Tito Mboweni alisema kwamba hakuwa tayari kuzungushwa zungushwa kama mpira katika kikosi kilekile cha mawaziri. Alisema wakati ulishafika wa kutoka kwenye baraza la mawaziri na badala yake kufanya kazi ya kutoa ushauri kwa vijana lakini Mboweni aliapishwa jumanne iliyopita kushika wadhifa wa waziri wa fedha.

Kushoto: Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Kulia: Waziri mpya wa fedha Tito MboweniPicha: picture alliance/AP Photo

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema uamuzi wa rais Ramaphosa wa kumwondoa bwana Nene ni sahihi kabisa. Gazeti hilo linasema waziri mpya atarejesha imani wakati ambapo Afrika Kusini imo katika mdororo wa uchumi, na wakati ambapo chama tawala cha ANC kimegawanyika kutokana na kashfa za ufisadi za rais wa hapo awali Jacob Zuma. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba katika uongozi wa Mandela, bwana Mboweni alikuwa waziri wa ajira lakini aliamua kujiweka mbali na siasa wakati wa utawala wa Zuma. Uamuzi huo umemjengea imani miongoni mwa wananchi na wawekazaji vitega uchumi nchini Afrika Kusini na nje ya nchi hiyo.

Aliyekuwa waziri wa fedha Nhlanhla Nene amefyekwa na rais Ramaphosa katika juhudi za kiongozi huyo za kukabiliana na kashfa ya ufisadi  iliyosababishwa na familia ya akina Gupta ndani ya serikali ya Afrika Kusini.

 die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung wiki hii linakumbusha juu ya juhudi za kuwakomboa wasichana wa Nigeria waliotekwa nyara Aprili 2014. Juhudi hizo zinafanywa na Oby Ezekwesili maarufu kwa kampeni aliyoanzisha pamoja na marafiki zake wawili inayoitwa "Bring back  our Girls". Pamoja na juhudi hizo mama huyo pia anawania kiti cha urais. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba Ezekwesili na wanzake wanakutana kila siku ili kuindeleza kampeni ya kutaka kuachiwa kwa wasichana 276 wa Chibok.

Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Song

Wasichana hao walitekwa nyara na magaidi wa kundi la Boko Haram. Ezekwesili amesema hatakaa chini mpaka hapo wasichana hao watakapokombolewa. Vuguvugu la Bring back our Girls yaani turudishieni wasichana wetu bado linaendelea ingawa idadi ya washiriki imepungua. Viongozi wa Nigeria kuanzia rais wa hapo awali Goodluck Jonathan hadi rais wa sasa Muhammadu Bohari wamekuwa wanagwaya juu ya mama huyo ambaye ni mke wa kasisi wa kanisa mojawapo kubwa katika jimbo la  Ambara nchini Nigeria.

Gazeti hilo la die tageszeitung linaendelea kuandika kwamba viongozi hao walitumia idara za usalama kwa lengo la kumyamazisha mama huyo. Oby Ezekwesili alinyang'anywa pasipoti yake. Hata hivyo hawakufanikiwa na badala yake amepata umaarufu duniani.Na sasa anataka kugombea kiti cha urais katika uchaguzi utakaofanyika nchini Nigeria mwaka ujao. Gazeti la die tageszeitung linakumbusha kwamba mama huyo si mgeni katika medani ya kisiasa kwani  aliwahi kuwa  mkaguzi  wa mambo  ya kiuchumi wakati wa utawala  wa rais Oluseguni Obasanjo. 

Mwandishi:Zainab Aziz/ Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW