1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

9 Novemba 2018

Gazeti la die tageszeitung linazungumzia juu ya Madagascar ambako uchaguzi wa rais umefanyika mnamo wiki hii. Gazeti hilo linasema yeyote atakayeshinda katika uchaguzi huo atakumbana na changamoto kubwa.

Madagaskar Wahlen Wahlkampf in einem Slum von Antananarivo
Picha: Getty Images/AFP/Rijasolo

die tageszeitung 

Gazeti hilo la die tageszeitung linakumbusha kwamba hadi wakati ilipopata uhuru wake mnamo mwaka 1960 Madagascar ilikuwa na hali nzuri kama Malaysia au Brazil lakini leo nchi hiyo ni miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani. Gazeti hilo linasema asilimia 90 ya watu wake milioni 25 wamo katika dimbwi la umasikini mkubwa, huku raslimali za nchi hiyo zikizolewa na wawekezaji vitega uchumi wasiojua hata kutahayari na linaendelea:

Wanasiasa wanaowania urais ni pamoja na Marc Ravalomanana ambaye hapo awali aliipiga mnada nchi yake. Mgombea mwengine ni Andry Rajoelina ambaye hapo awali aliitenga nchi yake na jumuiya ya kimataifa. Na mwengine ni Herry Rajaorimampianina aliyekuwa waziri wa fedha, ambaye gazeti linasema hana lolote jipya analoweza kuwasilisha. Gazeti hilo la die tageszeitung linaeleza kwamba Madagascar itapoteza fursa ya kujijenga upya ikiwa wanasiasa hao watatu watarudi tena katika uongozi.

Berliner Zeitung

Gazeti la Berliner linatufahamisha kwamba mwanaharakati maarufu wa Uganda Bobi Wine anadhamiria kuwa rais wa nchi hiyo lakini gazeti linasema anaijua hatari iliyopo. Bobi Wine ambaye pia ni mwanamuziki maarufu nchini Uganda, yeye mwenyewe amesema mambo yatakuwa magumu kwa sababu ya kuandamwa na hata kutiwa ndani. Mwanaharakati  huyo mwenye umri wa miaka 36 amesema baadhi  ya wafuasi wake pia wanaweza kuuliwa.

Gazeti hilo la Berliner linatujulisha kwamba wafuasi wa mwanaharakati huyo anayeitwa rasmi Robert Kyagulanyi Ssentamu anafahamika kama rais wa vibandani. Mwaka uliopita alifanikiwa kuingia bungeni na tangu wakati huo amekuwa anajenga  na kuimarisha umaarufu wake licha ya vitisho. Gazeti  la Berliner linatilia  maanani:

Mwanasiasa, mwanamuziki na pia mwanaharakati Bobi Wine wa UgandaPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Sampson

Harakati za kisiasa zinazoendeshwa na Bobi Wine sio jambo linalotokea nchini Uganda pekee. Katika nchi kadhaa za Afrika vijana wanajitokeza ili kutetea haki ingawa bara la Afrika linajulikana kuwa maskani na vijana wenye umri wa wastani wa miaka 19, nchi zao zinaongozwa na wazee kama Yoweri  Museveni ambaye sasa ana umri wa miaka 74.

Gazeti la Berliner linaelezea matumaini juu ya kufanikiwa kwa harakati za Bobi Wine kwa kutoa mfano wa kile kilichotokea katika nchi nyingine za Afrika kama vile Burkina Faso ambako vijana walifanikiwa kumwangusha dikteta Blaise Compaore. Gazeti hilo linasema rais Museveni analijua hilo vizuri na atajipanga wakati Bobi Wine atakapoendesha kampeni yake kwa kutumbuiza kwenye uwanja wa kandanda wa mjini Kampala.

Frankfurter Allgemeine

Taarifa za mafanikio juu ya juhudi za kupambana na maradhi ya ukimwi zinatoka Namibia mnamo wiki hii. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limefanya mahojiano na mke wa rais bi Monica Geingob. Mama huyo ameeleza kwamb hali ya maradhi hayo ilikuwa mbaya, mnamo siku za kwanza baada ya Namibia kujipatia uhuru wake. Waliokuwa wanaugua maradhi hayo walitengwa na jamii. Mtu yeyote aliyeonekana kuwa amepungua uzito alituhumiwa kuwa na ugonjwa huo. Hali imebadilika sasa kutokana na juhudi zinazofanyika ndani ya Namibia pamoja na msaada wa kimataifa, kasi ya maambukizi imepungua sana.

Rais wa Namibia Hage GeingobPicha: picture-alliance/Xinhua/W. Changwei

Mke huyo wa rais wa Namibia ameliambia gazeti la Frankfurter Allgemeine kwamba mgonjwa wa ukimwi wa kwanza aliyekutana naye alikuwa jamaa yake ambaye alikufa baada ya muda mfupi. Na  mwengine ameeleza alikuwa rafiki yake ambaye pia alikufa haraka lakini amesema alikutana na mgonjwa wa tatu wa ukimwi katika mazingira tofauti kabisa. Mke huyo wa rais ameeleza:

Alikutana na mtu huyo wa tatu muda mfupi tu baada ya kupimwa na kubainika kuwa alikuwa na virusi vya ukimwi. Bibi Monica Geingob amesema mgonjwa huyo hakuwa na wasiwasi juu ya kifo kwa sababu, hatua kubwa imepigwa katika kuwasaidia watu wanaoathirika. Mama huyo ameliambia gazeti la Frankfurter Allgemeine kwamba asilimia 90 ya watu wanajijua kwamba wanayo maradhi hayo na asilimia 90  wanapatiwa tiba. Amesema hatua hiyo iliyofikiwa,  ndiyo msingi wa kuzuia maambukizi  nchini Namibia.

mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW