1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

1 Februari 2019

Masuala na matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na makala juu ya hali ya nchini Sudan na pia juu ya ukatili dhidi raia nchini Zimbabwe.

Sudan Rede von Präsident Omar al-Bashir
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Frankfurter Allgemeine

Maandamano ya kuupinga utawala wa rais Omar al-Bashir yanaongezeka na hakuna kinachoonyesha iwapo yatazimika karibuni. Waandamanaji hao wanamtaka rais Omar al- Bashir ang'atuke lakini hakuna dalili ya kuonyesha iwapo atafanya hivyo. Rais al-Bashir ndiyo kwanza anasema panya warudi kwenye mashimo yao, akimaanisha waandamanaji hao. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba Urusi na Uturuki zinamuunga mkono rais huyo. Nchi hizo zimesema zitampa msaada Omar al Bashir. Rais huyo amekuwamo madarakani kwa miaka 29 sasa.

Gazeti hilo pia limeinukulu ripoti ya shirika la televisheni la Aljazeera inayosema kuwa maandamano ya kumpinga rais Omar al Bashir yameenea nchini Sudan kote.

Süddeutsche Zeitung 

Wiki hii,gazeti hilo linaturudisha nchini Zimbabwe ambako linasema rais mpya ameirudia mikakati ya zamani na linaeleza. Rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangangwa aliingia madarakani na ilani ya kuleta hali bora kwa watu wa Zimbabwe tofauti na yale yaliyofanywa na rais wa hapo awali Robert Mugabe. Lakini ukweli ni kwamba waandamanaji wanaopinga kupandishwa bei ya mafuta wanatendewa ukatili na maafisa wa usalama. Polisi na wanajeshi wanafanya ukatili katika kuwakabili waandamanaji japo Mnangagwa ameahidi kuwachukulia hatua polisi waliofanya ukatili huo.

Gazeti la Süddeutsche linasema rais Mnangagwa amejitetea kwa kueleza kwamba ilikuwa lazima kupandisha bei ya mafuta ili akiba ya mafuta nchini iweze kuwa ya uhakika. Hata hivyo gazeti hilo linakumbusha kwamba rais Mnangagwa ameahidi kuleta mapya nchini Zimbabwe lakini yeye mwenyewe ni mtu wa utawala wa zamani, aliyemtumikia Mugabe kwa muda wa miaka mingi. Mnangagwa alikuwa waziri wa usalama aliyekuwa anashika fagio kwa niaba ya Robert Mugabe.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher wiki hii linazungumzia juu ya kitendawili kilichopo nchini Ethiopia, linasema katika upande mmoja Ethiopia inastawi kiuchumi kwa asilimia zaidi ya 10 lakini katika upande mwingine upinzani dhidi ya serikali umekuwa unaongezeka mnamo miaka iliyopita. Jee! mambo yamebadilika tangu kuingia madarakani kwa waziri mkuu Abiy Ahmed? Gazeti la Neue Zürcher linasema kuwa mabadiliko anayofanya pia yana gharama zake na linaeleza kwamba hadi mnamo miaka ya hivi karibuni Ethiopia ilikuwa inaambatanishwa na umaskini na njaa lakini tangu mwanzoni mwa karne hii nchi hiyo imekuwa inastawi kiuchumi kuliko nyingine yoyote duniani.

Mashirika ya misaada ya kimataifa yameisifu Ethiopia kwa juhudi za kupambana na umasikini kutokana na ustawi wake wa uchumi. Lakini katika upande mwingine upinzani dhidi ya serikali umekuwa unapamba moto. Gazeti  hilo la Neue Zürcher linafahamisha kwamba watu wamefanya maandamano kupinga kutaifishwa kwa ardhi zao na kubaguliwa kwa makabila fulani linasema hali hiyo inasababisha wasiwasi wa kuzuka ghasia kubwa lakini linatilia maanani kwamba mwaka mmoja tangu waziri mkuu Abiy Ahmed aingie madarakani, hatari ya kuzuka ghasia imeepushwa.

Ujio wake umeleta mabadiliko ya kimsingi. Waziri mkuu Abiy Ahmed amethibitika kuwa mtetezi mkubwa wa mageuzi. Amewafungulia wafungwa wa kisiasa, amemaliza uhasama na nchi jirani ya Eritrea na anaendeleza mageuzi ya kiuchumi na ameondoa hali ya hatari. Hata hivyo gazeti la Neue Zürcher linatahadharisha kwamba kuondolewa kwa mfumo wa ukandamizaji kumeufunua mfuniko uliokuwa unafunika mivutano ya kikabila. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba tangu waziri mkuu Abiy Ahmed aingie madarakani mivutano ya kikabila imeongezeka hasa kwenye sehemu za mipakani ambako damu inavuja mara kwa mara.

Gazeti hilo linasema katika sehemu fulani mashambulio ya kulipiza kisasi yanafanyika. Wanaoshambuliwa ni watu wa kabila la waliokuwa watawala wa hapo awali nchini Ethiopia. Mamia ya watu wameshauawa na mamilioni wametimuliwa kutoka kwenye makaazi yao na wamelazimika kukimbilia kwenye sehemu nyingine za nchi. Gazeti la Neue Zürcher limewanukulu wataalamu wanaosema kuwa cheche ndogo tu inaweza kuwasha moto mkubwa nchini Ethiopia.

 

Mwandishi:Zaianab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW