1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
14 Agosti 2020

Matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na mazungumzo ya serikali za Namibia na Ujerumani juu ya mauaji ya halaiki ya watu wa makabila ya Herero na Nama.

Namibia Windhuk | Denkmal zur Erinnerung an den Völkermord an den Herero und Nama
Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya mauaji ya halaiki ya watu wa makabila ya Herero na Nama nchini Namibia yaliyofanywa na wakoloni wa kijerumani mnamo mwaka 1904. Gazeti hilo linafahamisha kwamba tangu miaka mitano iliyopita, mazumngumzo yamekuwa yanafanyika baina ya serikali za Namibia na Ujerumani hasa juu ya masuala mawili. Kwanza Ujerumani ilipe fidia na pili iombe radhi rasmi kwa mauaji ya halaiki ya waherero na wanama.

Gazeti la die tageszeitung linasema Ujerumani imekubali kuomba radhi rasmi lakini inakataa kutumia neno la fidia. Serikali ya Ujerumani imesema inatambua wajibu wake wa kisiasa na kimaadili juu ya Namibia lakini imesema kwamba suala la maangamizi ya waherero na wanama halina msingi wa kisheria.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya ufisadi katika nchi za Afrika na juhudi za kupambana na baa hilo.Hata hivyo gazeti hilo limenukulu uchunguzi uliofanywa nchini Nigeria ulionyesha kwamba juhudi hizo zinaendeleza ufisadi. Gazeti  la Neue Zürcher linasema kwamba wataalamu wanakubaliana kuwa ufisadi unaleta umasikini katika  nchi kwa sababu unazuia maendeleo.

Gazeti hilo linaeleza kwamba katika kupambana na ufisadi, juhudi zinaelekezwa katika kuzitaka nchi zitunge sheria dhidi ya uovu huo. Hata hivyo gazeti linatilia maanani kwamba njia hiyo haijaleta mafanikio katika nchi nyingi kwa sababu viongozi ndio wanaonufaika na mifumo  ya rushwa.

Neue Zürcher limemnukulu mwanaharakati maarufu John Githongo ambae kwa miaka mingi amekuwa anapambana na ufisadi nchini Kenya, akieleza kuwa kampeni za kupinga rushwa zinaishiwa upepo haraka. Amenukuliwa na gazeti la Neue Zürcher akifafanua kwamba watawala wanapindisha sheria kwa ajili ya  maslahi yao. Gazeti la Neue Zürcher limewanukulu watafiti wanaosema kwamba mfumo mzuri wa kulipa kodi unaweza kuwa njia ya ufanisi ya kupambana na ufisadi.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linauliza iwapo bara la Afrika limenusurika maafa makubwa ya maambukizi  ya virusi vya corona? Gazeti hilo linasema maambukizi yameenea duniani kote lakini idadi ya maambukizi  na vifo ni ndogo barani Afrika. Gazeti la Frankfurter linatilia maanani kwamba watu zaidi ya milioni 20 wameambukizwa virusi vya corona duniani. Gazeti hilo linasema wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza walitabiri vifo vya mamilioni ya watu barani Afrika kutokana na maambukizi hayo lakini linasema wataalamu hao wameshangazwa! 

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema licha ya kuwepo mazingira yanayoweza kusababisha kusambaa haraka kwa maambukizi, mpaka sasa ni watu wapatao milioni moja walioambukizwa na waliokufa ni 10,500  barani Afrika kote baada ya kupita muda wa miezi mitano. Gazeti hilo linakumbusha kwamba nchi nyingi za Afrika zilichukua hatua haraka za kudhibiti maambukizi, ikiwa pamoja na kufunga mipaka mapema.

Neues Deutschland 

Tunakamilisha kwa makala ya gazeti la Neues Deutschland juu ya mwanasiasa chipukizi Bobi Wine anayewania kiti cha urais nchini Uganda katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Gazeti hilo linasema Bobi Wine aliyeanzisha chama kipya cha kisiasa anatarajia kumpa changamoto rais Yoweri Museveni ambaye amekuwamo madarakani nchini Uganda kwa muda wa miaka 34. 

Gazeti la Neues Deustchland linaeleza kwamba kwa muda mrefu sasa Bobi Wine ambaye pia ni mwanamuziki maarufu, amekuwa anaongoza harakati za nguvu ya umma zenye lengo la kumwondoa rais Yoweri Museveni. Hata hivyo gazeti linasema bila ya wapinzani kusimama pamoja itakuwa vigumu kumwondoa Museveni. Gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba Museveni bado anaungwa mkono kwa kiwango kikubwa na watu wa sehemu za mashambani.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen