1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
11 Desemba 2020

Yaliyoandikwa juu ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na uchaguzi wa nchini Ghana, kampeni za uchaguzi wa rais nchini Uganda na wasiwasi juu ya kuongezeka umasikini barani Afrika.

Afrika Ghana Präsidentschaftswahlen
Picha: AP Photo/picture alliance

die tageszeitung

Tunaanza na gazeti la die tageszeitung juu ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Ghana. Gazeti linasema rais Nana Akufo-Addo ameshinda uchaguzi huo na hivyo ataendelea kuwa madarakani kwa muhula wa pili. Hata hivyo gazeti hilo linasema chama chake -The New Patriotic - kimepoteza viti 31 wakati chama cha mshindani wake mkuu John Mahama, National Democratic Congress kimeongeza viti 30. Die tageszeitung linatilia maanani kwamba kwa jumla uchaguzi ulifanyika vizuri licha ya matukio ya kasoro chache. Kwa mujibu wa tathmini ya Umoja wa Afrika na jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, kwa mara nyingine Ghana imeweza kuandaa uchaguzi mzuri tangu mwaka 1992.     

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaelezea wasiwasi juu ya kuongezeka kwa kiwango cha umasikini barani Afrika kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti hili linasema janga la corona limesababisha mdororo wa uchumi usiokuwa na kifani katika miaka 25 iliyopita. Kutokana na hali hiyo Frankfurter Allgemeine linasema huenda watu wengine milioni 32 wakaongezeka kwenye idadi ya watu masikini kabisa.

Gazeti hilo limeinukulu ripoti ya Umoja wa Mataifa inayosema juhudi zilizofanywa katika kupunguza umasikini, njaa na kutoa huduma za elimu zitarudi nyuma. Linasema idadi ya watu waliopoteza nafasi za ajira haijulikani kwa uhakika. Frankfurter Allgemeine linasema mgogoro wa uchumi barani Afrika unaweza kuwa mkubwa kuliko athari zilisosababishwa na janga la maambukizi ya corona ingawa linasema idadi ya watu waliokufa kutokana na maambukizi hayo ni ndogo sana kulinganisha na sehemu zingine za dunia. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba mpaka sasa ni watu 52,000 waliokufa kwenye nchi za Afrika. Idadi hiyo ndogo inatokana na hatua za haraka za karantini zilizochukuliwa na nchi hizo na pia imetokana na kuwepo kwa idadi ndogo sana ya wazee. Ni asilimia 3 tu ya waafrika ambao wamevuka umri wa miaka 65.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche linatupeleka nchini Uganda wakati ambapo watu wa nchi hiyo wanajiandaa kufanya uchaguzi. Linaeleza kuwa matumizi ya nguvu yanayofanywa na rais Yoweri Museveni yatatatiza kampeni za uchaguzi. Kampeni hizo hazitakuwa huru. Gazeti la Süddeutsche linasema video zinaonyesha jinsi mshindani mkubwa wa Museveni, mwanamuziki maarufu Bobi Wine anavyoandamwa na polisi. Gazeti linasema mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi, Uganda inapitia kipindi kibaya cha umwagikaji damu kisichokuwa na kifani katika miaka ya hivi karibuni. Bobi Wine amekamatwa mara kwa mara baada ya kutangaza nia ya kushiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi ili kupambana na rais Museveni. Hata hivyo gazeti la Süddeitsche linasema licha ya umaarufu wake Bobi Wine hana nafasi kubwa ya kushinda. Gazeti hilo limenukulu uchambuzi wa jarida la Africa Magazine unaoonyesha kwamba rais Museveni ameboresha mbinu zitakazomwezesha kushinda uchaguzi kwa mara nyingine. Njia mojawapo ni kumweka ndani Bobi Wine mara kwa mara ili kuudhoofisha msimamo wake.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neuer Zürcher linazungzumia juu ya hali ya nchini Ethiopia na linauliza kwa nini serikali kuu ya nchi hiyo inazuia misaada kupelekwa kwenye jimbo la Tigray licha ya kufikiwa mapatano na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya madhumuni hayo? Linasema serikali kuu ya Ethiopia inayoongozwa na waziri mkuu Abiy Ahmed inajaribu kuizuia jumuiya ya kimataifa kupata habari kamili juu ya kiwango cha madhara yaliyosababishwa na mashambulio ya majeshi ya serikali kuu kwenye jimbo hilo.

Kwa mujibu wa gazeti la Neuer Zürcher sababu kubwa ni ukweli kwamba waziri mkuu Abiy Ahmed alitangaza ushindi mapema mno. Gazeti hilo limemnukulu waziri, mmoja aliyekiri kwamba bado vipo vikosi vya Tigray ambavyo bado havijadhibitiwa. Wataalamu wa masuala ya kijeshi pia wamesema serikali inadhibiti sehemu fulani tu ya jimbo la Tigray.

Naam hadi hapo tunakamilisha makala haya ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani. Mimi ni mtayarishaji wako ZA kutoka hapa Bonn na hadi wiki ijayo kwaherini.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW