1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

11.06.2021 Afrika katika magazeti ya Ujerumani

11 Juni 2021

Karibu msikilizaji kwa mara nyingine katika magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika ni hapa unapoweza kuyasikia yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti mbali mbali ya ujerumani walioimulikia Afrika wiki hii.

Zentralafrikanische Republik UN Soldaten in Bangui
Picha: UN/RCA

Gazeti Frankfurter Allgemeine

Tuanze kuliangalia gazeti la Frankfurter Allgemeine linalochapishwa mjini Frankfurt ambalo limeandika kuhusu hatua ya Nigeria kuufungia mtandao wa kijamii wa Twitta nchini humo. Limeanza kwa kichwa kinachosema Hatua ya Nigeria kuipiga marufuku Twitta nchini humo inatia wasiwasi. Mhariri wa gazeti anasema hatua hiyo kali ya serikali ya Nigeria imezusha hasira na malalamiko makubwa kote lakini imepongezwa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump,je nchi nyingine za Afrika zitaelekea huko alikoelekea rais Buhari? Rais Buhari hapendi kunyamazishwa na hasa na hasa na mtandao huo wa kijamii wa Kimarekani,Twitta.

Inaonesha Twitta ndo kwanza inalifahamu hilo hivi sasa kuhusu Nigeria,nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.Mtandao huo wa Twitta hivi karibuni uliufuta ujumbe wa rais Muhammadu Buhari uliodaiwa kuwa wa vitisho. Siku mbili baadae akatangaza kuupiga marufuku mtandao huo nchi nzima.Makampuni yote ya mawasiliano yakalazimika kuuzima mtandao huo wa kijamii katika simu za mkononi nchini humo.Watumiaji wa mtandao huo wasiotaka kufuata maagizo ya marufuku hiyo wanahofia kuchukuliwa hatua.Lakini kama haitoshi serikali ya Nigeria imeongeza makali kwenye marufuku ya mtandao huo na kuyataka pia mashirika ya habari,televisheni na magazeti kutoutumia tena mtandao huo katika shughuli zao za kikazi za  kutoa na kupata habari.Vinginevyo wataangaliwa kama sio wazalendo.

Na kama ilivyotarajiwa hatua hiyo ilikutana na wimbi la hasira ambapo wanigeria wanaoishi nje wakaanzisha harakati za kutaka marufuku dhidi ya Twitta iondolewe Nigeria.Upinzani umekiita kitendo cha serikali ni unyanyasaji na ukatili wa kutaka kuwanyamazisha wanigeria na watuamiaji wa mtandao huo wameitisha maandamano makubwa tarehe 12 yaani Jumamosi hii.Ingawa kiroja ni kile cha rais wa zamani wa Marekani aliyejitokeza kumuunga mkono rais Mohammadu Buhari katika hatua yake hiyo ya kuizima Twitta nchini mwake.Trump ametowa pongezi akisema Nigeria imefanya vizuri sana kuifungia Twitta kwasababu mtandao huo umemfungia pia rais Buhari.Na hata nchi nyingine zinapaswa kuzifungia Twitta na Facebook kwasababu hazitaki watu wazungumze kwa uhuru na uwazi.Muhariri wa Frankfurter allgemeine anasema kwa kilichotokea Nigeria,yale yanayoelezwa na makampuni kwamba hayawezi kufanya kazi bila kuingiliwa nchini Nigeria,yanathibitishwa.

Gazeti Die Zeitung

Gazeti la Die Zeitung limetuwama huko Afrika ya Kati na kuandika hasa kuhusu namna Urusi ilivyoanzisha kile kinachoangaliwa kama ni mfumo maalum kiusalama. Mhariri anasema Urusi inatumia ukatili kuilinda serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mhariri wa Die Zeitung anaendelea kuandika kwamba hatua iliyochukuliwa na ufansa na kusimamisha msaada wake wa kifedha wa shughuli za kijeshi nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ni ndogo lakini inatoa ujumbe mkubwa.Hakuna mwanajeshi yoyote wa kutoa mafunzo aliyeko kwenye wizara ya ulinzi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mjini Bangui,hilo limethibitishwa na Ufaransa.Shughuli za mafunzo ya kijeshi zinazoendeshwa na Ufaransa zimesimamishwa na msaada wa  bajeti ya yuro milioni 10 nao umefutwa.Mhariri anasema hayo kwakweli ni mabadiliko.

Hadi katikati ya miaka ya 90 Uaransa imekuwa ikiendesha vita dhidi ya Libya na Rwanda kutokea Bangui ikiwa na kambi yake kubwa ya kijeshi.Lakini nchi hiyo ikaondoka na kuhamia Chad na kuelekeza nguvu zake katika mapambano dhidi ya makundi ya itikadi kali katika eneo la Sahel wakati Jamhuri hiyo ya Afrika ya Kati ilipotumbukia kwenye vita vya wenyewekwa wenyewe na kushindwa kusimamia uthabiti wake. Leo hii hakuna tena wanajeshi wa Ufaransa sio katika mji wa Bouar wala Bangui,waliotapakaa ni wanajeshi wa Urusi.Inakadiriwa,kuna mamia kama sio maelfu ya washauri wa kijeshi na wanajeshi wa  vikosi maalum kutoka Urusi katika nchi hiyo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.Hivi sasa mshauri mkuu wa masuala ya usalama wa  rais Toudera ni aliyekuwa afisa wa ujasusi wa jeshini wa Urusi Valeri Zakharov.

Vyombo vya habari katika Jamhuri ya Afrika ya Kati vinaripoti kwamba wanajeshi wakigeni wanapiga risasi na kuwala nguruwe wa wakulima,wanabaka wasichana na kuharibu vijiji vya watu chungunzima. Urusi inasema hizo ni matunda ya ndoto zinazosimuliwa na wendawazimu,ingawa Umoja wa Mataifa na maafisa wa nchi hiyo wameanzisha uchunguzi. Mhariri wa gazeti hili anakumbusha kwamba wanajeshi wa Urusi wanatajwa kuwa zaidi katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya kati ambako ndiko kwenye migodi ya dhahabu,wamekuwa wakiendesha harakati zao huko tangu muungano mpya wa waasi ulipoanzisha mapambano yao Desemba mwaka 2020.

Die Zeitung kuhusu Zambia

Gazeti la Die Zeitung pia limeandika kuhusu Zambia na mhariri anagusia hali ya mchezo wa paka na panya iliyopo kufuatia kile kinachoonekana kukosekana uongozi  unaotambuliwa kisiasa nchini humo. Mhariri anasema Tangu  kupigwa marufuku shughuli za kampeini za uchaguzi kutokana na  janga la virusi vya Corona,mazingira ya kisiasa nchini Zambia yanaonesha kuwepo joto kali.

Kwanza ni jaribio la mauaji linalodaiwa kufanywa na polisi dhidi ya kiongozi wa upinzani nchini humo.Wanaharakati kadhaa wameishia kujikuta hospitali kutokana na vurugu kubwa zilizoshuhudiwa nchini humo,nchi ambao kwahakika ni moja ya zile nchi zenye utulivu mkubwa barani Afrika.Hivi sasa imejikuta imeingia kwenye vurugu wakati umebakia muda mfupi iingie kwenye uchaguzi Agosti 12.Kilichochochea vurugu hizo ni kitendo cha rais Edgar Lungu cha kupiga marufuku Kampeini za uchaguzi kisa na maana ni janga la virusi vya Corona.

Rais Lungu nae pia anawania kuchaguliwa tena madarakani kupitia chama chake cha Patriotic Front-PF.Kiongozi wa Upinzani Hakainde Hichilema anasema anachokifanya Lungu ni mchezo wa paka na panya,anadai anajaribu kuuzuia upinzani usikusanyike na wananchi kwa sababu anajua kishindo chake.Wapinzani wanadai chama cha PF na rais Lungu mara hii hawana ubavu wa kushinda uchaguzi.

Neue Zürcher Zeitung

Na mwisho ni gazeti la  Neue Zürcher Zeitung lililoandika juu ya kifo cha kiongozi wa kundi la itikadi kali la Nigeria,Boko Haram Abubakar Shekau.Mhariri huyo amegusia kwamba Abubakar Shekau ameuwawa,lakini pia amekumbusha kwamba sio mara ya kwanza kiongozi huyu kutangazwa kwamba amekufa tangu alipotwaa uongozi wa kundi hilo mwaka 2009. Ameshatangazwa amekufa mara chungunzima na baade kujitokeza kukanusha kifo chake.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW