1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu
8 Oktoba 2021

Kati ya masuala ya Afrika yaliyoangaziwa na magazeti ya Ujerumani wiki hii, ni pamoja na uhali ya kisiasa Sudan, na mvutano wa Ujerumani na Namibia juu ya fidia na madhara yaliyosababishwa na Ujerumani enzi za ukoloni

Sudan Port Sudan | Hafenblockade
Picha: Ibrahim Ishaq/AFP/Getty Images

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland liliandika kuhusu uhaba wa chakula unaoinyemelea Sudan huku maandamano yakisababisha kufungwa kwa bandari kubwa zaidi nchini humo.

Gazeti hilo limeandika, mwaka mmoja na nusu uliopita, hata baada ya kupinduliwa kwa aliyekuwa mtawala wa muda mrefu nchini humo Omar Al Bashir taifa hilo halina utulivu.  Makundi ya kikabila, waasi na baraza la mpito wanawania kupata ushawishi na madaraka. Kwa wiki kadhaa sasa, watu wa kabila la Beja ambao ni moja ya makabila makubwa zaidi nchini humo, wamekuwa wakizuia  watu wasifike katika bandari kubwa zaidi nchini humo katika pwani ya bahari ya shamu wakitumia mawe na vizuizi vingine.

Serikali ya Sudan sasa imeonya kuwa nchi hiyo muda si mrefu, itakabiliwa na uhaba wa dawa, mafuta na ngano kutokana na vizuizi hivyo. Katika kauli ya serikali ya hivi karibuni, baraza la mawaziri la Sudan lilitambua madai waliyoyaita ‘halali ya watu wa kabila la Beja na kusisitiza haki yao ya maandamano ya amani. Hata hivyo serikali hiyo imeonya kuwa kuzuia bandari na barabara zinazounganisha ukanda huo na nchi nzima kunaathiri maslahi ya raia wote wa Sudan. 

Frankfuter Allgemeine

Frankfuter Allgemeine limeandika kuhusu makosa yaliyofanywa na Ujerumani enzi za ukoloni na madhara yake kwa Namibia bila kusahau mvutano juu ya fidia ambayo Ujerumani inapaswa kuilipa Namiba. Limeandika, mauaji ya halaiki ya enzi za ukoloni dhidi ya Wanama na Waherero yameacha kovu hadi leoi. Wazawa wengi hawataki kukubali mazungumzo ya usuluhishi na fidia yaliyopendekezwa na Ujerumani.

Gazeti hilo linaendelea kueleza kuwa, bunge la Namibia limekuwa na mjadala mkali kuhusu mkataba wa usuluhishi juu ya ukatili uliotokea kipindi cha vita ya Waherero mnamo mwaka 1904 hadi 1908. Baadhi ya wabunge wamekosoa mpango wa fidia wa zaidi ya euro bilioni 1. wa Ujerumani kwa mauaji hayo ya halaiki ya jamii ya Herero na Nama

Neu Zücher

Gatezi la Neu Zücher limeandika kuhusu hatua ya Somalia kuanza kuangalia upya sinema katika jumba la taifa la sinema ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30. Gazeti hilo limeandika, kufunguliwa tena kwa ukumbi huo wa sinema wa taifa nchini humo sasa kunarejesha maisha ya utamaduni.

Kwa miongo mitatu, hakuna hata filamu moja iliyowahi kuoneshwa hadi wiki iliyopita. Jumatano jioni, jumba hilo la sinema lilifurika watu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1991. Uwepo wa ulinzi mkali na vikosi vya usalama ndani na mbele ya jengo hilo kulikumbusha kwamba, vita ya wenyewe kwa wenyewe bado inafukuta katika sehemu kubwa ya Somalia.

Jumba hili la sinema, ambalo kimsingi ni zawadi kutoka kwa rais wa zamani wa Jamhuri ya watu wa China Mao Zedong, lilifunguliwa mwaka 1967 na kuwa sehemu ya simulizi za utamaduni Somalia. Nchi hiyo ilipotumbukiw kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1991, jengo hilo liliharibiwa na kulazimika kufungwa ambapo lilitumiwa na wababe wa vita kama ngome na sehemu ya kuhifadhi silaha. Ukumbi huo ulifunguliwa tena mwaka 2012 lakini wiki mbili baadaye ulilipuliwa na wanamgambo wenye itikadi kali wa al-Shabab ambapo lilifungwa tena kwa miaka mingine  tisa.

Blätter für deutsche und internationale Politik

Jarida la siasa za Ujerumani na za kimataifa, ''Blätter für deutsche und internationale Politik,'' limeandika kuhusu kukosekana kwa usawa katika kukabiliana na majanga kunavyoliathiri bara la Afrika. Limeandika, mwanzoni mwa janga la COVID 19, wakuu wa mataifa na serikali katika serikali za nchi zilizoendelea waliapa kuonesha mshikamano katika kupambana na janga la virusi vya corona. Lakini leo hilo halipo tena.

Juni 2021, mpango wa Umoja wa Mataifa wa ugawaji chanjo wa COVAX ambao lengo lake ilikuwa kutoa chanjo dhidi ya covid 10 kwa usawa duniani, ulipeleka dozi 530,000 nchini Uingereza, kati ya nchi tajiri zinazozalisha chanjo zake yenyewe na wakati chanjo hizo zilipopelekwa,  nusu ya waingereza milioni 66.6, walishachanjwa kwa mara ya pili. Afrika kwa upande mwingine, bara lenye nchi 55 na zaidi ya wakaazi bilioni 1.2 ambao hadi mwezi huo wa Juni chini ya asilimia 2 walikuwa wamechanjwa dhidi ya Covid 19 na halikupokea hata nusu ya dozi hizo.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW