Afrika katika magazeti ya Ujerumani
17 Desemba 2021Frankfurter Allgemeine
Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika makala juu ya rais wa hapo awali wa Afrika Kusini Jacob Zuma. Mahakama imeamuru Zuma arudi kifungoni jela kwa sababu imesema sababu iliyotolewa hapo awali kwamba anahitaji kuwa nje kwa ajili ya matibabu haina mashiko kisheria. Hata hivyo wakfu wake umesema utakata rufani.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba hapo awali Jacob Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela kwa kosa la kuidharau mahakama, lakini aliachiwa kutokana na hali mbaya ya afya baada ya miezi miwili.
Gazeti linaelezea wasiwasi kwamba huenda wafuasi wake wakafanya ghasia kupinga uamuzi huo wa kumpeleka Zuma jela. Linakumbusha ghasia walizofanya wafuasi hao mnamo mwezi wa Julai na kusababisha vifo vya watu 300 na hasara kubwa kutokana na maduka kuporwa.
Der Tagesspiegel
Gazeti la Der Tagesspiegel linatueleza jinsi mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa ulivyobadilika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Linasema mji wa Addis Ababa tayari umo vitani. Wakaazi wa mji huo wanafanya kazi ya kuulinda dhidi ya wanaowaita magaidi. Gazeti hilo linaeleza kwamba tangu mwezi uliopita makundi ya watu wa mji huo wanawasaka magaidi hao na wanawatambua kutokana na majina yao.
Yeyote mwenye jina lenye nasaba ya jimbo la Tigray anatuhumiwa kuwa gaidi. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza mwezi Novemba mwaka uliopita nchini Ethiopia. Waasi wa jimbo la Tigray wanapambana na majeshi ya serikali kuu tangu wakati huo. Gazeti linafahamisha kuwa maalfu ya watu wameshakufa na zaidi ya milioni mbili wamegeuka kuwa wakimbizi kutokana na vita hivyo.
Der Tagesspiegel linasema serikali ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed inatumia mkakati wa kuzuia mahitaji muhimu kuwafikia watu wa jimbo la Tigray na sasa kuna hatari kubwa ya watu wa sehemu hiyo kufa njaa. Gazeti limekariri taarifa ya mashirika ya Umoja wa Mataifa inayosema watu zaidi laki nne tayari wanakabiliwa na baa la njaa katika jimbo hilo. Gazeti hilo linasema serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed inawalaumu watu na mashirika ya nje kwa kukoleza moto wa vita nchini mwake na hasa mashirika ya habari ya Marekani na Uingereza.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung linasema watawala wa kijeshi nchini Mali sasa wanakabiliwa na mtihani mgumu. Ikiwa hawatarejesha demokrasia nchini, hadi mwezi Februari mwaka ujao Mali itakuwamo katika hatari ya kutengwa. Gazeti linasema watawala wa kijeshi wanapaswa kuitisha uchaguzi mnamo mwezi huo la sivyo jumuiya ya maendeleo ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS itawawekea vikwazo wanajeshi hao.
Kiongozi wa utawala wa kijeshi Assimi Goita ameahidi kuwasilisha ratiba ya uchaguzi mwezi Januari mwaka ujao. Gazeti la die tageszeitung linasema kiongozi huyo wa wanajeshi atakabiliwa na matatizo kutokana na muda mfupi wa matayarisho. Linasema uhafifu wa miundombinu, ugavi na usafirishaji nchini Mali, zitakuwa changamoto. Licha ya ahadi hiyo, gazeti linatilia mashaka iwapo mwanajeshi huyo Assimi Goita atakuwa tayari kuachia madaraka. Hata hivyo linatilia maanani kwamba mkutano wa kitaifa wa kutayarisha uchaguzi utafanyika mnamo wiki mbili zijazo nchini Mali.
Neue Zürcher Zeitung
Gazeti la Neue Zürcher linatupasha habari juu ya mkasa wa akina mama watano waliozaliwa kutokana na mahusiano ya mama zao waafrika na wanaume wa kizungu katika enzi za ukoloni wa wabelgiji nchini Kongo mahusiano yaliyokuwa yamepigwa marufuku! Gazeti linaeleza kuwa wakoloni waliamini mahusiano kama hayo yalikuwa hatari kwa mfumo wao wa ukoloni na ndiyo sababu wazazi walipokonywa watoto hao na kupelekwa kwenye nyumba za malezi za kanisa Katoliki. Mama zao walilazmishwa kutia saini hati zilizokuwa zimeandikwa katika lugha ambayo hawakuijua kukubali kuchukuliwa kwa mabinti zao. Watoto hao waliambiwa kuwa mama yao alikuwa malkia na baba yao ni serikali ya Ubelgiji.
Gazeti la Neue Zürcher linasema baada ya miaka mingi ya kunyamaza kimya wanawake hao wameishtaki serikali ya Ubelgiji kwa maovu waliotendewa. Hata hivyo mashtaka yao yametupiliwa mbali katika raundi ya kwanza. Mahakama ya Ubelgiji imeyatupilia mbali mashtaka hayo ya uhalifu dhidi ya ubinadamu. Mahakama imesema katika uamuzi wake kwamba kuchukuliwa kwa nguvu kwa watoto hao kutoka kwa wazazi haukuwa uhalifu wakati wa ukoloni.
Vyanzo: Deutsche Zeitungen