1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
7 Januari 2022

Miongoni mwa yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni matukio ya nchini Mali na gazeti la Weser Kurier linauliza iwapo demokrasia itapewa nafasi nchini Sudan? pamoja na mengineyo.

Mali | Übergangspräsident Oberst Assimi GOÏTA
Picha: Präsidentschaft von Mali

die tageszeitung

Makala ya gazeti la die tageszeitung juu ya matukio ya nchini Mali. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba watawala wa kijeshi nchini humo wameamua kuahirisha uchaguzi kwa muda wa miaka mitano! Utawala wa wanajeshi hao uliandika barua kwa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS kueleza hayo. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na jumuiya ya kimataifa uchaguzi huo ulikusudiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao. Gazeti la die tageszeitung linakumbusha kwamba wanajeshi nchini Mali walitwaa mamlaka kwa kuiangusha serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia mnamo mwezi wa Agosti mwaka 2020.

Gazeti linaeleza kuwa Kiongozi wa wanajeshi hao Kanali Goita Assimi alitoa ahadi ya kurejesha demokrasia hadi mwezi Februari mwaka huu. Kwa ahadi hiyo aliweza kuhakikisha uwepo wa wanajeshi wa kimataifa ikiwa pamoja na wa kutoka Ujerumani. Wanajeshi hao wa kimataifa walimsaidia Kanali Assimi kupambana na magaidi wanaoishambulia Mali mara kwa mara. Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba ikiwa uchaguzi hautafanyika uwepo wa wanajeshi hao wa kimataifa nchini Mali utakuwamo mashakani.

Weser-Kurier

Gazeti la Weser-Kurier linauliza iwapo demokrasia itapewa nafasi nchini Sudan? Linasema yalitokea yalitarajiwa nchini humo. Waziri mkuu Abdullah  Hamdok alierejeshwa madarakani baada ya  kuangushwa na wanajeshi sasa ameamua mwenyewe kujiweka pembeni. Gazeti linasema wote walisimama dhidi yake.

Gazeti la Weser-Kurier linasema wanajeshi nchini Sudan wanataka kushika hatamu za uongozi na walikusudia kumtumia waziri mkuu Hamdok kama kibaraka wao lakini wananchi walirejea tena  mabarabarani kumpinga kwa sababu alifikia mapatano na wanajeshi.

Baada ya Hamdok kujing‘atua hali sasa ni ya kutatanisha nchini Sudan linasema gazeti la Weser-Kurier. Linauliza jee watetea demokrasia watapata  fursa nyingine ya kuirudisha Sudan kwenye demokrasia? Gazeti hilo linahofia huenda wanajeshi wakaendeleza mipango yao.

Kwa sasa hakuna uwezekano wa kufikia mwafaka nchini Sudan linasema gazeti hilo na ndiyo sababu kujiuzulu kwa waziri Mkuu Abdallah Hamdok kunawahusu watu wa pande zote pia Ujerumani. Gazeti linasema pana haja ya kuchukua hatua thabiti ili kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher linasema katika makala yake kwamba uchunguzi juu ya ufisadi uliofanywa nchini Afrika Kusini wakati wa utawala wa rais Jacob Zuma unakilemea pia chama tawala cha nchi hiyo African National Conngress ANC. Linasema kiwango cha ufisadi wakati wa utawala wa Zuma kilikithiri. Rais Cyril Ramaphosa alikabibidhiwa hati ya uchunguzi huo mapema wiki hii baada ya kazi ya miaka mitatu.

Gazeti la Neue Zürcher linafahamisha kwamba Zuma  na wapambe wake waliiteka nchi na kuweza kuiba mabilioni. Gazeti hilo linastaajabu kwamba chama tawala ANC hakikuwa na habari juu ya ufisadi huo! Hata hivyo uchunguzi uliofanywa unakilemea chama  hicho pia, linasema gazeti la Neue Zürcher. Chama hicho kilipewa michango mikubwa mikubwa ya fedha na baadhi ya wanachama waliokuwa na mahusiano ya karibu na wakubwa walijipatia tenda nono nono.

Hata hivyo gazeti linatilia maanani kwamba uchunguzi huo hautakuwa na uzito wa kisheria kama ilivyobainika kwamba hata baada ya miaka minne ya Zuma kuondolewa madarakani hakuna kiongozi yeyote mwenye uzito wa chama cha ANC aliyefunguliwa mashtaka mpaka sasa kwa makosa ya ufisadi.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linauangalia uhusiano baina ya Ujerumani na Morocco na linasema waziri mpya wa  mambo ya nje wa Ujerumani amepiga hatua ambayo haikuwahi kufikiwa na waziri wa hapo awali. Gazeti linasema serikali mpya ya Ujerumani imepata mafanikio yake ya kwanza katika sera za nje. Serikali hiyo imerejesha uhusiano na Morocco. Na linasema nchi hiyo ni muhimu kwa Ujerumani katika masuala ya uhamiaji na nishati.

Gazeti la Die Welt linatujulisha kwamba Morocco na Ujerumani zinaweza kupeana mambo mengi. Pamoja na bidhaa za kilimo Morocco pia inauza biadhaa za viwanda nchini Ujerumani. Gazeti linasema Morocco ni mshirika mkubwa wa Ujerumani katika nishati ya maji. Gazeti la Die Welt linatilia maanani kwamba siku chache tu baada ya serikali mpya ya Ujerumani kuingia madarakani iliweza kurekebisha uhusiano na nchi hiyo ya Afrika Kaskazini. Kwa mara ya kwanza Ujerumani inakubaliana na mpango wa Morocco juu ya sehemu ya Sahara Magharibi lakini bila ya kuzingatia dhima ya Umoja wa Mataifa juu ya mgogoro huo.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW