1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
21 Januari 2022

Mvutano kuhusu ugavi wa chanjo duniani, Rais wa Cameroon Paul Biya ayatumia mashindano ya kugombea ubingwa bara ni Afrika kwa shabaha za propaganda ni matukio ya Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani wiki hii.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa
Picha: SHELLEY CHRISTIANS/REUTERS

Die Welt

Gazeti la Die Welt juu ya mvutano unatokana na ugavi wa chanjo duniani. Gazeti linakumbusha kwamba mpaka sasa bara la Afrika bado linategemea hisani ya mataifa tajiri ili kupatiwa makombo ya chanjo. Gazeti linasema Afrika Kusini inataka kuondokana na hali hiyo. Imesema haitaki tena kuwa omba omba wa chanjo kutoka kwa mataifa tajiri. Kwa ajili hiyo gazeti la Die Welt linaeleza amejitokeza mwananchi wa Afrika Kusini ambaye pia ni raia wa Marekani anayetaka kuanzisha kiwanda cha kutengeneza chanjo dhidi ya maambukizi  ya virusi vya corona.

Mjasiriamali huyo Patrick Soon-Shiong ametajirika nchini Marekani kutokana na kuuza dawa za kutibu saratani. Gazeti la Die Welt linasema daktari huyo mwenye asili ya kichina mapema wiki hii alifungua maabara pamoja na kiwanda cha kutengeneza chanjo nchini Afrika Kusini ambazo pia zitauzwa nje ya bara hilo. Gazeti la Die Welt linasema limelikariri jarida la Bloomberg linalokadiria utajiri wa mjasiriamali huyo Soon-Shiong kufikia dola bilioni 11.

Gazeti hilo linasema mfanyabiashara huyo ambaye pia ni daktari amekubali kutoa Euro milioni 170 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Die Welt linaarifu kwamba chanjo zitaanza kutengezwa katika muda wa mwaka mmoja. Watu zaidi ya 400 watapatiwa ajira kwenye kiwanda hicho kinachoitwa NantSA. Gazeti la Die Welt linatilia maanani kwamba mpaka sasa watu waliopatiwa chanjo barani Afrika hawatimii hata asilimia 10.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatueleza zaidi juu ya mjasiriamali huyo Patrick Soon-Shiong. Linatueleza kuwa alimaliza masomo ya udaktari kwenye chuo kikuu cha Witwatersrand nchini Afrika Kusini alipokuwa na umri wa 23 na ingawa alikuwa miongoni mwa madaktari hodari alihitaji kibali maalumu kwa ajili ya kazi yake. Sababu ni kwamba kama Mchina hakuhesabika kuwa mweupe chini ya utawala wa makaburu. Gazeti hilo linatujulisha kwamba alilipwa nusu ya mishahara ya madaktari weupe. Patrick Soon- Shiong alienda Marekani mnamo miaka ya 70 ambapo aliendelea na masomo na kuanza shughuli za kibiashara.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya mashindano ya kandanda ya kugombea ubingwa wa  bara la Afrika yanayoendelea nchini Cameroon. Gazeti hilo linasema rais wa nchi hiyo Paul Biya anayatumia mashindano hayo kwa shabaha za propaganda. Biya mwenye umri wa miaka 88 amekuwa rais nchini Cameroon tangu mwaka 1982. Gazeti la Neue Zürcher linasema ushindi wa Cameroon walipocheza na Burkina Faso uliisuuza roho ya rais Biya. Cameroon iliilaza Burkina Faso mabao mawili kwa moja. Gazeti linasema mambo yalikuwa mazuri kwa propaganda za rais Paul Biya.

Katika hotuba ya mwaka mpya rais Biya alisema kombe la Afrika ni wasaa wa kuonyesha undugu mkubwa wa waafrika. Amesema mashindano hayo yataipa Cameroon fursa ya kuonyesha nyanja mbambali za utamaduni wake. Hata hivyo gazeti la Neue Zürcher linasema tatizo ni kwamba kinachoonekana juu ya Cameroon ni kuzidi kugawika.

Linakumbusha juu ya mgogoro baina ya maeneo yanayotumia lugha ya kiingereza na yale yanayotumia lugha ya kifaransa. Gazeti hilo pia linakumbusha kwamba upande wa magharibi wa Cameroon unataka kuwa sehemu huru ya watu wanaotumia lugha ya kiingereza. Gazeti la Neue Zürcher linatilia maanani kwamba mashindano ya kombe la ubingwa wa Afrika yanaendelea katika muktadha wa hatari ya mashambulio ya kigaidi.

Süddeutsche

Jee kimetokea nini?. Hilo ni swali linaloulizwa na gazeti la Süddeutsche. Ndege ya kijeshi ya Ujerumani ilinyimwa ruhusa ya kupita kwenye anga ya Mali. Gazeti hilo linasema hatua hiyo ya utawala wa kijeshi nchini Mali imeathiri shughuli za wanajeshi wa Ujerumani wanaolinda amani nchini humo. Gazeti linaeleza kuwa Ujerumani inahisi kuwa inakabiliwa na matatizo ya aina mpya nchini Mali katika utekelezaji wa majukumu ya askari wake 1300 ambao ni sehemu ya jeshi la Umoja wa Mataifa linalolinda amani nchini Mali. Gazeti la Süddetsche linaeleza kwamba Mali kwa sasa inapambana na magaidi na katika mapambano hayo utawala wa kijeshi wa nchi hiyo unapoendelea kushirikiana zaidi na mamluki wa Urusi.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW