1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
18 Machi 2022

Magazeti ya Ujerumani yamezingatia juu ya mshikemshike wa kisiasa wakati zimebakia wiki chache kufanyika uchaguzi mkuu nchini Kenya. Hali ya nchini Ethiopia. Mtazamo wa nchi za Afrika juu ya vita vya nchini Ukraine.

Kenia Nairobi 2021 | Uhuru Kenyatta, Präsident
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung ambalo limeandika juu ya mshikemshike wa kisiasa wakati zimebakia wiki chache kufanyika uchaguzi mkuu nchini Kenya. Gazeti hilo linazungumzia juu ya mfungamano wa kihistoria ulioundwa kwa ajili ya kuleta maridhiano nchini Kenya. Linatufahamisha kwamba rais Uhuru Kenyatta anampigia debe Raila Odinga aliyekuwa hasimu wake mkubwa hapo awali. Gazeti la die tageszeitung linasema rais Kenyatta ameamua kumuunga mkono Raila Odinga katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mnamo mwezi Agosti. Die tageszeitung linafahamisha kwamba bwana Odinga, kiongozi wa upinzani mwenye umri wa miaka 77 amechaguliwa kuwa mgombea wa kiti cha urais kwa niaba ya mfungamano unaoitwa Azimio la Umoja wa vyama vya ODM na Jubilee na pande nyingine za kisiasa jumla ya 24 zinazowakilisha asilimia 70 ya wapiga kura nchini Kenya.

Gazeti la die tageszeitung linasema hatua hiyo inawakilisha mabadiliko ya kihistoria katika nchi hiyo ya Afrika mashariki. Linasema ikiwa atachaguliwa kuwa rais, atakuwa mjaluo wa kwanza kushika wadhifa huo. Hata hivyo gazeti linatilia maanani kwamba Odinga atakabiliwa na ushindani wa William Ruto ambaye mapaka sasa ni naibu rais. Die tageszeitung linasema baadhi ya wadadisi wanahofia kwamba akichaguliwa kuwa rais, Odinga hatazifuatilia juhudi za kupambana na ufisadi uliofanyika katika enzi za Kenyatta.

Neue Zürcher 

Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya hali ya nchini Ethiopia. Linasema wakati waziri mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed anaiambia dunia kwamba vita vimekwisha nchini humo watu kwenye jimbo la kaskazini wanasema bado wanaendelea kuuliwa. Gazeti la Neue Zürcher limekariri habari juu ya kuendelea kwa mapigano kwenye jimbo la kaskazini la Afar. Gazeti hilo linasema tangu mwishoni mwa mwezi Januari jimbo hilo la kaskazini limekuwa linashambuliwa na wapiganaji wa jeshi linaloitwa la ukombozi wa Tigray, TPLF.

Gazeti la Neue Zürcher limeikariri taarifa ya serikali ya jimbo inayosema kuwa watu zaidi ya laki tatu wa jimbo hilo wametimuliwa kutoka kwenye maakazi yao au wamekuwa wakimbizi wa ndani. Neue Zürcher linasema majeshi ya Tigray yanajaribu kendeleza mapigano kwenye jimbo la Afar ili kuweza kupata nguvu ya kufanyia mazungumzo na serikali kuu ya Ethiopia. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba jimbo hilo lina utajiri wa madini. Linasema haidhuru wapi mapigano yanatokea, jambo moja ni wazi, nalo ni kwamba wananchi wanaathirika kwa namna mbalimbali. 

Frankfurter Allgemeine

Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine linauzungumzia mtazamo wa nchi za Afrika juu ya vita vya nchini Ukraine. Gazeti hil linasema uhusiano baina ya Urusi na nchi za Afrika umekuwa mgumu tangu Urusi ifanye uvamizi nchini Ukraine. Gazeti hilo linatoa mfano wa hotuba ya balozi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa aliyeitaka Urusi ikubali mipaka iliyopo kama vile nchi za Afrika zilivyoikubali mipaka iliyowekwa na wakoloni. Frankfurter Allgemeine linasema nchi tatu za Afrika zimelaani uvamizi huo. Umoja wa Afrika pia unataka vita visimamishwe mara moja. Na kwenye baraza la Usalama kati ya nchi 54 za Afrika 28 ziliunga  mkono azimio la kuitaka Urusi iondoe majeshi yake mara moja. Nchi 17 za Afrika hazikupiga kura.

Gazeti la FrankfurterAllgemeine linakumbusha juu ya kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa Afrika  zinazoonyesha hisia za enzi za ukoloni wakati ambapo Umoja wa kisoviet uliviunga mkono vyama vya  ukombozi. Gazeti linasema licha ya uhusiano kuanza kupaliliwa baina ya Urusi na Afrika tangu kufanyika  mkutano wa mjini Sotchi lakini malengo yaliyokusudiwa bado hayajafikiwa. 

Die Welt

Gazeti la Die Welt linatupa mchapo juu ya mvutano kati ya wanasiasa na viwanda vya sigara nchini Lesotho. Gazeti hilo linaeleza kuwa uuzaji wa sigara ni biashara inayostawi nchini humo kutokana na idadi ya wavutaji kuongezeka. Gazeti la Die Welt linasema licha ya madhara yanayosababishwa na uvutaji sigara, serikali ya Lesotho inahitaji fedha ili kurekebisha bajeti ya nchi hasa baada ya kupitia janga la maambukizi ya virusi vya corona. Na kwa hivyo serikali ya Lesotho iliamua kupandisha kodi ya tuambaku. Hata hivyo gazeti linasema haikuwa rahisi kwa serikali kufikia lengo lake kamili. Badala ya kutoza asilimia 30 serikali ilipunguza kodi hiyo kwa asilimia 6.

Gazeti la Die Welt linasema hali hiyo imetokana na nguvu ya wenye viwanda vya sigara walioendesha kampeni ili kuzuia kodi ya tumbaku kupanda juu sana nchini Lesotho. Wawakilishi wa viwanda vya sigara nchini Lesotho walilazimisha kufanyika mikutano na viongozi wa serikali juu ya kodi hiyo. Gazeti la Die Welt linasema watu hao, wapiga debe kwa niaba ya viwanda vya tumbaku walifanikiwa katika lengo lao.

Gazeti linasema yaliyotokea Lesotho si mapya barani Afrika inapohusu viwanda vya tumbaku. Kampuni  maarufu ya tumbaku British American Tobacco pia iliwahonga wahusika nchini Kenya. Gazeti la Die Welt linakumbusha kwamba shirika la utangazaji la Uingereza BBC lilitangaza ushahidi wa mfanyakazi mmoja wa BAT, Paul Hopkins juu ya ufisadi uliokuwa unafanywa na kampuni hiyo ya sigara nchini Kenya.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW