1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Josephat Charo
12 Agosti 2022

Uchaguzi wa Kenya, ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken na mtihani unaolikabili shirikisho la soka barani Afrijka CAF, ni miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Kenia Wahlen 2022
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Uchaguzi mkuu wa Kenya ulihanikiza katika magazeti ya Ujerumani huku wahariri wakifuatilia kwa karibu matukio yaliyokuwa yakiendelea nchini humo. Gazeti la Neues Deutschland lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema "Kenya ina matumaini ya mkondo wa amani". Mhariri wa gazeti hilo Katrin Voss alisema mnyukano mkali ulioshuhudiwa baina ya wagombea nafasi ya urais naibu wa rais William Ruto na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga umeleta kumbukumbu mbaya ya machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007. Hata hivyo matumaini ni makubwa kwamba amani itatawala hata baada ya mshindi kutangazwa.

Nalo gazeti la Tageszeitung kuhusu uchaguzi wa Kenya liliandika kuhusu kupanda kwa joto la kisiasa na uwezekano wa Odinga kuibuka mshindi kwa kuwa aliungwa mkono na rais Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa hasimu wake wa kisiasa kwa muda mrefu lakini baadaye wakaelewana na kushirikiana kwa karibu. Hata hivyo mhariri alisema hakukuwa na uhakikika kamili kwamba usuhuba kati ya viongozi hao wawili ungemhakikishia ushindi Odinga baada ya miongo zaidi ya mitano ya uhasama wa kurithi.

Ziara ya Blinken Afrika

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilizungumzia ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken barani Afrika. Mhariri alisema nusu ya ziara ya Blinken ilihusu Urusi, huku waziri mwenyewe akisisitiza kwamba ziara yake hiyo haikuhusu eneo lolote lengine lile. Katika mahojiano na kituo cha televisheni ya Afrika Kusini Enca siku ya Jumatatu, siku ya pili ya ziara yake katika nchi tatu za Afrika, zikiwemo Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda, Blinken alisisitiza ziara hiyo ililihusu tu bara la Afrika. Hata hivyo fikra za umma zilikuwa tofauti, huku baadhi wa wafuatiliaji wakiiona ziara hiyo kama iliyolenga kuukabili ushawishi wa Urusi na China katika Afrika ambao Marekani inataka kuupunguza na kuudhibiti.

Mojawapo ya hoja nzito katika ziara ya Blinken Afrika Kusini ni kukataa kwa nchi hiyo kuikosoa Urusi kuhusiana na vita nchini Ukraine. Kabla ya ziara hiyo mawaziri kadhaa walielezea wasiwasi wao kwamba Marekani ingeishinikiza serikali, lakini Afrika Kusini haikuonekana ikibanduka kutoka kwa msimamo wake kuhusu suala la Ukraine. Mhariri alikumbusha juu ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov katika mataifa kadhaa ya Afrika yakiwemo Jamhuri ya Congo, Uganda na Ethiopia ambapo alifanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu kisiasa na kuimarisha hadhi ya Urusi katika mataifa hayo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema mkakati mpya wa Marekani katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara unafichua masilahi mengine.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken, kushoto, na rais wa Rwanda, Paul KagamePicha: Andrew Harnik/AFP/Getty Images

Nalo gazeti la Neue Zürcher kuhusu ziara ya Blinkenlilisema Marekani haitaki kuliacha bara la Afrika peke yake kwa mahasimu wake. Waziri wa mambo ya nje ya wa Marekani Anthony Blinken aliuwasilisha mkakati wa Marekani kwa ajili ya bara la Afrika nchini Afrika Kusini katika ujumbe alioutoa katika chuo kikuu cha Pretoria. Katika ujumbe wake Blinken alisema Marekani inazitazama nchi za Kiafrika kama washirika na wanataka kufanya kazi pamoja kwa usawa.

Rais wa Senegal Macky Sall akabiliwa na mtihani

Suala lengine lililowashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani ni shinikizo linalomkabili rais wa Senegal Macky Sall. Gazeti la Neues Deutschland lilisema rais Sall amepoteza uungwaji mkono wa muungano unaotawala na analazimika kutafuta washirika watakaomuunga mkono baada ya kupoteza vibaya katika uchaguzi wa bunge uliofanyika Julai 31. Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya uchaguzi huo muungano tawala wa rais Sall ulipoteza wingi bungeni. Mhariri amesema mkataba wa amani ulioafikiwa kati ya serikali na waasi wa eneo la Casamance umekuja wakati muafaka kwa rais Sall. Rais huyo alitangaza siku ya Alhamisi jioni kwa mshangao wa wengi, mkataba wa amani na sehemu ya kundi la waasi la MFDC ambalo limekuwa likiendesha uasi katika eneo la kusini mwa Senegal kwa miaka mingi. Waasi hao ambao wanapigania uhuru wa Casamance walikuwa wamewateka nyara wanajeshi wa Senegal mwanzoni mwa mwaka huu na hivyo kukoleza makali ya mzozo kati ya serikali kuu ya Mali na waasi hao.

Shirikisho la CAF mashakani

Tunakamilisha na taarifa ya gazeti la Süddeutsche kuhusu shirikisho la soka barani Afrika CAF. Gazeti hilo lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema "Dola milioni 82 zayeyuka: Shirikisho la soka la Afrika CAF lakaribia kutumbukia katika shimo la maangizi". Mhariri alisema rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino anatarajiwa kuingilia kati, lakini katika kongamano kubwa la CAF lililofanyika mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania, suala hilo lilitarajiwa kuwekwa chini ya zulia na kutozungumziwa. Gazeti la Süddeutsche liliripoti kwamba shirikisho la CAF, ambalo ndilo kubwa dunia likiwa na jumla ya nchi 56 wanachama, lilikutana kujadili mustakhbali wake, hususan hali ya kifedha inayolikabili na kuangalia fedha zilizopo katika makabrasha yake. Mhariri alisema hali ya kiuchumi ya shirikisho la CAF ni tete.

(Inlandspresse)