1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu Mhariri: Zainab Aziz
5 Aprili 2024

Miongoni mwa masuala ya Afrika yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani wiki hii ni pamoja na uteuzi wa Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuapishwa kwa Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye.

Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye akitoa hotuba baada ya kuapishwa
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye FayePicha: John Wessels/AFP

Miongoni mwa masuala ya Afrika yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani wiki hii ni pamoja na uteuzi wa Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuapishwa kwa Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye na ngezeko la mashambulizi katika pembe ya Afrika.

die tageszeitung

die tageszeitung wiki hii liliandika juu ya uteuzi wa hivi karibuni wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Juliofanywa na Rais Felix Tshisekedi. Limeanza kwa kuandika, kwa mara ya kwanza, taifa hilo lina kiongozi wa serikali mwanamke. Ni Judith Suminwa Tuluka aliyekuwa Waziri wa Mipango na mshirika wa karibu wa Rais Felix Tshisekedi.

Linaeleza kwamba, Suminwa ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa juu kama huo katika taifa lenye watu milioni 110. Gazeti hili linamnukuu Waziri wa Mazingira wa Kongo Eve Bazaiba, aliyempongeza Rais Tshisekedi kwa kumteua Tuluka kuushika wadhifa huo na kusema kwa kufanya hivyo, amejipambanua kuwa mwenye kuwaheshimu wanawake.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti hili, lilikuwa na habari juu ya kuapishwa kwa Bassirou Diomaye Faye, kuwa Rais wa Senegal.  Rais huyo mwenye umri mdogo zaidi barani Afrika, aliapishwa Jumanne, baada ya kushinda katika awamu ya kwanza ya uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 54 ya kura zote zilizopigwa. Diomaye Faye, aliachiliwa kutoka jela siku kumi kabla ya uchaguzi.

Gazeti hilo linafafanua kuwa, ahadi ya Faye kuwapa kisogo wanasiasa wasomi wa zamani, na kuhamasisha mabadiliko makubwa ya kisera yanatambuliwa na vijana walio wengi. Lakini ni wazi kuwa, hata waumini wa siasa za kihafidhina walimpigia kura. Sasa waangalizi wanatarajia mabadiliko mapya ya haraka. Jambo la kwanza kabisa ni kulivunja bunge na kisha, chaguzi zinatarajiwa kuitishwa.

Der Tagesspiegel

Der Tagesspiegel limeandika kuhusu ongezeko la mashambulizi katika pembe ya Afrika. linaeleza kuwa, hatari ya usafirishaji bidhaa kupitia Bahari katika pembe ya Afrika inaongezeka. Mbali na mashambulizi dhidi ya meli za kusafirisha bidhaa yanayofanywa na waasi wa Kihouthi wa Yemen katika Ghuba ya Aden na Bahari ya Shamu, sasa kumekuwa pia na ongezeko la mashambulizi ya maharamia.

Zaidi, gazeti hilo linafahamisha kwamba, Bahari kusini mwa Yemen na nje kidogo ya Somalia imekuwa ikifuatiliwa tangu meli za kimataifa za kivita zilipojikita kwenye Bahari ya Shamu, ili kuzilinda meli za mizigo dhidi ya Wahouthi katika mfereji wa Suez.

Maharamia nao, wananufaika kwa hili. Tangu mwezi Novemba, wameziteka nyara meli nyingi zaidi za wafanya biashara karibu na Somalia kuliko mwaka mzima uliopita. Miaka 10 iliyopita, maharamia wa Somalia walikuwa kitisho kikubwa kwa meli za mizigo kiasi kwamba Umoja wa Ulaya na mataifa mengine yalipeleka  meli za kivita katika eneo la pembe ya Afrika.

Meli yenye bendera ya Malta iliyokombolewa na jeshi la wanamaji la India baada ya kutekwa na maharamia wa SomaliaPicha: SpokespersonNavy via X via REUTERS

Der Tagesspiegel linaongeza kuwa Serikali ya Somalia haina nguvu. Maharamia wengi wanazitumia bandari zilizo katika jimbo linalojitawala la Puntland mahali ambapo mamlaka za serikali kuu mjini Mogadishi, haziwezi kufanya lolote. Ngome za maharamia katika maeneo ya bahari zipo karibu. Pwani ya Puntland iko katika Rasi ya Aden na la mlango bahari wa bahari ya shamu uko kilometa 200 pekee kutoka pwani ya kusini mwa Yemen.

die Tageszeitung

die Tageszeitung limeimulika kuhusu hatua ya Umoja wa Ulaya kuzilipa nchi kadhaa za Afrika ili kuwazuia wahamiaji haramu wasiingie Ulaya. Mhariri wa gazeti hili ameyataja mataifa hayo yaliyolipwa kuwa ni Tunisia, Mauritania na Misri.

Gazeti hilo limeandika, makubaliano yaliyofanyika kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki mwaka 2016 yalikuwa ni mwanzo tu, na sasa ni zamu ya nchi nyingine za Kaskazini mwa Afrika. Hati ya makubaliano kati ya Ulaya na Tunisia Julai 16,  2023 ilifuatiwa na makubaliano mengine yaliyofanywa na Mauritania Machi 7, 2024 na kisha Misri ikafuatia Machi 17.

Katika mikataba hiyo yote ya makubaliano, hakuna unaoonesha kiasi hasa cha fedha, lakini Tunisia iliahidiwa kupewa msaada wa kifedha wa hadi Euro milioni 165, na Mauritania iliahidiwa Euro milioni 210.

die tageszeitung linaongeza kuwa, sababu ya kufanya hivy iko wazi. Kumekuwa na ongezeko kubwa la wahamiaji wanaoelekea kaskazini wakitaka kufika Ulaya kupitia bahari ya Mediterania. Wengi wao hasa ni watu wanaokimbia vita kutoka Sudan ambayo ni Jirani wa Misri.  Kulingana na shirika la kimataifa la uhamiaji IOM, takriban wahamiaji 2,498 walikufa katika bahari ya Mediterania mwaka 2023 walipokuwa wakijaribu kuingia Ulaya.

Welt plus

Gazeti la Weltplus limeandika juu ya hatua ya Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi kutishia kuipa Ujerumani tembo 20,000. Kauli hiyo inatafsiriwa kuwa ni ya kupinga mipango ya Waziri wa Mazingira wa Ujerumani kutoka chama cha kijani Steffi Lemke, ya kutaka kupiga marufuku uingizwaji wa  wanyamapori wanaowindwa Afrika kama sehemu ya michezo, na kisha kutumika Ulaya kwa ajili ya maonesho.

Tembo katika moja ya mbuga za wanyama nchini Botswana Picha: ARTUSH/Zoonar/picture alliance

Rais Masisi ameweka wazi kwamba, mpango wa Lemke unahamasisha uwindaji haramu na umasikini. Kiongozi huyo wa Botswana aliyetoa kauli hiyo alipofanya mahojiano na gazeti la Ujerumani la Bild alisema, uwindaji wa tembo, unasaidia kudhibiti idadi ya wanyama hao.

Alitoa ufafanuzi kuwa, baada ya miaka mingi ya kampeni ya kuwalinda wanyama hao, sasa nchi yake inakabiliwa na idadi kubwa ya tembo kupindukia. Hii inasababisha vijiji na mazao kuharibiwa na wanyama hao, na ndiyo maana Masisi ametangaza kuipa bure Ujerumani tembo 20,000 kama hatua ya kupinga mpango wa marufuku ya waziri Lemke. 

Vyanzo: Deutsche Zeitungen

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW