1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika

Angela Mdungu
24 Mei 2024

Kati ya masuala ya Afrika yaliyopewa umuhimu na magazeti ya Ujerumani wiki hii ni kitisho cha kutokea mauaji ya kimbari Darfur

Symbolbild Pressespiegel
Picha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

die tageszeitung

die tageszeitung liliiangazia tahadhari iliyotolewa na Mshauri Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari Alice Wairimu Nderitu kuhusu hali ya sasa ya Darfur, aliyosema kuwa  ina sifa zote za hatari ya mauaji ya kimbari. 

Mwakilishi huyo  wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa alitoa tahadhari hiyo wakati wa mkutano maalumu uliozihusisha nchi zote wanachama wa baraza hilo ambapo ilitolewa pia ripoti ya mwaka. Ripoti hiyo iliweka wazi hali ya raia katika maeneo yote yenye mizozo kote duniani kwa mwaka uliopita. Ilionesha kuwa vifo vya raia viliongezeka kwa asilimia 72 ikilinganishwa na mwaka mmoja kabla.

Sababu kubwa ya ongezeko hilo ni mzozo wa Gaza, lakini pia watu 219,000 waliripotiwa kuwa waliuwawa na kujeruhiwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wengine 12,260 walikufa na 33,000 walijeruhiwa Sudan.

Kwa sasa mvutano kati ya jeshi la serikali na kundi la RSF unatia wasiwasi mkubwa. Kwa mujibu wa makadirio, raia wengi zaidi wameuwawa Darfur kuliko takwimu za Umoja wa Mataifa zinavyoonesha. Mapigano kwa sasa yamejikita zaidi katika eneo la El-Fashir ambao ndiyo mji mkuu pekee wa mikoa mitano ya Darfur ulio chini ya udhibiti wa serikali.

Waangalizi wa Sudan wanadhani kundi la RSF ambalo mtangulizi wake, yaani kundi la Janjaweed lilifanya mauaji ya kimbari dhidi ya wanamgambo wa kikabila  Darfur miaka 20 iliyopita, linapanga tena kufanya mauaji makubwa kwa madhumuni ya kufanya safisha safisha ya kikabila.

Welt Online

Kwa upande wake gazeti la Welt Online mwanzoni mwa juma lililiangazia jaribio la mapinduzi lillotibuliwa na jeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  Kiongozi wa jaribio hilo, mwanasiasa wa upinzani Christian Malanga has aliuwawa kwenye tukio hilo. Akiwa na washirika wake kadhaa wa kijeshi, Jumapili usiku alijaribu kuipindua serikali ya Kongo wakati jaribio hilo la uasi likirushwa mubashara kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Zaidi Welt Online linaandika, hata hivyo kasri walilolivamia lilikuwa tupu. Hata shambulizi lililoelekezwa kwa makazi ya rafiki wa karibu wa Tshisekedi liliambulia patupu. Tshisekedi na mshirika wake hawakudhurika lakini polisi wawili na washambuliaji wanne waliuwawa katika tukio hilo. Kisha, msemaji wa jeshi la Kongo alitangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa Malanga mwenyewe aliuwawa baada ya kuonesha upinzani alipokamatwa.

Jumla ya watu 50 waliopanga kufanya uasi huo walikamatwa. Watu hao ni pamoja na mshirika wa kibiashara wa Malanga, Zalman Pouln 36, anayehusishwa na biashara ya madini na kilimo cha bangi huko Msumbiji.  Wengine waliokamatwa ni mtoto wa Malanga aitwaye Marcel, mwenye miaka 21 ambaye pia ni raia wa Marekani.

Frankfurter Allgemeine

Juma hili, Frankfurter Allgemeine liliumulika uamuzi wa mahakama ya kikatiba ya Afrika Kusini iliyoamuwa kuwa  rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma hastahili kugombea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu. Siku mbili kabla ya uamuzi huo, wafuasi wa Zuma kupitia chama chake kipya cha uMkhonto weSizwe (MK.) waliujaza uwanja wa Soweto wakati wa uzinduzi wa ilani ya chama. Chama hicho kilianzishwa baada ya mpasuko katika chama tawala cha African National Congress (ANC).

Jacob ZumaPicha: Kim Ludbrook/Pool/AP/picture alliance

Hukumu hiyo imetolewa wakati tayari karatasi za kura zimeshachapishwa na Waafrika Kusini waishio nje ya nchi wameshapiga kura. Kurejea kwa Zuma katika jukwaa la siasa kama mgombea wa chama cha MK ni moja ya masuala yanayopewa uzito kabla ya uchaguzi wa bunge. Bado kuna shauku ya kuona watakachokifanya wafuasi wa chama hicho kutokana na uamuzi wa mahakama uliotolewa unaomzuia Zuma kuwa mgombea.

Miaka mitatu iliyopita, Jacob Zuma alipohukumiwa miezi 15 jela kwa kukaidi amri ya mahakama, machafuko yaliibuka katika miji muhimu ya kibiashara ya Kwa-Zulu-Natal na Gauteng, hali iliyosaabisha vifo vya mamia ya watu. Haijawa wazi pia ni hatua gani atakazochukua Zuma baada ya uamuzi huo wa mahakama.

Zeit Online

Gazeti la mtandaoni la Zeit, lilijadili namna viongozi wa bara la Afrika walivyoomboleza kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Iran Ebrahim Raisi, aliyefariki dunia kwa ajali ya helikopta Jumapili iliyopita. Limeandika, salamu za rambirambi ni sehemu ya diplomasia. Mtu anaweza kujua namna mtoa rambi rambi alivyokuwa akifikiri kisiasa juu ya aliyefariki kutokana na uchaguzi wa maneno yanayotolewa na mtoa rambirambi.

Gazeti hilo limezinukuu salamu za pole alizozitoa Rais William Ruto wa Kenya aliyesema "Tunawafariji watu wa Iran." Watu wa Iran wanaweza kujibu, asante lakini hatuhitaji. Zeit Online linadai kuwa hii ni kwa sababu Raisi alikuwa mtu asiye na huruma aliyeyazima maandamano baada ya kifo cha mwanamke wa Kikurdi Mahsa Amini.

Linabainisha kamba, uhusiano wa nchi za kiafrika na utawala wa Raisi ulitokana tu na biashara za malighafi, silaha, chuki dhidi ya mataifa ya magharibi na sera mpya ya ushirika wa kimkakati. Iran ni muhimu kwa Afrika pia kwa sababu nyingine kubwa. Kupitia mawasiliano ya kisiasa, makubaliano ya kibiashara na biashara ya silaha wanaonesha aina mpya ya kujiamini hasa mbele ya Marekani na hili linadhihirika zaidi Niger.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW