1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu
19 Julai 2024

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na tukio la miili 42 ya wanawake kugunduliwa Nairobi ikiwa imetelekezwa, na uchaguzi wa Rwanda uliompa ushindi Rais Paul Kagame

Symbolbild Pressespiegel
Picha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Süddeutsche Zeitung

Gazeti hili mwanzoni mwa juma lilimulika tukio la mwanamume mmoja aliyekiri kuwauwa wanawake 42 nchini Kenya. Kugunduliwa kwa miili ya wanawake hao iliyokuwa imetupwa katika dampo la taka jijini Nairobi kumewashtusha Wakenya wengi, tangu idara ya upelelezi ilipoanza uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa wa mauaji hayo ya kupanga.

Mtuhumiwa mwenyewe, ni kijana wa miaka 33, alikamatwa Jumatatu asubuhi. Alipohojiwa na vyombo vya usalama, alikiri kuhusika na mauaji na kuitupa miili ya wanawake hao akiwa ameifunga katika mifuko ya plastiki. Mamlaka husika zilipopekua makazi ya kijana huyo zilipatikana kadi kadhaa za simu, kompyuta, vitambulisho vya wanawake na wanaume, mikoba ya wanawake, nguo za ndani za kike pamoja na mifuko ya plastiki.

Mtuhumiwa anadaiwa kuwa aliyafanya mauaji ya wanawake hao 42 kati ya mwaka 2022 na Julai 11, 2024. Mwanamke wa kwanza aliyemuuwa, alikuwa mkewe ambaye alimnyonga kabla ya kumkatakata na kuitupa maiti yake. Hata hivyo hadi sasa haifahamiki ni kwanini kijana huyo alifanya mauaji hayo.

die tageszeitung

die tageszeitung kwa upande wake liliuangazia uchaguzi wa Rwanda uliompa ushindi wa zaidi ya asilimia 99 Rais Paul Kagame. Gazeti hilo liliandika, Rais Kagame amekuwa madarakani tangu miaka ya 1990.. Matokeo yaliyompa ushindi wa asilimia 99.15 hayashangazi.

Zaidi ya vituo vya 2,500 vya kupigia kura vilifungwa Jumatatu mchana na kisha zoezi la kuhesabu kura likaanza. Jioni siku hiyo hiyo, tume ya taifa ya uchaguzi, ilitoa matokeo ya awali baada ya asilimia 80 ya kura zote kuhesabiwa.

Wapinzani wawili wa Kagame kwa pamoja hawakupata hata asilimia moja ya kura zote. Frank Habineza wa chama cha kijani alipata asilimia 0.53 ya kura na mgombea binafsi Philippe Mpayimana alipata kura 0.32. die tageszeitung linaarifu kuwa, takriban Wanyarwanda milioni 2 walishiriki kupiga kura kwa mara ya kwanza. Raia wengine 70,00 waliandikishwa kama wapiga kura walio nje ya Rwanda na walishapiga kura Jumapili.

Rais Paul Kagame wa Rwanda wakati wa uchaguzi mkuu wa Julai 15Picha: Luis Tato/AFP via Getty Images

Licha ya kuwa raia wengi wa taifa hilo wanaoishi uhamishoni wanamkosoa vikali Kagame, kiongozi huyo alipata zaidi ya asilimia 95 ya kura zao. Kagame mwenyewe baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, alisema kampeni za uchaguzi na matokeo yaliyokwisha kutangazwa yana maana kubwa kwake na yanadhihirisha imani kubwa watu waliyonayo kwake. Matokeo rasmi ya uchaguzi huo hata hivyo yatatangazwa Julai 27.

Frankfurter Allgemeine

Frankfurter Allgemeine wiki hii liliandika kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani umezidi kuwa mbaya.  Idadi ya wakimbizi wanaotokana na vita vya Sudan imezidi watu milioni kumi, kulingana na taarifa ya Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Uhamiaji IOM. Katika ripoti iliyototewa Jumanne wiki hii.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa karibu robo tatu ya watu hao wamelazimika kuhama  au hawana makazi tangu vita hiyo vilipoanza Aprili 15 2023. Idadi hiyo ni sawa na humusi ya idadi yote ya watu nchini humo. Zaidi ya watu milioni 2.2 wamekimbilia nchi nyingine na wengine wako ndani ya mipaka ya Sudan. 

Vita nchini humo vilianza kutokana na ugomvi wa madaraka kati ya mkuu wa jeshi rasmi la Sudan Jenerali Abdel-Fattah Burhan na  Mohammed Hamdan Dagalo, anayeongoza kikosi cha RSF.

Gazeti hilo limeongeza kuwa,  mapigano ni makali hasa Darfur. Shirika la kimataifa la uhamiaji la IOM linasema, karibu nusu ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao wanaishi huko. Wengi wao wanakabiliwa na njaa. Na kutokana na mapigano mashirika mengi ya kutoa misaada yanashindwa kufika katika maeneo mengi.

Jumanne wiki hii, mwakilishi wa shirika la afya duniani WHO alisema kuwa zaidi ya watu 800,000 wamenasa katika eneo hilo na hawawezi kupatiwa mahitaji muhimu kama vile chakula na dawa. Mazunguzo ya usuluhishi kati ya pande hasimu chini ya Umoja wa Mataifa yanaendelea Geneva ili kusaidia misaada ifike katika maeneo kama al-Fashir.

die tageszeitung

die tageszeitung liliimulika hali ya kisiasa nchini Misri. Lilikuwa na kichwa cha habari kilichouliza; Ni nani mwenye uthubutu wa kusimama dhidi ya Rais Sisi? Limeandika, Mwanasiasa  wa upinzani Ahmed al-Tantawi alitaka kuonesha upinzani dhidi ya Rais Sisi na sasa yuko gerezani. Mwanasheria wa kutetea haki za binadamu anayemuwakilisha pia Tantawi, Khaled Ali amesema hajamuona mteja wake tangu alipohukumiwa kifungo gerezani, licha ya ofisi ya mwendesha mashtaka kutoa kibali cha kumuona.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mkosoaji mkubwa wa rais Abdelfattah al-Sisi, alikamatwa na mamlaka za Misri mwezi Mei baada ya mahakama kuamuru yeye na wafuasi wake 22 wafungwe kwa mwaka mmoja. Tantawi pia amepigwa marufuku kushiriki katika uchaguzi kwa muda wa miaka mitano kwa madai ya kuvunja sheria ya uchaguzi.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Misri Ahmad al-TantawiPicha: Ahmed Hasan/AFP

Kifungo chake kimeibua ukosoaji mkali Misri na nje ya nchi hiyo. Mwezi Juni, raia, mashirika, pamoja na vyama vya siasa waliwasilisha malalamiko ya kutaka mwanasiasa huyo na wenzake waachiwe huru.

Hakujawa na maandamano ya umma ya kumuunga mkono kutokana na ukandamizaji wa polisi. Vikosi vya usalama, tayari vimeshawakamata makumi ya wafuasi wa Tantawi, wanaharakati na baadhi ya wanachama wa chama chake.

Mustakabali wa mwanasiasa huyo hautofautiani na wa wanasiasa wengine waliowahi kutaka kumuonesha upinzani Sisi. Katika uchaguzi wa mwaka 2018, wagombea watatu kati ya wanne walilazimishwa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW