1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu
25 Oktoba 2024

Kati ya yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika ni pamoja na mauaji dhidi ya wanasiasa wawili wa upinzani nchini Msumbiji na kuonekana tena hadharani kwa Rais wa Cameroon Paul Biya 91.

Symbolbild Pressespiegel
Picha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

die tageszeitung

die tageszeitung wiki hii liliiyamulika  mauaji dhidi ya wanasiasa wa upinzani nchini Msumbiji. Limeeleza kwamba, kuuwawa kwa wanasiasa hao kumesababisha mgogoro baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 9. Jumatatu, polisi katika mji mkuu Maputo, walilazimika kutumia mabomu ya machozi dhidi ya waandamanaji  baada ya upinzani kuitisha mgomo na maandamano ambayo yalipigwa marufuku.

Wanasiasa wa upinzani waliouwawa ni Elvino Dias na Paulo Guambe wa chama kipya cha upinzani cha Podemos. Walikuwa ndani ya gari mjini Maputo wakati magari mengine yalipozuia barabara waliyotumia, na kisha watu wawili wenye silaha waliwafyatulia risasi.

Chama cha Podemos cha wanasiasa hao kilimuunga mkono mgombewa Urais Venancio Mondlane, anayekituhumu chama tawala FRELIMO kwa udanganyifu katika uchaguzi wa Oktoba 9. FRELIMO ambacho kulingana na matokeo ya uchaguzi yaliyotangwazwa na tume ya uchaguzi kimeshinda kupitia kwa mgombea wake Daniel Chapo, kimeiongoza Msumbiji tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno mnamo mwaka 1975.

Gazeti hilo hilo, die tageszeitung liliandika pia kuhusu kurejea nyumbani kwa Rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani Paul Biya wa Cameroon baada ya kutoonekana hadharani kwa muda mrefu.

Gazeti hilo limeandika, televisheni ya taifa ilirusha matangazo ya moja kwa moja yaliyoonesha misururu mirefu ya watu wakishangilia barabarani. Zulia jekundu lilitandikwa katika uwanja wa ndege Jumatatu jioni kumpokea rais Paul Biya mwenye miaka 91 baada ya kiongozi huyo kutokuwepo nchini humo kwa zaidi ya siku 49.

Ujio wake ulichukuliwa mithili ya ziara ya kiongozi wa kigeni wakati Biya akitokea Uswisi anakokwenda mara kwa mara kwa ajili ya matibabu. Mara ya mwisho, kiongozi huyo wa Cameroon alionekana hadharani Septemba 8 akielekea katika mkutano wa kilele wa China na bara la Afrika.

Oktoba 7, shirika la Habari la ABS lenye makao yake Marekani lilinukuu chanzo kimoja ambacho hakikutajwa jina kikidai kuwa Rais huyo amekufa.  Ofisi ya Biya ilitoa taarifa kukanusha uvumi huo na kusema Biya hajambo na angerejea Cameroon baada ya siku chache na kuwa alikuwa kwenye shughuli zake Geneva akiwa na afya njema.

Rais wa Cameroon Paul BiyaPicha: Jemal Countess/UPI/newscom/picture alliance

Zaidi serikali ya Yaounde ilipiga marufuku vyombo vya Habari kujadili hali ya Rais Biya ama la vingeadhibiwa. Kiongozi huyo aliyekaa madarakani tangu mwaka 1982  anataka kukitetea tena kiti chake kwa muhula wa nane katika uchaguzi wa mwakani.

Süddeutsche Zeitung

Süddeutsche Zeitung  liliuangazia mgogoro wa uhamiaji barani Ulaya na juhudi za kuwadhibiti wahamiaji hasa kutoka  Afrika. Lilianza kwa kuandika, mkutano wa hivi karibuni wa Umoja wa Ulaya ulitawaliwa na hofu. Zaidi liliandika, kuna mazungumzo kuhusu nchi zinazopaswa kutumika kama vituo vya kuwarejesha wahamiaji hao nje ya Umoja wa Ulaya ambapo waomba hifadhi walionyimwa hadhi hiyo wanawaza kuhifadhiwa hadi nchi zao zitakapowachukua. Mfano mzuri wa hivi karibuni ni Albania ambapo waomba hifadhi kutoka Italia walipelekwa Albania.

Hata hivyo mataifa kama vile Poland, Hungary na Uholanzi hayataki tena kutumia sheria hiyo ya Umoja wa Ulaya, na Rais wa Halmashauri Kuu ya umoja huo Ursula von der Leyen, si tu kuwa anaunga mkono bali pia  anatoa wito wa kufanyika makubaliano ya kuwa na vituo vingine vya kuwapeleka wahamiaji hao kama ilivyo kwa Libya na Tunisia.

Mhariri wa Süddeutsche Zeitung  ameandika mapendekezo haya hayana uhalisia kwani hakuna nchi inayotaka ardhi yake iwe na vituo vya aina hiyo  ambavyo mara nyingi huzungushiwa uzio thabiti vikiwa vimezingirwa na walinzi wenye silaha.

Mpango wa Italia kwa mfano wa kuwapeleka gerezani wahamiaji huko Albania umezuiwa na mahakama. gazeti hilo linaongeza kuwa, makubaliano yasiyo na maadili yaliyofanywa baina ya Ulaya na nchi za Kaskazini mwa Afrika  yanayolenga kuwazuia wahamiaji kuingia Ulaya nayo hayana uhalisia na hayawezi kufika kokote.

Welt Plus

Gazeti la Welt Plus, wiki hii liliandika kuhusu mtandao wa uhalifu wa Afrika ujulikanao kama Black axe unaozidi kuota mizizi Ulaya na hata Ujerumani. Mtandao huo unachukuliwa kuwa ndiyo mtandao wa uhalifu wenye nguvu zaidi barani Afrika. Unahusisha ulanguzi wa dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu. Mtandao huo una ushawishi mkubwa katika ngazi ya juu ya siasa na tayari umeshaingia barani Ulaya. 

Habari hii iliandikwa baada ya mmoja wa wahusika wa mtadao huo aliyejitambulisha kama Francisco kukubali kufanya mahojiano na Welt plus kwa masharti kadhaa yakiwemo kutotajwa jina, kutochapisha sauti iliyorekodiwa wakati wa mahojiano na kuwa sura yake haipaswi kuchapishwa kokote.

Afisa upelelezi wa Munich, Ujerumani akionesha shoka dogo jeusi lenye maneno, King Zulu linalotumika kama alama ya mtandao wa uhalifu wa Black Axe.Picha: Britta Schultejans/dpa/picture alliance

Kijana huyo ni mwanachama wa ngazi ya chini wa genge hilo la uhalifu lililodumu kwa miongo mingi ambalo asili yake ni Nigeria. Anasema aliingizwa kwenye mtandao huo miaka 20 iliyopita kwa kufanyiwa tambiko. Alianza kwa kufanya uporaji na uhalifu mwingine mkubwa lakini kwa sasa anatumika kufuatilia shughuli za polisi na makundi hasimu Pamoja na kusajili wanachama wapya wa mtandao huo haramu.

Francisco amezungumzia kuhusu mauaji, uhalifu wa mtandaoni, usafirishaji wa dawa za kulevya na binadamu ikiwemo kuwaingiza wahamiaji ulaya kinyume cha sheria.

Tangu mwezi Aprili hadi Julai mwaka huu polisi ya kimataifa Interpol ilifanya operesheni inayoitwa Jackal III katika nchi 21 ili kuunasa mtandao huo. 

Tayari watu 300 wanashikiliwa na polisi, 11 kati ya hao walikamatwa Ujerumani. Akaunti 720 za benki za mtandao huo na mali zenye thamani ya mamilioni ya fedha  zimezuiwa. Taarifa ya Interpol inasema kuna uhitaji mkubwa wa ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na mitandao mikubwa ya uhalifu kama Black axe.