1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu
15 Novemba 2024

Magazetini Ujerumani, matarajio ya uhusiano wa Afrika na serikali ijayo ya Donald Trump yameangaziwa na athari zilizosababishwa na mafuriko Sudan Kusini zimemulikwa.

Symbolbild Pressespiegel
Picha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Zeit Online

Zeit Online Juma hili limeandika kuhusu matarajio ya uhusiano kati ya bara la Afrika na uongozi wa Rais mteule wa Marekani Donald Trump atakayeanza muhula wake wa uongozi mwezi Januari.

Limeeleza kuwa, hadi sasa Trump hajaonesha kutaka kujihusisha na nchi za Kiafrika. Lakini kutokana na ushindani na China huenda akanza kuchagua nchi anazoweza kuzipa kipaumbele barani humo, na maadui wapya.

Jambo moja bado linaendelea kukumbukwa wakati wa mhula wake wa kwanza madarakani. Aliziita nchi za Kiafrika zisizo na maana na kulipuuzia bara hilo, na hakuna ishara  inayoonesha kama amebadili msimamo wake. Licha ya hilo, Marekani haitarajiwi kuachana na bara hilo kwa namna yoyote.

Zeit Online, limejaribu kuziainisha nchi za Kiafrika zilizoupokea vyema ushindi wa Trump kuwa ni Uganda, ambayo chama chake tawala kilikuwa na uhusiano mbaya na utawala wa  Biden, anayeelekea kumaliza muda wake kutokana na sera za Kampala zinazopinga mapenzi ya jinsia moja.

Limeongeza kuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kwa upande wake alionesha kufurahishwa na ushindi wa Trump. Serikali mpya ya Marekani huenda ikawa na uhusiano mzuri na nchi hiyo, ambayo Wakristo wake wa madhehebu ya Orthodox wanafahamika kuwa upinzani dhidi Waislamu wenye itikadi kali.

Kwa upande wa Kenya, Rais Ruto anasubiri kwa tahadhari kuapishwa kwa Trump. Nchi yake ilikuwa kipenzi cha utawala wa Biden. Gazeti hili limeeleza mengi lakini limemalizia kwa kuandika kuwa, huenda Trump akapunguza misaada ya fedha ambayo tayari ni midogo kwa mataifa masikini ya Kiafrika yanayohitaji sana msaada huo, katika kuwalinda watu wake dhidi ya ukame, mafuriko na kuratibu mipango ya mabadiliko ya kuelekea matumizi ya nishati jadidifu.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine katika toleo lake la mtandaoni mwanzoni mwa juma, lilijielekeza katika athari za mafuriko yaliyotokea Sudan Kusini juma lililopita. Limezinukuu takwimu za Umoja wa Mataifa zinazoonesha kuwa, karibu watu 400,000 hawana makazi kutokana na mafuriko hayo na kwamba maambukizi ya Malaria yako katika kiwango cha juu. Hali hiyo inauelemea mfumo wa huduma za afya wakati nchi hiyo tayari ina hali tete ya kiutu.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu milioni 1.4 wameathiriwa na mafuriko hayo yaliyosababisha uharibifu mkubwa hasa kaskazini mwa nchi.

Benki ya dunia ilishatahadharisha kuwa mafuriko yangeifanya hali kuwa mbaya zaidi katika taifa hilo linalokabiliwa na uhaba wa chakula, kudorora kwa uchumi na mzozo wa wa muda mrefu, milipuko ya maradhi na athari za vita vinavyoendelea kwenye taifa jirani la Sudan.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP linakadiria kuwa zaidi ya watu milioni saba wa Sudan Kusini wanahitaji chakula, na Watoto milioni 1.65 wanakabiliwa na utapiamlo. Zaidi ya hapo nchi hiyo imekuwa katika mgogoro mkubwa wa uchumi na siasa tangu ilipopata uhuru kutoka Sudan mwaka 2011. Lakini pia bado haijaimarika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu laki nne.

die tageszeitung

die tageszeitung limejitosa kuyamulika matumaini ya watu wa Senegal katika serikali ya Rais Diomaye Faye. Aidha, gazeti hilo limeandika kuwa, vijana wengi wa Senegal wanafanya safari hatari za kuvuka bahari ya Atlantiki kuelekea Ulaya. Rais anayefuata siasa za mrengo wa kushoto Bassirou Diomaye Faye anataka vijana hao wabaki nyumbani wakati sera na matumaini yake vikitegemea wingi wa viti vya wabunge vitakavyopatikana baada ya uchaguzi wa Jumapili.

Rais wa Senegal Diomaye Faye Picha: Mosa'ab Elshamy/AP/picture alliance

Uchaguzi huo unachukuliwa kuwa hatua muhimu kwa utekelezaji wa ajenda mpya za kisiasa za serikali mpya ya Faye na Waziri  Mkuu Ousmane Sonko walioingia madarakani mwezi Aprili mwaka huu.

Neue Zürcher

Kwa upande wake Neue Zürcher liliimulika hatua ya kukamatwa kwa Meneja wa mgodi wa Resolute nchini Mali. Limeanza kwa kueleza kuwa mgogoro kati ya serikali ya kijeshi chini ya Rais Assimi Goïta na makampuni ya magharibi unaendelea kupamba moto.

Tukio la hivi kariuni zaidi linaihusu kampuni ya kuchimba madini ya Resolute ya Australia inayofanya kazi kwenye mgodi wa Siyama. Mwishoni mwa wiki iliyopita, mamlaka za Mali zilimkamata Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Terry Holohan na watendaji wengine wawili wa ngazi ya juu mjini Bamako.

Tangu wakati huo, thamani ya soko la kampuni hiyo imeporomoka kwa theluthi moja. Kampuni ya Resolute kwa upande wake iliandika kwenye tovuti yake kuwa Watendaji wake hao watatu walikamatwa bila kutarajia baada ya kuzungumza na serikali kuhusu matakwa yake kwa kampuni hiyo. Hakukutolewa ufafanuzi wa haraka zaidi kuhusu suala hilo.

Gazeti la Neue Zürcher limekumbusha kuwa mwezi Semptemba, mamlaka nchini humo ziliwakamata wafanyakazi watatu wa kampuni nyingine ya Canada inayojishughulisha na Sekta ya madini iitwayo Barrick Gold kwa tuhuma za malimbikizo ya kodi yanayokaribia dola milioni tano.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya usalama  Beverly Ochieng, kukamatwa huko ni sehemu ya juhudi za serikali ya Mali  kuongeza kipato kupitia sekta ya madini. Sheria mpya iliyopitishwa nchini humo mwaka 2023 inaiwezesha serikali hiyo kuongeza hisa zake kwenye makampuni za kimataifa kutoka asilimia 20 hadi 35. Taifa hilo lina kampuni 15 za kigeni za uchimbaji madini zinazofanya kazi Mali kwa muda mrefu.