1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu
29 Novemba 2024

Magazetini Ujerumani, hali ya misaada ya chakula Sudan imeangaziwa, maandamano ya Msumbiji baada ya uchaguzi nayo pia yamemulikwa.

Misaada ya chakula Sudan
Malori ya misaada ya chakula ya Shirika la mpango wa Chakula WFP nchini SudanPicha: ASHRAF SHAZLY/AFP

die tageszeitung

die tageszeitung juma hili limeangazia hali ya njaa na upelekwaji wa msaada wa chakula huko Sudan. Limeandika, kwa mara ya kwanza katika miezi mingi, watu milioni moja wanaokadiriwa kuishi katika kambi kubwa zaidi ya raia waliokimbia vita Darfur huko magharibi mwa Sudan, wamepokea msaada wa chakula kutoka Umoja wa Mataifa.

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limetangaza kuwa msafara wa malori mawili yaliyobeba chakula yaliifikia kambi hiyo ya Zamzam iliyo nje kidogo mwa mji wa El Fashir ambao ni uwanja wa mapambano, Ijumaa iliyopita.

Msafara huo uliokuwa ukitokea katika mji wa Port Sudan, ulibeba tani 330 za chakula na mwingine kutoka kwenye mji wa Adre katika taifa jirani la Chad, ulibeba tani nyingine 150. Hata hiyvo Shirika la Mpango wa Chakula la WFP linasema kiasi hicho cha chakula ni kidogo sana kwa wakimbizi wote wa kambi ya Zamzam.

Shirika hilo kwa ujumla linasema walau kumekuwa na ongezeko la msaada wa kukabiliana na njaa, tangu katikati mwa mwezi Novemba, wakati  utawala wa jeshi nchini humo uliporuhusu kufunguliwa kwa kivuko cha mpaka wa Adre kutoka Chad.

Mapema Jumatatu, Kiongozi wa utawala huo,  Jenerali  Abdelfattah al-Burhan aliruhusu kufunguliwa kwa vituo vya kutoa  misaada vya Umoja wa Mataifa katika baadhi ya maeneo. Aliruhusu pia wafanyakazi wa shirika hilo kuyasindikiza malori ya misaada ili kusimamia ugawaji. Awali serikali ya kijeshi ya Sudan ilitaka kuisimamia yenyewe misaada hiyo.

Frankfuter Allgemeine

Frankfuter Allgemeine limeimulika hali ya kisiasa Msumbiji. Mhariri ameanza kwa kueleza kuwa, nchini humo, vikosi vya usalama kwa mara nyingine vimetumia nguvu dhidi ya maandamano makubwa ya amani yaliyolenga kupinga ushindi wenye utata wa chama tawala cha FRELIMO.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, saa chache kabla ya hatua hiyo, Tume ya Umoja wa Ulaya ilitoa wito kwa pande zote kuwa na uvumilivu na kuepuka kufanya ghasia.

Akitoa hotuba yake kwenye bunge la Umoja wa Ulaya mjini Strasbourg Jumanne wiki hii, Kamishna wa masuala ya usawa  Helena Dalli, alisema Umoja wa Ulaya unapaswa kuzungumza kwa uwazi na serikali ya Msumbiji na kuwa haupaswi kuikalia kimya hali katika taifa hilo.

Wanajeshi wa Msumbiji wakikabiliana na waandamanaji mjini MaputoPicha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limemnukuu Dalli akisema, tangu uchaguzi wa rais na wabunge uliofanyika Oktoba 9, machafuko yamesambaa na kwamba, ukatili na ukandamizaji wa polisi umezidisha vurugu. Zaidi ameongeza kusema, ni muhimu kwa kila sauti kusikika na matumizi mabaya ya nguvu yanayofanywa na pande zote hayana budi kukoma.

Die Zeit

Jingine lililopewa nafasi katika magazeti ya Ujerumani juma hili ni tukio la kusikitisha la boti ya watalii iliyozama katika eneo la Sataya Jumatatu nje kidogo ya Pwani ya Misri. Gazeti la die Zeit limeripoti kuwa, kufikia Jumanne, miili minne ya watu waliokuwemo kwenye boti iliyozama iliopolewa na timu ya uokoaji .

Kabla ya ajali hiyo inaarifiwa kuwa, wahudumu wa boti hiyo walituma ishara ya kutokea kwa hitilafu Jumatatu asubuhi baada ya kuanza safari Jumapili kwa ajili ya kufanya utalii karibu na Hurghada. Kwa mujibu wa Gavana wa Mkoa ulikotokea mkasa huo Amr Hanafi, chombo hicho kilikuwa na abiria 31 na wahudumu 14.

Hadi Jumanne ni watu  33 waliokuwa wameokolewa karibu na mji wa Pwani wa Marsa Alam. Gavana Hanafi, awali alisema kuwa Wajerumani wanne ni miongoni mwa abiria waliokuwemo kwenye boti hiyo sambamba na watalii wengine 20 kutoka mataifa ya Ulaya.

Kutokana na maelezo ya abiria na wahudumu waliookolewa, boti hiyo ilipinduka na kuzama baada ya kupigwa na mawimbi makali. Baada ya hali hiyo, baadhi ya abiria hawakufanikiwa kutoka kwenye vyumba vyao kwa wakati. Gavana Hanafi amesema, boti hiyo haikuwa na tatizo lolote la kiufundi na ilifshafanyiwa ukaguzi mnamo mwezi Machi.

die tageszeitung

die tageszeitung limeandika pia kuhusu hali ya mambo ndani ya utawala wa kijeshi wa Mali kutokana na kufutwa kazi kwa aliyekuwa Wazri Mkuu wa mpito Choguel Maïga.

Miaka minne baada ya mapinduzi, sasa umesalia utawala kamili wa kijeshi nchini Mali. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa kiraia Choguel Maïga amefutwa kazi na nafasi yake sasa inashikiliwa na Jenerali Abdoulaye Maiga.

Waziri Mkuu wa mpito aliyetimuliwa alikuwa kiongozi wa juu zaidi wa kiraia katika serikali hiyo ya kijeshi. Alitokea katika chama cha vuguvugu la waandamanaji la M5-RFP ambalo liliipinga serikali iliyopinduliwa na jeshi, ya Rais aliyekuwa amechaguliwa kwa njia ya demokrasia  Boubacar Keita.

Vuguvu  hilo la waandamanaji liliunga mkono mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Kanali Goita, aliyejihakikishia mamlaka kamili mwaka 2021. Baada ya hapo, Kanali huyo aliahirisha uchaguzi uliokuwa umeahidiwa kufanyika mwaka 2022 hadi Machi 2024. Uchaguzi huo uliahirishwa tena kwa kipindi kisichojulikana.

Choguel Kokalla MaïgaPicha: Website des Premierministers Choguel Kokalla Maïga

Wakati vuguvugu la kiraia limekuwa likipinga tena utawala wa sasa, Choguel Maiga aliendelea kuwa mtiifu kwa uongozi wa kijeshi. Hivi karibuni alipokuwa bado Waziri Mkuu, aliruhusu kiasi kidogo cha ukosoaji.

November 16, Maiga aliwaambia wanaharakati wa vuguvugu la M5-RFP kuwa serikali anayoiongoza imejawa na mkanganyiko na taifa linahitaji maelezo ya namna kipindi cha mpito kitakavyokamilika.

Siku chache baadaye Waziri Mkuu huyo alitumbuliwa. Vyombo vya habari vya Mali vinaashiria kuwa baada ya Choguel Maiga, kuondolewa madarakani, yawezekana sasa upinzani umepata mgombea dhidi ya Jenerali Goita ikiwa atataka kuthibitishwa kuwa rais kama uchaguzi utafanyika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW