1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu
17 Januari 2025

Magazetini Ujerumani, Kuapishwa kwa Daniel Chapo Msumbiji, kutekwa nyara kwa mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi Tsehai, na vifo vya watu 100 mgodini Afrika Kusini ni miongoni mwa yaliyozingatiwa.

Daniel Chapo - Msumbiji
Rais mpya wa Msumbiji Daniel Chapo aliyeapishwa 15.01.2025Picha: PHILL MAGAKOE/AFP/Getty Images

 die tageszeitung

Juma hili, die tageszeitung limeandika kuhusu kuapishwa kwa Daniel Chapo ambaye ameingia madarakani na kuwa Rais wa tano wa Msumbiji. Limeeleza kwamba, wakuu wengi wa mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC hawakuhudhuria katika shughuli ya kuapishwa kwa kiongozi huyo na badala yake waliwakilishwa na mawaziri.

Marais pekee waliohudhuria katika shamrashamra hizo ni Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na Umaro Sissoco Embaló wa Guinea Bissau. Mahudhurio hayo ni tofauti na yale ya wiki moja iliyopita wakati wa kuapishwa kwa Rais mpya wa Ghana John Dramani Mahama ambapo zaidi ya wakuu 30 wa nchi walishiriki.

Katika hotuba yake kwenye shughuli hiyo Rais Daniel Chapo hakuzungumzia kwa uwazi ghasia za miezi kadhaa ya hivi karbuni za baada ya uchaguzi. Alikaa kimya kwa dakika moja pekee kutoa heshima kwa watu 120 waliouwawa kwa kimbunga Chido na  wale aliowataja kuwa waliokufa, na kujeruhiwa au kupata hasara kubwa. Aliongeza kuwa kwa sasa watu wa Msumbiji wanahitaji kuungana ili kutengeneza mustakabali bora kwa taifa hilo.

Uhalali wa Chapo unapingwa baada ya kupata ushindi katika uchaguzi, ambapo aligombea kwa tiketi ya  chama cha FRELIMO kilicho madarakani tangu mwaka 1975.

 die tageszeitung

Gazeti hilohilo,  die tageszeitung,  mwanzoni mwa Juma liliandika juu ya tukio la kutekwa nyara kwa saa kadhaa kwa mwandishi habari na mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi Tsehai mchana kweupe, katikati mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi anapoishi uhamishoni kwa miaka minne sasa. Gazeti hili limebainisha kuwa,  Tsehai alitekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni maafisa wa usalama wa taifa wa Tanzania

Akiuzungumzia mkasa huo siku iliyofuata mwanaharakati huyo wa haki za binadamu anasema alitekwa wakati alipokuwa akitoka kutengeneza nywele saluni. Wakati akitoka katika eneo la kupaki magari, alisimamishwa na wanaume wawili waliovalia mavazi meusi.

Die tageszeitung linamnukuu Sarungi akisema kuwa watu hao walifungua mlango wa gari kisha wakamvuta na kumuingiza kwa nguvu kabla ya kuondoka naye.

Mwanaharakati wa haki za binadamu wa Tanzania Maria Sarungi TsehaiPicha: Imani Nsamila

Linaenda mbele zaidi na kueleza kwamba Sarungi si mwathiriwa wa kwanza maarufu aliyewahi kutekwa jijini Nairobi. Mwishoni mwa mwezi Novemba, watu wenye silaha waliovalia nguo za kiraia walimkamata kwa nguvu kiongozi mkubwa wa upinzani wa Uganda, Kiiza Besigye na kumrejesha Kampala ambako sasa anakabiliwa na kesi katika mahakama ya kijeshi ya Uganda.

Kwa sasa, kupitia #EndAbductionsKe, inayomaanisha komesha utekaji Kenya, watu wanawasaka watekaji wa Maria Sarungi Tsehai. Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International upande wa Kenya lilichapisha video zinazowaonesha watu wawili waliovalia mavazi meusi walioonekana muda mfupi kabla ya  kutekwa kwa mwanaharakati huyo nje ya saluni aliyokuwemo Tsehai. Chini ya chapisho la video hizo kuna maandishi yanayosomeka, "Yeyote mwenye taarifa kuhusu utambulisho wa watu hawa wawili anaombwa kuwasiliana nasi”.

Die Welt

Mkononi nalikamata gazeti la die welt, ambalo kwa upande wake lilivimulika vifo vya watu takriban 100 waliokufa katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa huko Afrika ya Kusini. Idadi hiyo ni kulingana na Sabelo Mnguni afisa mkuu kitaifa wa jamii zilizoathiriwa na uchimbaji wa madini.

Mnguni alitanabaisha kuwa,  picha za video zilizochukuliwa kwa njia ya simu, zilionesha makumi ya miili ya watu ikiwa imefungwa katika mifuko ya plastiki chini ya ardhi, ndani ya machimbo hayo.

Die Welt limemnukuu Mnguni akisema watu waliokuwa kwenye mgodi huo ambao polisi walijaribu kuwaondoa mnamo mwezi Novemba, huenda walikufa kwa njaa kali au kutokana na  kiu.

Miezi miwili iliyopita, kwa mara ya kwanza mamlaka za Afrika Kusini  zilijaribu kuwatoa wachimbaji hao nje ya mgodi huo uliotelekezwa. Polisi nchini humo imefafanua kuwa wachimbaji hao walikataa kutoka nje wakihofia kukamatwa.

Die Welt

Gazeti hilo hilo la die Welt limeandika kuhusu hofu ya kuwepo kwa mlipuko wa virusi  vya Marburg nchini Tanzania. Linaeleza kwamba, watu 8 wanaaminiwa kuwa  wamefariki dunia kutokana na maambukizi hayo.  Shirika la Afya Duniani WHO linakadiria kuwa kitisho cha maradhi hayo katika eneo hilo ni kikubwa.

Katibu Mkuu wa WHO Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Jean Bizimana/REUTERS

Kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali, kuharisha, kutapika damu, kudhoofika na kisha kutokwa damu katika matundu ya mwili.

Shirika hilo la Afya la Umoja wa Mataifa linakisia kuwa hadi sasa hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo duniani kote ni ndogo. Hii ni kwa sababu wagonjwa walioripotiwa kuwa na maambukizi walikuwa kutoka mkoa wa Kagera ambao ni kituo kikubwa cha wasafiri. Kutoka hapo watu kadhaa wanaweza kuvuka mpaka kuingia Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi  ya Kongo. Hivyo hatari ni kubwa katika kiwango cha taifa na kanda pekee.

Die Welt linaandika, virusi va Marburg, haviambukizwi kirahisi. Mara nyingi huambukizwa kupitia mgusano wa majiaji ya mwili ya mtu ambaye tayari anaonesha dalili.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW