1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hijabu lazima Gambia

11 Januari 2016

Magazeti ya Ujerrumani yameandika juu ya idadi kubwa ya vijana wa Eritrea wanaoikimbia nchi yao ,na amri iliyotolewa nchini Gambia kuwalazimisha akina mama kuvaa hijabu. .

Wakimbizi kutoka Eritrea wawasili Italia
Wakimbizi kutoka Eritrea wawasili ItaliaPicha: DW/M. Williams

Gazeti la "Die Zeit" linafahamisha katika makala yake kwamba hakuna kwingineko barani Afrika ambako wananchi na hasa vijana wanaikimbia nchi yao kwa wingi, kama jinsi inavyotokea nchini Eritrea.


Gazeti la "Die Welt" limetoa mfano wa daktari mmoja- Tesfay.Daktari huyo aliondoka Eritrea mnamo mwezi wa Oktoba mwaka uliopita na kuacha pengo katika utoaji wa huduma za afya.

Kwa wastani,watu 5000 wanaondoka kila mwezi, katika nchi hiyo yenye jumla ya wananchi Milioni sita. Gazeti hilo linauliza kwa nini watu hao wenye umri wa kuanzia miaka 17 hadi 40 wanaihama nchi yao?

Haki za binadamu zikiukwa kwa kudhamiria

Gazeti la "Die Welt" linaeleza kwamba mnamo mwezi wa Juni mwaka uliopita Baraza la haki za binadamu, la Umoja wa Mataifa lilichapisha ripoti juu ya kukiukwa haki za binadamu,kwa kudhamiria nchini Eritrea.

Serikali ya Eritrea inautekeleza mpango wa kujenga taifa ambao ni wa lazima kwa kila mwananchi. Gazeti la "Die Welt " linafahamisha kwamba, kila mwananchi anapaswa kushiriki katika mpango huo wa kujenga taifa kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Lakini unaweza kurefushwa kwa muda usiojulikana.

Gazeti hilo limezikariri taarifa za mashirika ya haki za binadamu ,yanayodai kwamba watu nchini Eritrea wanalazimishwa kulitumikia jeshi kwa muda usiojulikana chini ya mpango huo wa kujenga taifa.

Akina mama watumishi wa umma wameambiwa lazima wavae hijabu wanapokuwa kazini nchini Gambia.

Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" Rais wa Gambia Yahya Jammeh alitoa amri hiyo baada ya kuitangaza nchi yake kuwa ,Jamhuri ya Kiislamu mnamo mwezi wa Desemba mwaka uliopita. Rais Jammeh ameichukua hatua hiyo ili kuvutia misaada kutoka nchi tajiri za kiislamu .

Rais wa Gambia Yaha JammehPicha: picture-alliance/Landov/M. Theiler

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema uamuzi wa Rais Jammeh unaweza kuelekweka ikiwa mtu atatumbua kwamba mfadhili mkubwa wa Gambia, yaani Umoja wa Ulaya, siku nyingi umesimamisha misaada yake ya fedha kwa nchi hiyo ya Afrika magharibi. Ingawa idadi kubwa ya wananchi, yaani, asilimia 90 ni Waislamu,wako pia Wakristo na watu wanaofuata imani za jadi.

Mwaka wa 2015 ulikuwa mbaya sana kwa ndovu barani Afrika.Ulikuwa mwaka wa maangamizi ya viumbe hao.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeikariri taarifa ya shirika la ulinzi wa wanyama pori, IFAW inayosema kwamba tani 32 za pembe za ndovu zilikamatwa mnamo mwaka wa 2015.

Gazeti hilo linafahamisha kwamba nchini Thailand pekee tani saba za meno ya tembo, zilikamatwa mwaka jana .Na katika Singapore, maafisa wa idara ya ushuru walizinasa tani 3.7 za vipusa. Kuanzia mwaka wa 2013, idadi ya ndovu waliouliwa ni kubwa kuliko ya wale wanaozaliwa.

Kwa mujibu wa idara kuu ya takwimu za ndovu,wanyama hao wamekuwa wanapungua, barani Afrika kuanzia mwaka wa 2006, kutoka 550,000 hadi 470,000 .Gazeti la "Süddeutsche" linasema walinzi wa wanyama pori wamefanikiwa kwa kiasi fulani kupunguza mauaji ya ndovu.Lakini gazeti hilo linasema, habari hizo siyo nzuri kwa wakulima wadogo wadogo wanaolima maboga na mahindi kandoni mwa hifadhi za wanyama.

Usena ndiyo "dawa " ya ndovu

Gazeti hilo linaeleza katika makala yake kwamba ndovu mmoja peke yake, anaweza kulimaliza shamba lote mara moja na kusababisha hasara kubwa kwa mkulima.

Badala ya kuwaua wanyama hao gazeti la "Süddeutsche" linafahamisha, walinzi wa wanyama pori wamempata askari hodari, anaeitwa nyuki. Gazeti linaarifu kwamba tembo anasumbuliwa sana na usena, yaani mwiba wa nyuki. Nyuki wanayalinda mashamba, na ndovu wanaepuka risasi.

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW