ANC yatuhumiwa kutaka kumuua rais Zuma
30 Machi 2024Ajali hiyo ilitokea saa chache baada ya maafisa wa uchaguzi kumzuia Zuma kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Mei 29, na hivyo kuzua hali ya mvutano. Zuma na walinzi wake walinusurika na ajali hiyo ambayo inadaiwa ilisababisha na dereva aliyekuwa amelewa.
Polisi wa Afrika Kusini wamesema gari la Zuma liligongwa na mwanaume mwenye umri wa miaka 51 ambaye amekamatwa katika Jimbo la KwaZulu Natal kwa kosa kuendesha gari akiwa amelewa na kwa uzembe barabarani.
Msemaji wa chama cha Zuma cha Umkhonto we Sizwe (MK) Nhlamulo Ndhlela amesema katika taarifa kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, Zuma amenusurika katika ajali mbili zinazowahusisha madereva wanaodaiwa kuwa walevi.
Ndhlela amesisitiza kuwa hili linaonekana kama jaribio la makusudi la kutaka kumuua Rais Zuma mwenye umri wa miaka 81, ambaye ni mwanasiasa mkongwe na mwenye ushawishi mkubwa aliyelazimika kuondoka madarakani mwaka 2018 kufuatia tuhuma za ufisadi.
Msemaji huyo ameongeza kuwa chama hicho "kimekuwa kikifuatilia kwa karibu mlolongo wa matukio yanayoshabihiana" ambayo yamemtokea Zuma chini ya utawala wa "serikali ya Cyril Ramaphosa ", mara tu baada ya Zuma kutangaza mwezi Disemba kwamba atafanya kampeni kwa tiketi ya chama cha MK katika jitihada za kufufua upya safari yake ya kisiasa.
Soma pia: ANC yamsimamisha uanachama Zuma baada ya kuunga mkono chama kipya
Binti wa Zuma, Duduzile Zuma ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa X (zamani Twitter) na kudai kuwa ajali hiyo ya gari haikuwa bahati mbaya, huku akisisitiza: "Tafadhali msituone wajinga, sisi sio wafuasi wa Ramaphosa", aliandika Duduzile.
Vitisho dhidi ya Zuma na anguko la ANC
Msemaji wa chama cha Zuma Ndhlela ameliambia Shirika la Habari la AFP kwamba Waziri anayehusika na vikosi vya polisi na msimamizi wa kitengo cha ulinzi wa rais wa zamani hajaboresha gari lake kwa miaka minane na aliwahi hapo awali kutoa ujumbe ulioashiria "kumzika Zuma".
Pia alibainisha kile alichokiita "kauli za hatari na za kizembe" zilizotolewa na wanasiasa wa ANC dhidi ya Zuma, akiwemo afisa mmoja wa mkoa aliyesema kuwa "Zuma atakuwa hospitalini kabla ya uchaguzi."
Soma pia: ANC yashindwa katika kesi dhidi ya chama cha Zuma
Wakati uchaguzi wa Mei ukikaribia, chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC, kwa mara ya kwanza tangu kilipoingia madarakani mwishoni mwa enzi za ubaguzi wa rangi mwaka 1994, kiko katika hatari ya kushuka na kutotimiza asilimia 50 ya kura. Chama hicho kimekuwa kikipoteza uungwaji mkono kutokana na matatizo ya kiuchumi, tuhuma za ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.
Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mnamo Juni, 2021 baada ya kukataa kutoa ushahidi kwa jopo lililokuwa likichunguza kuhusu vitendo vya ufisadi. Aliachiliwa kutokana na matatizo ya kiafya, miezi miwili tu baada ya kuanza kutumikia kifungo chake.
Lakini kitendo cha Zuma kuwekwa gerezani kilizusha maandamano, ghasia na uporaji ambavyo vilisababisha vifo vya zaidi ya watu 350 katika ghasia mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Afrika Kusini tangu ilipoanza kuongozwa kidemokrasia.
Alipoulizwa kuhusu hali ya Zuma baada ya ajali hiyo, Ndhlela amesema: "Ana furaha tele kama kawaida yake na alitania kuhusu ajali hiyo, lakini haimaanishi kwamba amepuuzia tukio hili au hafahamu kinachoendelea." Amemalizia kwamba Zuma alikuwa kanisani akiomba shetani asiingie kwenye chama cha MK," akimaanisha kuwa ANC ndiye shetani mwenyewe.